Sera ya Gesi: Maoni ya awali #RasimuyaGesiAsilia #TanzaniaNaturalGasPolicyby zittokabwe |
Jana
wabunge tumegawiwa rasimu ya Sera ya Gesi Asilia. Leo Wizara ya Nishati
na Madini itaendesha semina kwa wabunge kuhusu sera hiyo.
Nimepata
muda kidogo wa kuipitia hii rasimu ya 3 nikiwa safarini kwenda Tabora
kwa shughuli za chama changu cha CHADEMA , nina maoni ya awali kama
ifuatavyo;
1). Kwa
ujumla kupata Sera mpya ya gesi asilia ni hatua muafaka japo imechelewa
sana. Hata hivyo ni bora kuchelewa kuliko kutofika kabisa. Ni vema
wananchi wachukue fursa hii kuisoma na kuijadili rasimu hii na
kuiboresha ili iwezeshe wananchi wenyewe kufaidika na utajiri ambao nchi
yetu imejaaliwa.
2).
Sera ina jumla ya sura Sita. Sura ya kwanza ya inaweka sababu na
masuala ya jumla na utangulizi . Sura ya pili inaweka sababu za kuwepo
kwa sera mpya na madhumuni maalumu, Sura ya tatu ndio yenye matamko ya
msingi ya kisera (fundamental policy issues) ikiwemo masuala ya
miundombinu ya gesi kwa ajili ya soko la ndani, usimamizi wa mapato
yatokanayo na gesi asilia na masuala ya ‘’ local content’’.
Sura hii pia imezungumzia masuala ya uwazi na uwajibikaji. Sura ya nne
ni masuala ya mfumo wa kisheria na udhibiti na sura ya tano ni taasisi
za usimamizi wa sera ya gesi asilia. Sura ya sita ni hitimisho. Kila
sura imeweka matamko ya kisera.
3). Rasimu
ya sera imeshindwa kutofautisha suala la Mafuta na Gesi kuwa ni suala
la Muungano au sio suala la muungano katika muktadha wa Katiba mpya
inayojadiliwa sasa. Hii inadhihirisha umuhimu wa kuwianisha mchakato wa
katiba na michakato mingine inayoendelea nchini. Hivi sasa Zanzibar
inajiandaa kuwa na sera na sheria yao ya mafuta ya gesi, iweje sera hii
itamke gesi asilia ni mali ya Jamhuri ya Muungano wakati upande mmoja wa
Muungano utakuwa unafaidi utajiri wake peke yake? Rasimu ya sera
imeshindwa kutambua kuwa kuna vitalu vya mafuta na gesi ya (vitalu namba
9-12) vimesimamisha shughuli kwa sababu Serikali ya Zanziabar haitambui
mafuta na gesi kuwa suala la muungano. Rasimu inapaswa kuzingatia jambo
hili kabla ya kupata sera yenyewe.
4). Rasimu imetamka katika ukurasa wa 9 kwamba sera hii haitambui shughuli za utafutaji (‘This policy document only covers mid-and downstream segments’ ndio nukuu ya neno kwa neon ya Sera hii). Hiki ni kichekesho cha milenia .
Taifa
linawezaje kuandika sera ya gesi asilia kwa upande wa uchuuzi tu
(biashara) na kuacha kazi yenyewe haswa ya utafutaji na uchimbaji (exploration and exploitation are upstream). Shughuli za utafutaji na uchimbaji ndio msingi haswa wa sera ya gesi asilia.
Mikataba
yote huamuliwa kwa kuzingatia kwanza utafutaji, shughuli nyingine ni
biashara tu ya kitakachogunduliwa . Rasimu kuacha kabisa eneo la
utafutaji na uendelezaji (upstream) ni sawa na kutokuwa na sera kabisa.
Kwa
namna eneo hili lilivyoachwa kuna harufu ya mkakati wa siri wa
kuwanyima wananchi msimamo wa kisera kuhusu utajiri wao unavyonyonywa .
Sentensi hii yenye maneno 10 katika uk. wa 9 wa kijitabu cha rasimu ya
sera unaondoa kabisa umuhimu wa sera yenyewe wakati dhumuni kuu la sera
linatamkwa uk.6 kwamba Gesi asilia ni mali ya wananchi wa ‘Jamhuri ya
Muungano’ wa Tanzania’’ kurasa tatu baadaye zinaiondoa sera kwenye eneo
hilo la umiliki wa mali hii ( Upstream). Tumeamua kuandika sera ya
uchuuzi wa gesi asilia?
5). Rasimu
katika 3.2.2(uk.24) imeweka matamko ya kisera kuhusu uwazi na
uwajibikaji . Uwazi ndio eneo ambalo watanzania wengi walikuwa
wanasubiri kwa hamu sana . Usiri wa mikataba katika sekta mbali mbali
nchini ni chanzo cha ufisadi na uporaji wa utajiri wa mali yetu. Sera
hii imeJibu swala hili? HAPANA. Sera haisemi ni namna gani mikataba
itakuwa wazi kwa wananchi. Sera haisemi ni namna gani wananchi
wataiwajibisha Serikali na vyombo vyake (Accountability) kwenye masuala
ya mafuta na gesi. Sera imepiga porojo kuhusu uwazi na uwajibikaji. Bila
misingi imara ya Uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali ya gesi asilia,
sera haina maana yoyote ile.
6). Serikali ni lazima ijue kwamba hivi sasa nchi yetu nchi tajiri yenye watu masikini.[i] sera
ya gesi inapaswa kutuondoa kuwa nchi yenye laana ya rasilimali. Sera
hii haina mwelekeo huo kabisa . Sera inapaswa kuwezesha wananchi kupata
thamani ya maliasili yetu na kuwezesha matumizi mazuri ya mapato
yatokanayo na utajiri wa nchi.
Sera
yetu lazima ioneshe dhahiri kwamba gesi asilia ni mali ya wananchi na
uendelezaji na unyonyaji wa rasilimali hii utafaidisha wananchi kwanza
na kwa ruhusa yao (Prior informed Consent Principle)
sera ni lazima itamke hilo kinagaubaga.Sera ni lazima ionyeshe kuwa
katika ushindani wa soko makampuni ya mafuta na gesi asilia yatapata
faida ya halali ( normal retuns) ya uwekezaji wao na kwamba lolote linalozidi litabakia kuwa mali ya wananchi wa Tanzania.
Mkakati
wa makampuni ya mafuta na gesi asilia ni kuhakikisha taifa linapata
kiduchu na wanasaidia serikali kutoa majibu ya kipato hicho kiduchu.
Watanzania hawatakubali tena.
7).
Ni lazima tuseme kuwa tunataka utajiri wetu uwe neema kwa wananchi
wetu, na siyo laana. Maendeleo yetu yatategemea ni namna gani
tunafaidika na utajiri wetu wa maliasili kama gesi asilia. Sera ya Gesi
Asilia itujengee imani hiyo. Hii Sera (Rasimu) inapaswa iangaliwe upya
na hasa maeneo ya uwazi na uwajibikaji.
Kabwe Z. Zitto, Mb Kigoma Kaskazini
Tabora, tarehe 18 Mei 2013
No comments:
Post a Comment