JESHI la polisi mkoani Kagera linamshikilia diwani wa kata
ya Rutoro Abubakar Saidi na watu wengine sita akiwemo afisa mtendaji wa kata ya Rutoro
Japhet Kuyeyumba kwa kuhusika na tuhuma
ya kuwaua watu wanne kwa nyakati tofauti
ambao ni walinzi wa wawekezaji waliorasimishwa eneo la ardhi ya ranchi ya Kagoma ya kwa ajili ya ufugaji wa
kisasa na wa kibiashara.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kaimu
kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, kamishina msaidizi wa jeshi hilo Henry Mwaibambe alisema wanaoshikiliwa
wanatuhumiwa kufanya mauaji ya watu hao kati ya mei 17 na mei 18, mwaka huu.
Alisema tukio la kwanza la mauaji lilitokea mei 17 katika kitongoji cha
Rwamisha, kijiji na kata ya Rutoro wilayani Muleba ambapo kundi la watu
wanaokadiriwa kuwa kati ya 50 wakiwa na silaha za jadi na mapanga wakiongozwa
na diwani anayeshikiliwa na jeshi la polisi walimuua kwa kumkata koromeo
mchunga Ng’ombe James Venus (20) mlinzi wa kitalu namba 9 kinachomilikiwa na
Faustin Rutaoile.
Mwaibambe alisema diwani huyo anatuhumiwa kuwahamasisha wananchi wamuue mchungaji huyo kwa madai kuwa ameachia
ng’ombe wa mwekezaji huyo aliokuwa
anawachunga wakaingia kwenye shamba la
mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la James kuharibu mazao yake.
Aliendelea kusema kuwa tukio la pili lilitokea mei 18, mwaka
huu majira ya mchana ambapo wananchi wale wale wakiongozwa na diwani huyo
waliwaua walinzi watatu baada ya kuwazingira ambao aliwataja kuwa ni pamoja Mhidin
Yassin, Amos Richard na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Mugisha.
Kaimu kamanda huyo alisema kuwa katika tukio hilo la pili
mmoja wa walinzi aliyekuwa na bunduki aina ya shortgun alimuua mwananchi mmoja aliyemtaja kwa jina la Said
Ndyanabo (35) katika harakati za kujiokoa na hivyo kufanikiwa kutoroka toka
mikononi mwa wauaji.
Alisema mauaji yote yalitekelezwa kwa staili ya pekee ambapo
wauaji walikuwa wakiwaua walinzi kwa kuwakata makoromeo na kuwakata sehemu mbalimbali za miili
yao.
Alimaliza kwa kuwaambia waandishi wa habari kuwa uchunguzi
wa awali unaonyesha kuwa mauaji yote
yaliyotekelezwa yalikuwa yamepangwa chini uongozi wa mheshimkiwa diwani ambaye
jeshi la polisi linamshikilia kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa ngazi
ya kijiji cha Rutoro.
Watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kwa
tuhuma ya kuhusika na mauaji ni pamoja na James Kabeba (51), Andrew Lucas (45),
Dawson Sylivester (26), Ernest Reuben na Ancheleus Kahatano (65) wote wakazi wa
kijiji na kata ya Rutoro.
No comments:
Post a Comment