*Asema Serikali hii siyo ya watu wapole
WAZIRI
MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha
kila kinachokusanywa kama mapato ya nchi kinatumika kwa maslahi ya Watanzania
wote na si kwa manufaa ya wachache.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Novemba 29, 2015) wakati akifunga maadhimisho
ya miaka 20 ya Dayosisi ya Pwani ya Kanisa la African Inland Church Tanzania
(AICT) kwenye ukumbi wa PTA, viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Serikali
imeanza kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali na kuepuka matumizi yasiyo
ya lazima ya fedha za umma. Nia yetu ni kuhakikisha kila kinachopaswa
kukusanywa kama mapato ya nchi, kikusanywe na kitumike kwa masuala ya msingi
kwa ustawi wa Watanzania wote na si kwa watu wachache,” alisema.
Akifunga
maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu
alisema Serikali imedhamiria kupambana na maovu yote na kuondoa kero
zinazowaumiza wananchi wa kawaida. “Wako watu wanaoamini kwamba hatuwezi,
nawaomba waondoe hiyo dhana. Wako watu wanaodhani kwamba kwamba utawala huu ni
wa watu wapole, nao pia waondoe hiyo dhana,” alisema huku akishangiliwa na
mamia ya waumini waliohudhuria sherehe hizo zilizoanza Novemba 27, 2015.
“Tunawaomba
Watanzania wote mtuunge mkono kwenye vita hii na mtuwezeshe kuifanya kazi hiyo.
Tunaomba waumini wote mtuombee katika sala zenu za kila siku ili tuweze kuongoza
kwa haki na kuwaletea Watanzania wote maendeleo,” aliongeza.
Akinukuu
kitabu cha Mithali sura ya 29 mstari wa pili, Waziri Mkuu alisema: “Wenye haki
wakiwa na amri, watu hufurahi, bali mwovu atawalapo, watu huugua. Mtuombee
viongozi wenu tuwe waadilifu na wenye kutenda haki. Nasi tutaendelea kuwa waadilifu
ili watu wetu wasigue,” alisema.
Aliwataka
viongozi wa kanisa hilo waendelee kuisaidia Serikali katika kujenga kundi la
watu wenye maadili mema ili walisaidie Taifa kuwa na watu waadilifu na hivyo kupunguza
kero nyingi zinazoikabili jamii.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na waumini wa kanisa la hilo kutoka mikoa mbalimbali, Askofu Mkuu wa
Kanisa la AICT, Askofu Silas Kezakubi alisema Kanisa hilo litaendelea kumuombea
Rais Dkt Magufuli na viongozi wenzake ili wawe na afya njema, wawe na hekima na
kuahidi kwamba wataendelea kuwaweka chini ya ulinzi wa Mungu siku zote.
Alisema
wao kama kanisa wanaamini kwamba Serikali ya awamu ya tano ina nia ya
kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu lakini akasisitiza kuwa siri ya
bidii na uadilifu inapatikana kwenye neno la Mungu.
Akisoma risala ya kanisa hilo, Askofu wa AICT
Dayosisi ya Kibaha, Askofu Charles Salalah alisema kanisa halina budi
kushirikiana na Serikali kwa sababu wote wanawahudumia watu walewale isipokuwa
katika malengo tofauti.
Alisema
kanisa hilo linahubiri maadili mema na bidii katika kazi kwa vile linaamini
kuwa maendeleo hayadondoki kutoka juu wala hayaoti kama uyoga bali yanapatikana
kwa watu kufanya kazi.
Akisisitiza
kuhusu uadilifu, aliwataka wazazi kudumisha ndoa zao ili watoto wapate malezi
mema kutoka kwa baba na mama na kwamba baba na mama wasipokaa vizuri, watoto
hawawezi kuwa waadilifu.
“Wazazi
tunao wajibu wa kupanda mbegu bora ya uzalendo kwa watoto wetu. Endapo
tutapanda mbegu mbaya ya kuwagawa watoto wetu kwa itikadi tofauti, ni lazima
tujue kuwa tutavuna tunachopanda.”
“Tukumbuke
kuwa tunalo Taifa moja tu la Tanzania. Hata kama watoto wetu watakuwa na upenzi
na vyama vyao, ni lazima tuwalee katika misingi ili wakue wakijua Taifa letu ni
moja tu. Ndiyo maana tunaweka mkazo kwenye familia kwa sababu maadili mema
yanaanzia nyumbani,” alisisitiza.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA
WA MAGOGONI,
No comments:
Post a Comment