Tuesday, July 19, 2016

MAJALIWA: MALIASILI NA UTALII JIPANGENI VIZURI



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii
kujipanga vizuri na kufanya mapitio ya idara zake hususan ya misitu baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo makubwa.
“Eneo la misitu limekuwa na matatizo makubwa, watendaji wengi si waaminifu na sura ya wizara si nzuri miti mingi inakatwa na fedha haiingii Serikalini. Huu ni mgogoro mpya,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana alipokutana na watumishi wa wizara hiyo jana (Jumatatu, Julai 18, 2018) jijini Dar es Salaam, na kusisitiza kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasiokuwa na uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.
Alisema lengo la mkutano huo ni kukutana na watumishi
kusikiliza changamoto zao, kukumbushana wajibu, pamoja na kutoa maagizo ili
yatekelezwe kwa utaratibu unaokubalika kisheria.

Alisema mtumishi ambaye atabainika kuwa haitendei haki nafasi yake kwa
kutokutimiza majukumu ipasavyo hana sababu ya kuwepo kwa sababu serikali
inapoteza fedha nyingi kuwalipa watu wasio na tija.

Waziri Mkuu alisema sababu inayoikosesha Serikali mapato ni
uwepo wa watumishi wasio waadilifu kwenye ofisi za Serikali ikiwemo Wizara
ya Maliasili na Utalii hivyo kuna umuhimu wa kuzisafisha.

Alisema kuna uvunaji mkubwa wa misitu kuliko upandaji huku asilimia 50 ya mapato yatokanayo na uvunaji huo yanapotea na kuisababishia Serikali hasara ambapo alihoji sababu ya wizara kushindwa kusimamia jambo hilo.

Katika hatua nyingine; Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya
misitu kwenye barababara mbalimbali baada ya kukosa tija kutokana na upotevu wa misitu unaotokea kila siku.

Alitoa mfano wa barabara ya kwenda mikoa ya kusini  kuanzia Dar es Salaam
ambapo alisema ina vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa.

“Vizuizi vya katikati ya safari havina umuhimu na badala yake kuwe
na vizuizi mwanzo na mwisho ili rasilimali zingine zitumike kuongeza nguvu
na umakini wa ukaguzi kwenye vituo vichache vitakavyosalia,”.

“Kwa mfano ukitokea Ikwiriri kuja Dar, kuna vituo vya ukaguzi wa maliasili
visivyopungua sita, kuna Ikwiriri, Kibiti,  Jaribu Mpakani,Mkuranga, Vikindu  kote huku
wanakagua lakini linapofika kituo cha mwisho cha Mbagala linakutwa na makosa kwenye mzigo kwanini’’?

“Yule mkaguzi wa kwanza alifanya kazi gani? Kuna tatizo la uadilifu na
ninyi ni mashahidi, sasa naagiza ongezeni nguvu kwenye vituo vikuu vya
ukaguzi yaani mwanzo na mwisho,” alisema.

Aidha alisema ni muhimu kukawa na mabadiliko kwenye mfumo wa mauzo ya
misitu kutoka wa sasa (kuuza kwa eneo) na kuhamia kwenye mfumo wa mnada
ambao utaongeza mapato ya Taifa na utaweka uwazi.

Pia aliwataka watumie mashine za malipo za kielektroniki (EFD),wanapofanya mauzo ya mazao ya misitu ili
kuepusha matumizi ya daftari na risiti bandia ambazo hazitambuliwi na
wizara.

No comments:

Post a Comment