Thursday, May 23, 2013

AFISA USHIRIKA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA RUSHWA



TAASISI ya  kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera  imemfikisha mahakamani  kaimu afisa ushirika wa wilaya ya Misenyi  Bi. Faustina Majala (52) kwa makosa  kumi ya rushwa na kughushi  nyaraka.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na mkuu wa TAKUKURU mkoani Kagera Laulent Ndalichako, mtuhumiwa huyo alifikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Bukoba  Sylivia Rushasi mei 20, mwaka huu.

Katika taarifa hiyo Ndalichako alisema mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya mei 26, mwaka 2007 na mei 27, mwaka 2008, alisema mtuhumiwa huyo alitenda makosa ya rushwa na kughushi  kwa kutumia madaraka yake ya ukaimu wa nafasi afisa ushirika wa wilaya ya Bukoba, mjumbe wa mkutano mkuu wa chama cha ushirika Kagera (KCU) na  mkuu wa vyama vya ushirika vya msingi wilayani Bukoba.

Ndalichako alisema TAKUKURU kupitia kwa mwendesha mashtaka wakeRonald Manyiri  ilimsomea pia mtuhumiwa makosa matatu ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri  wake kinyume na kifungu  cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa .

Alisema mtuhumiwa amekana mashtaka yote hivyo yuko nje kwa dhamana ambapo kesi yake itatajwa tena juni 5, mwaka huu.


No comments:

Post a Comment