Tuesday, January 05, 2016

WAZIRI MKUU AKAGUA JENGO LA MAKAO MAKUU YA HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wialaya ya Songea lilipo katika kijiji cha Lundusi, Wilaya ya Peramiho mkoani Ruvuma.

Alipowasili  jana katika eneo hilo alikutana na viongozi wa jadi ambapo  Mzee Daniel Gama  alimkabidhi  ngao na silaha ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kijijini hapo, pia alipata fursa ya kutazama ngoma ya mila ya kabila la Wangoni.

Mara baada ya kukagua jengo hilo  la ghorofa,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lundusi Bwana Rajabu Mtiula amesema jengo hilo lenye  ofisi 50, vyoo 4, ukumbi mkubwa 1 na kumbi ndogo 2, ambapo mradi huo umetekelezwa kwa fedha za mfuko wa Mradi wa Maendeleo na Serikali. Hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha zaidi ya  shilingi bilioni 200 na utekelezaji wake umekamika kwa 85%, hivyo wanatarajia kuanza kutumia jengo hilo mwezi Februari, 2016.

Akizungumza  jana  (Jumatatu, Januari 4, 2016)  na wananchi wa kijiji cha Lundusi, Waziri Mkuu, amewapongeza   wananchi  wa Lundusi kwa hatua hiyo ya maendeleo na kusema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono ujenzi wa jengo hilo.

Waziri Mkuu Majaliwa, ametaka kuwepo na mikakati ya uboreshaji wa eneo hilo kwa kusogeza huduma karibu ili kuvutia watu zaidi katika eneo hilo.

Naye, Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Uratibu, Ajira na Walemavu  Jenista Mhagama  ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na Waziri Mkuu kwa kuchaguliwa na kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia, ameishukuru Serikali kwa kusaidia kujenga jengo hilo, na pia ameeleza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo ikiwemo wakulima kutofaidika kwa bei ya soko ya kuuza mahindi, kutokuwepo na umeme na maji.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Waziri Jenista kufuatilia kero hizo kwa Wizara husika na baadae kuleta mrejesho kwa wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa anaendelea na ziara mkoani Ruvuma, leo siku ya jumanne (Januari 5, 2016)  atatembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuongea na Watumishi wa hospitali hiyo  na baadae ataongea na Watumishi wa Umma.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment