WAKANDARASI wazalendo hapa nchini wameshuriwa kuimarisha umoja unaowaunganisha  ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowakabili zinazokwamisha katika mchakato wa kushinda zabuni.
 
Hayo yameelezwa na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya TEKI mhandisi Emmanuel  Bishanga ambaye pia ni katibu wa umoja wa kandarasi wa mkoa wa Kagera  (TASEKA)  wakati akitolea  ufafanuzi malalamiko  yanatolewa na  baadhi ya wakandarasi wanaodai kuwa zabuni za ujenzi wa barabara zinatolewa kwa upendeleo hasa  kwa makandarasi  wenye uwezo mkubwa.
 
Bishanga amesema  umoja wa wakandarasi unapokuwa hai unaweza kuleta wawekezaji wenye mitambo mikubwa ya ujenzi ambayo ambayo wakandarasi wenye uwezo mdogo wanaweza kuikodisha  tofauti na utaratibu wa sasa ambao wakandarasi  wanaitumia wa kukodi mitambo toka kwa makandarasi wenye uwezo mkubwa wanaoshindana nao zinapotangazwa zabuni.
 
 
Alisema  si kweli kwamba TANROADS inatoa zabuni za ujenzi wa barabara kwa upendeleo hasa kwa wakandarasi wakubwa, Bishanga alisema wakala hao wa barabara wanatoa zabuni kwa kuangalia vigezo vingi.
 
"Ndugu mwandishi kawaida zabuni ufunguliwa mbele ya wakandarasi wote wanaokuwa wameomba kazi, zikifunguliwa kila ombi moja moja uchambulisha hapo ndipo mshindi wa zabuni utangazwa" mhandisi huyo.
 
"Mimi siwatetei maofisa wa  TANROADS wanaogawa zabuni  ninachokisema kulingana na uzoefu nilionao kwamba wanaonyimwa zabuni ni makandarasi wasio na sifa ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara, makandarasi wasio na sifa ni wale wasio na mitaji, vitendea kazi na wsenye sifa za kutokuwa waaminifu hasa katika kukamilisha kazi wanazopewa" alisema Bishanga.
 
Naye Manyus Rweyendelela ambaye pia ni mkandarasi aliwaomba wakandarasi watimize vigezo vyote vinavyotakiwa wakati wa kuomba zabuni.
 
"Sio siri taarifa zinazoenezwa za kuichafua TANROADS  zinaenezwa na makandarasi wanakosa tenda kwqa kushindwa kutimiza vigezo" Alisema.
 
"Mimi ni mkandarasi mdogo ila huwa ninaomba kazi TANROADS, wakati mwingine nakosa wakati mwingine napata, nasema tangu nianze kuomba zabuni TANROADS sijawahi kutoa rushwa ili nishinde zabuni, wanaoeneza taarifa za upotoshaji wana mawazo mufilisi" alisema Manyus.
 
Kwa upande wake Julius Basinda alisema ndani ya TANROADS hakuna  namna mkandarasi anaweza kushinda zabuni kwa kutoa rushwa siku ya kufungua zabuni kila kitu huwekwa hadharani.
 
"Ninachosema ushindi wa zabuni ni kutimiza vigezo, ndugu zangu wakandarasi msijidanganye kwa kufikiri kwamba mtashinda zabuni kwa maneno au kwa kutumia rushwa hali hiyo ilishabadili siku nyingi" alimaliza.