Tuesday, January 05, 2016

WAZIRI MKUU AKAGUA MAGHALA YA WAKALA WA HIFADHI YA TAIFA YA CHAKULA (NFRA) KANDA YA SONGEA


Waziri Mkuu  Kassim  Majaliwa amekagua  maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea, wakati akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma.

Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala hiyo, wadau wa kilimo pamoja na wananchi jana, (Jumatatu, Januari 4, 2016) nje ya majengo ya Wakala mara baada ya kukagua mahindi yaliyohifadhiwa katika maghala  ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , mkoani Ruvuma amesema  kufuatia taarifa ya kuwepo na baadhi ya maeneo yenye njaa nchini, Serikali imetoa tamko kuwa hakuna mtanzania atayakekufa kwa njaa.

Ambapo, Serikali  kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa imeweka mikakati ya  kukabiliana na  tatizo la  njaa kwa kutoa msaada wa chakula katika maeneo yanayokabiliwa na njaa.

 “Ni wajibu wangu kuhakikisha nasimamia vizuri hili, nimeona hali ya uhifadhi  wa chakula, tunayo mahindi ya kutosha lakini hakuna sehemu ya kuhifadhi chakula” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kwa kusema uwezo wa maghala hayo yaliyopo chini ya Wakala Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea yana uwezo wa kuhifadhi tani 29 pekee   na Songea  inauwezo wa kuzalisha zaidi tani 70 hadi 80.

Pia , ameagiza  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , kuanzia mwaka huu kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa pamoja Wakuu wa Wilaya  kuanzisha  vituo vya kununulia mahindi  na kuhakikisha magunia yanawafikia wakulima katika vituo hivyo ambapo wataweza kuhifadhi mahindi  na  kuuza  kwa bei ya kwenye soko.

Waziri Mkuu  pia, ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea ,kutumia teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa chakula, kuandaa utaratibu maalum utakaozuia msongamano wa  malori  yanayosubiri kupata huduma ya kununua mahindi  nje ya majengo ya Wakala na kukamilisha miradi itakayosaidia Wakala kuwa na fedha za kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Meneja Hifadhi wa  Chakula kanda ya Songea, Bwana. Morgan Mwaipaya amesema kati ya maghala 33 ya kuhifadhi mahindi nchi nzima, Songea ina maghala 6 kati ya hayo. Hivyo, Wakala imeweka vipaumbele vyake ambavyo ni  pamoja na kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yenye matatizo ya njaa, kuongeza upatikanaji wa mahindi ili kuzuia kupanda kwa bei ya chakula mwaka 2015 – 2016, Wakala kununua na kuhifadhi  mahindi katika maeneo yaliyozalisha zaidi na kuzingatia sehemu ya sehemu ya akiba ya chakula na kuuza kwa wakulima, mawakala pamoja na Wakala wa Chakula duniani (World food program).

Amesema Wakala imeandaa mikakati ya mbalimbali ikiwemo  kuongeza  uwezo  wa tani 24600 hadi tani  45000 kwa mwaka 2014- 2017, kuboresha mfumo wa utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya stahili ya TEHAMA na kutumia fursa za mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha ili kuendesha shughuli za uwezeshaji I kiwemo kuelimisha taratibu za ununuzi kwa mawakala.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Songea, Mheshimiwa Leonidas Gama amesema   wakulima wachache wamekua wakiuza mahindi yao kwa bei ya soko,  wengi wao wamekua wakiuza mahindi kwa mawakala kwa bei ya shilingi 150 hadi 200  kwa kilo na  wakala wakiuza kwa shilingi 500 kwa Serikali. Ambapo amemuomba  Waziri Mkuu  kutatua tatizo la soko la mahindi kwa wakulima. Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima kuendelea kuzalisha mahindi akiahidi Serikali kununua mahindi hayo kwa bei ya soko  ambayo itamnufaisha mkulima.

Waziri Mkuu Majaliwa anaendelea na ziara mkoani Ruvuma, leo siku ya jumanne(Januari 5, 2016)  atatembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuongea na Watumishi wa hospitali hiyo  na baadae ataongea na Watumishi wa Umma.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

No comments:

Post a Comment