Tuesday, July 19, 2016

MAJALIWA: MALIASILI NA UTALII JIPANGENI VIZURI



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii
kujipanga vizuri na kufanya mapitio ya idara zake hususan ya misitu baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo makubwa.
“Eneo la misitu limekuwa na matatizo makubwa, watendaji wengi si waaminifu na sura ya wizara si nzuri miti mingi inakatwa na fedha haiingii Serikalini. Huu ni mgogoro mpya,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana alipokutana na watumishi wa wizara hiyo jana (Jumatatu, Julai 18, 2018) jijini Dar es Salaam, na kusisitiza kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasiokuwa na uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.
Alisema lengo la mkutano huo ni kukutana na watumishi
kusikiliza changamoto zao, kukumbushana wajibu, pamoja na kutoa maagizo ili
yatekelezwe kwa utaratibu unaokubalika kisheria.

Alisema mtumishi ambaye atabainika kuwa haitendei haki nafasi yake kwa
kutokutimiza majukumu ipasavyo hana sababu ya kuwepo kwa sababu serikali
inapoteza fedha nyingi kuwalipa watu wasio na tija.

Waziri Mkuu alisema sababu inayoikosesha Serikali mapato ni
uwepo wa watumishi wasio waadilifu kwenye ofisi za Serikali ikiwemo Wizara
ya Maliasili na Utalii hivyo kuna umuhimu wa kuzisafisha.

Alisema kuna uvunaji mkubwa wa misitu kuliko upandaji huku asilimia 50 ya mapato yatokanayo na uvunaji huo yanapotea na kuisababishia Serikali hasara ambapo alihoji sababu ya wizara kushindwa kusimamia jambo hilo.

Katika hatua nyingine; Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya
misitu kwenye barababara mbalimbali baada ya kukosa tija kutokana na upotevu wa misitu unaotokea kila siku.

Alitoa mfano wa barabara ya kwenda mikoa ya kusini  kuanzia Dar es Salaam
ambapo alisema ina vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa.

“Vizuizi vya katikati ya safari havina umuhimu na badala yake kuwe
na vizuizi mwanzo na mwisho ili rasilimali zingine zitumike kuongeza nguvu
na umakini wa ukaguzi kwenye vituo vichache vitakavyosalia,”.

“Kwa mfano ukitokea Ikwiriri kuja Dar, kuna vituo vya ukaguzi wa maliasili
visivyopungua sita, kuna Ikwiriri, Kibiti,  Jaribu Mpakani,Mkuranga, Vikindu  kote huku
wanakagua lakini linapofika kituo cha mwisho cha Mbagala linakutwa na makosa kwenye mzigo kwanini’’?

“Yule mkaguzi wa kwanza alifanya kazi gani? Kuna tatizo la uadilifu na
ninyi ni mashahidi, sasa naagiza ongezeni nguvu kwenye vituo vikuu vya
ukaguzi yaani mwanzo na mwisho,” alisema.

Aidha alisema ni muhimu kukawa na mabadiliko kwenye mfumo wa mauzo ya
misitu kutoka wa sasa (kuuza kwa eneo) na kuhamia kwenye mfumo wa mnada
ambao utaongeza mapato ya Taifa na utaweka uwazi.

Pia aliwataka watumie mashine za malipo za kielektroniki (EFD),wanapofanya mauzo ya mazao ya misitu ili
kuepusha matumizi ya daftari na risiti bandia ambazo hazitambuliwi na
wizara.

MAJALIWA: BARA LA AFRIKA BADO LINAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA UPATIKANAJI WA MAJI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hasa vijijini kwa sababu nchi zake bado hazijamudu kuunganisha huduma hiyo katika maeneo hayo.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa masuala ya maji watafute njia sahihi itakayowezesha kutatua tatizo hilo kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya maji vilivyoko.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Julai 18, 2016) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere  jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (AMCOW) ambao unaokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Maji Afrika.
“Tunategemea baada ya kumazika kwa mkutano huu wataalamu wetu wataondoka na maazimio mazuri ya kumaliza tatizo la maji katika Bara letu kwa kutumia mito na maziwa ili kufikisha maji kwa wananchi,” alisema.
Akizungumzia kwa upande wa Tanzania alisema,  suala la maji limepewa kipaumbele hata katika bajeti ya mwaka huu na kwamba Serikali itahakikisha maji yanapatikana katika maeneo yote ili kutimiza sera yake ya kila mwananchi kupata maji umbali usiozidi mita 400.
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki ambaye ni Mjumbe Maalumu wa UNESCO kwa ajili ya masuala ya maji Barani Afrika alisema maji ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi, hivyo wataalamu wanatakiwa kuhakikisha huduma hiyo inapatika katika maeneo yote.
Mkutano huo  wa siku tano unahudhuriwa Mawaziri wa Maji kutoka nchi 45 za Afrika na unaongozwa na Waziri wa Maji na Mazingira wa Senegal Amadou Mansour Faye ambaye ni Rais wa AMCOW.
(mwisho)
 

NSSF YACHANGIA MILIONI 50 HARAMBEE YA UJENZI MPYA WA LINDI SEKONDARI


Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Jamii NSSF Makao Makuu ikishirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Lindi Imechanga Jumla ya Shilingi Milioni 50 Kwa Ajili ya Kuchangia Harambee ya Kusaidia Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Lindi Iliyoungua Moto Wiki Iliyopita
Kwa Kutambua Umuhimu wa Elimu kwa  Watoto Shirika Hilo Kupitia Mkurugenzi Mkuu Wake ,Aliewakilishwa na Meneja wa Mkoa Bi Nour Aziz Limetoa ahadi hiyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Majaliwa Kasim Majaliwa Alieongoza Harambee Hiyo Ambayo Ilihudhuriwa na Wadau Mbali mbali Akiwemo Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,Mama Salma Kikwete
Katika Harambee Hiyo Jumla ya Shilingi Milioni 80 Taslimu zilichangwa Huku Ahadi na Vifaa vya Ujenzi zikifikia Shilingi Milioni 640 Ambapo Katika Ujenzi Mpya Waziri Mkuu Ameagiza Kujengwa Jengo la Ghorofa litakalokuwa na Ofisi na  Madarasa
Katika Tukio Hilo la Moto,Jumla Ya Madarasa 9 na viti na Meza zaidi ya 300,Ofisi 4 na Vyoo Matundu 24  Viliteketea na Moto Uliotokana na hitilafu ya Umeme

MAJALIWA: MARUFUKU WANAFUNZI KUTUMIA VIBERITI, MISHUMAA MABWENINI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na hita za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.
“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Waziri Mkuu amesema kwa namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema yakavunjwa na kujengwa upya ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga madarasa mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, mama Salma Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na wanafunzi waliosoma shule hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali nchini kufunga vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia pindi ajali za moto zinapotokea.
(mwisho)
 IMETOLEWA NA: