Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo ya jinsi mashimo yatayosimikwa nguzo za daraja hilo yanavyochimbwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake inakaribia
kukamilisha ujenzi wa madaraja yote 10 yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2010 na ambayo yanagharimu mabilioni ya fedha.
Rais Kikwete amesema kuwa kati ya madaraja hayo
ambayo thamani yake inakaribia sh. bilioni 415, madaraja mawili tayari ujenzi
wake umekamilika. Madaraja hayo ni lile la Ruhekei lililoko Wilaya ya Mbinga
katika Mkoa wa Ruvuma na Daraja la Mwatisi katika Mkoa wa Morogoro.
Rais Kikwete amesema kuwa madaraja mengine saba
yanaendelea kujengwa, ikiwa ni pamoja na
Daraja la Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam linalogharimu sh bilioni 214.6,
Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, Mkoa wa Kigoma unaogharimu sh bilioni
90.185, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro linalogharimu sh bilioni 53.214
na Daraja la Rusumo, Mkoa wa Kagera linalogharimu sh bilioni 31.7.
Madaraja mengine yanayoendelea kujengwa ni Daraja
la Sibiti, Singida, linalogharimu sh
bilioni 17.5, Daraja la Nangoo, Mkoa wa Mtwara linalogharimu sh bilioni 4.29 na
Daraja la Maligisu, Mwanza, linalogharimu sh bilioni 2.51.
Amesema Rais Kikwete: “Madaraja niliyotaja ujenzi
wake ukikamilika, tutakuwa tumetimiza ahadi yetu ya kujenga madaraja yote
yaliyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 isipokuwa Daraja la Ruhuhu
ambalo maandalizi yake ya ujenzi yanaendelea.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumza wakati anaweka
jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mbutu, Wilaya ya Igunga, Mkoa
wa Tabora katika sherehe ya kufanya iliyofanyika Jumatatu, Januari 7, 2013.
Rais Kikwete amesema kuwa baadhi ya madaraja
yanayojengwa sasa na Serikali yalipangwa kujengwa katika Mpango wa Pili wa
Taifa wa Maendeleo mwaka 1968 lakini kwa bahati mabaya hayakuweza kujengwa.
Madaraja hayo ni Daraja la Kigamboni, Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja
la Rufiji, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro na Daraja la Kikwete kwenye
Mto Malagarasi.
Awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu ilijenga
Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Awamu na pili ikafanya maandalizi na Awamu ya
tatu ikajenga Daraja la Rufiji na Awamu ya sasa inajega madaraja matatu
yaliyobakia – Kilombero, Kigamboni na Kikwete.”
Daraja la Mbutu lina urefu wa kilomita tatu, na
linajengwa katika Bonde la Mbutu na litaunganisha mikoa ya Tabora, Singida,
Simiyu na Shinyanga.
Daraja hilo litakuwa na daraja moja kubwa la mita
60 na madaraja mengine madogo saba na hivyo kufanya urefu wa daraja lote kuwa
na mita 165. Mpaka sasa asilimia 45 ya ujenzi wa daraja hili lenye thamani ya
sh bilioni 11.28 umekamilika na inakadiriwa kuwa litakuwa tayari ifikapo
Novemba mwaka huu.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
No comments:
Post a Comment