Wednesday, September 18, 2013

Washukiwa wa shambulizi la tindikali wakamatwa


 
Kasisi aliyeshambuliwa kwa tindikali Zanzibar akiendelea kupokea matibabu
Polisi visiwani Zanzibar, wamewakamata watu 15 wanaoshukiwa kuhusika na mashambulizi ya tindikali visiwani humo.
Mkuu wa polisi nchini humo, Mussa Ali Mussa, alidai kuwa baadhi ya washukiwa wana uhusiano na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab nchini Somalia.
Wiki jana kasisi wa kanisa katoliki alishambuliwa kwa kumwagiwa tindi kali katika mji wa kale.
Shambulizi hilo linakuja baada ya wasichana wawili wa uingereza kushambuliwa mwezi jana.
Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18, walimwagiwa tindi kali wakiwa wanatembea mjini humo.
Maafisa nchini Zanzibari, wametangaza kumzawadi mtu atayetoa taarifa kuhusu shambulizi hilo.
Katika shambulizi lililofanyika siku ya Ijumaa, kasisi Joseph Anselmo Mwangamba alimwagiwa tindi kali alipokuwa anaondoka kwenye duka la huduma za internet katika mji wa kale.
Shambulizi hilo ni la tano la aina yake visiwani humo tangu Novemba mwaka jana.
Bwana Mussa alisema kuwa polisi walinasa mitungi iliyokuwa na lita 29 za Tindi kali wakati wa msako wao.
Kwa mujibu wa polisi, washukiwa walikamatwa wakiwa katika harakati za kujiandaa kwa mapigano kwengineko nje ya Tanzania.
Hadi sasa polisi wanakamilisha uchunguzi wao kabla ya kuwafungulia mashtaka washukiwa watatu waliowashambulia wasichana wawili raia wa Uingereza.
Hata hivyo haijulikani ikiwa washukiwa hao 15 waliokamatwa wamehusishwa na shambulizi walilofanyiwa wasichana hao wawili au ikiwa ni wao waliomshambulia kasisi Mwangamba.
Visiwa vya Zanzibar hupokea watalii wengi na wenyeji wansema kuwa mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni sio jambo la kawaida.

No comments:

Post a Comment