Monday, September 23, 2013

SERIKALI KUPELEKA MAGUNIA 200,000 YA MAHINDI NGORONGORO - WAZIRI MKUU






WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itahakikisha inawapatia chakula cha uhakika wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro wakati ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa wakazi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili waweze kujikimu.

Amesema ili kukabiliana na tatizo la njaa linalowakabili wakazi wa tarafa hiyo, kwa kuanzia Serikali itaipatia kila kaya magunia matano kila baada ya miezi sita wakati ikitafuta suluhisho la kudumu la tatizo la njaa linalowakabili wakazi hao wanaokadiriwa kufikia kaya 20,000.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Septemba 19, 2013) wakati akizungumza na wakazi wa kata saba za Tarafa ya Ngorongoro katika mkutano wa hadhara uliofanyika Enduleni Madukani wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Alikuwa akijibu maswali yaliyoulizwa na wakazi zaidi ya 10 wa tarafa hiyo ambao walipewa fursa ya kuuliza maswali ambapo wengi wao walitaka Serikali iwaruhusu kulima mashamba ya kujikimu katika maboma wanayoishi ambayo yamo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

“Nimelitazama jambo hili kwa kina, najua wengi mnataka kusikia habari ya kulima kwenye mashamba ya kujikimu lakini mimi nina pendekezo la tofauti. Serikali ichukue hatua ya kuwapatia chakula cha uhakika wakati jambo hili likiangaliwa kwa undani katika ngazi mbalimbali,” alisema.

“Nimeelezwa kuwa kuna kaya karibu 20,000 na kila kaya ina watu karibu watano hadi sita, tukiamua kutoa magunia matano kwa miezi sita ni sawa na tani 10,000 na miezi sita mingine tukawapa magunia matano tutakuwa tumetatua tatizo la njaa kwa kila kaya. Hili ni jambo ambalo Serikali inaweza kulifanya kwa sababu mmetusaidia kutunza hifadhi hii,” alisema.

Waziri Mkuu aliwaahidi wakazi hao kwamba suala la kuwa na mashamba madogo ya kujikimu litajadiliwa kwa pamoja baina ya Baraza la wafugaji na Bodi ya Ngorongoro ambayo inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.

“Suala la mashamba ya kujikimu halitaki kutolewa kauli za pupa, inabidi tukae na Baraza la Wafugaji tuone tunapataje njia ya kudumu ya kutatua tatizo hili. Kila aliyekuja hapa anataka shamba la kujikumu nilipodadisi nikapata picha kuwa ni mashamba madogo. Sasa ni lazima tukae na Malaigwanan na Baraza lenu ili tujue kama tunaruhusu mashamba ni ya ukubwa gani na ni mazao gani yalimwe katika hayo mashamba...,” alisisitiza.

Aliwakumbusha wakazi hao umuhimu wa kutunza hifadhi hiyo ya Ngorongoro ambayo imejizolea sifa duniani kote na imepata fursa ya kuwa miongoni mwa maajabu saba ya dunia katika Bara la Afrika.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, kabla ya kuhutubia mkutano huo aliamua kukutana na Baraza la Wafugaji pamoja na wazee wa kimila (Malaigwanan) na kusikiliza baadhi ya kero kutoka kwa wazee hao.

Waziri Mkuu alisema anatambua taabu inayowapata wakazi hao kwani katika tathmini iliyofanyika mwezi Julai hadi Agosti 2013 juu ya hali ya watu na uchumi katika tarafa ya Ngorongoro imebainika kuwa tarafa hiyo inakabiliwa na umaskini wa kipato unaosababishwa kutegemea ufugaji kama njia kuu ya uchumi.

Kwa mujibu wa tathmini hiyo, tarafa ya Ngorongoro ina wakazi 87,851 kwenye jumla ya kaya 19,908 ikiwa na idadi ya ng’ombe 131,509; mbuzi 163,207 na kondoo 166,872. Hata hivyo, hali ya uchumi wa mifugo imeendelea kushuka kwani ni asilimia tatu (3%) pekee ya wenyeji wa Hifadhi ya Ngorongoro wanamiliki asilimia zaidi ya 80 ya mifugo yote iliyopo kwenye tarafa hiyo wakati asilimia 97 ya wenyeji ndio wanaomiliki asilimia 20 ya mifugo yote.

Tathmini hiyo ilifanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa alipokutana na Malaigwanan pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafugaji la Ngorongoro jijini Arusha na mjini Dodoma Juni mwaka huu.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Karatu na kesho atakwenda Weruweru, Moshi kwenye Jubilei ya miaka 50 ya shule hiyo ya sekondari.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, SEPTEMBA 20, 2013.



--

No comments:

Post a Comment