Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefungua shule ya kisasa ya msingi ya Ntulya katika kata ya Mondo,
Wilaya ya Misungwi, iliyotolewa kama zawadi kwa wanakijiji cha Ntulya na
taasisi moja ya Marekani.
Aidha, Rais Kikwete
amezindua huduma za x-ray kwenye Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mjini Misungwi
ikiwa ni hatua zake za mwanzo kwenye siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Rais
Kikwete katika mkoa wa Mwanza ambako atakaa siku tano akikagua na kuzindua
miradi na shughuli za maendeleo.
Shule ya Ntulya
iliyoko kilomita 47 kutoka mjini Misungwi ina wanafunzi 466 na walimu 11 na ni
zawadi ya Taasisi ya Africa School House ya Marekani kwa wanakijiji cha Ntulya
ambako Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt. Aimee Bessire ambaye
amehudhuria sherehe za uzinduzi wa shule hiyo na mume wake, Mark Bessire
walipata kuishi wakifanya utafiti kuhusu utamaduni wa Kabila la Wasukuma.
Shule hiyo ya kisasa
imejengwa kwa matofali ya kuchomwa na ilijengwa kati ya 2008 na 2010. Ina
madarasa 11, nyumba 10 za walimu na kisima cha maji safi. Kwa jumla shule hiyo
ina uwezo wa kuwa na wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.
Akizungumza kwenye
sherehe za leo, Dkt. Bessire ambaye amezungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza,
Kiswahili na Kisukuma, amesema kuwa shule hiyo imejengwa kwa jumla ya sh
bilioni 1.038, na kati ya hizo sh milioni 980 zilitolewa na Africa School
House, Halmashauri ya Misungwi ilichangia sh milioni 28 na nguvu za wananchi
zilichangia sh milioni 30.
Taasisi hiyo ya
Marekani pia imewajengea wanakijiji hao wa Ntulya Kituo cha Afya kwenye eneo
hilo la shule na Dkt. Bessire amesema kuwa Taasisi hiyo ina mipango ya kujenga
shule ya mfano ya sekondari ya bweni ya wasichana.
Dkt. Bessire pia
amesema kuwa yataanzishwa madarasa kwenye shule hiyo kwa ajili ya watu wazima
wasiojua kusoma na kuandika.
No comments:
Post a Comment