Mahakama moja nchini Misri,
imeamuru kufungwa kwa vituo vinne vya televisheni, ambavyo vimetuhumiwa
kupendelea chama cha Muslim Brotherhood.
Vituo hivyo ni pamoja na kituo cha chama hicho,
Ahrar 25 na tawi la kituo cha Al-Jazeera kinachopeperushia matangazo
yake nchini Misri.Wakati huohuo, jeshi la Misri, limefanya mashambulizi ya angani dhidi ya maeneo yanayoshukiwa kuwa ngome za wapiganaji wa kiisilamu katika rasi ya Sinai na kumuua mtu mmoja.
Jeshi linajaribu kuonyesha kuwa lina udhibiti wa eneo hilo linalopakana na Gaza.
Kufungwa kwa vituo hivyo, kunakuja baada ya serikali kufanya msako dhidi ya vyombo vya habari vinavyoonekana kuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi, aliyepinduliwa na jeshi tarehe 3 mwezi Julai.
Vituo kadhaa pia vililazimia kufunga kufuatia hatua za kijeshi.
Sasa mahakama mjini Cairo, imeamuru stesheni ya Al-Jazeera, Mubashir Misr kufungwa na Ahrar 25 pamoja na vituo vingine Al-Quds na Al-Yarmuk.
Siku ya Jumatatu , Misri iliwafurusha waandishi watatu wa habari wa kigeni waliokuwa wanafanya kazi na Al-Jazeera ikisema kuwa hawakuwa na stakabadhi zinazohitajika kufanya kazi nchini humo.
Bwana Morsi amezuiliwa akisubiri kufunguliwa mashtaka .
Viongozi wa mashtaka walitangaza wiki jana kuwa atashtakiwa kwa kosa la kuchochea mauaji ya waandamanaji mwaka jana.
Vuguvugu la Muslim Brotherhood limeitisha maandamano chini ya kauli mbiu 'Mapinduzi ni ugaidi'.
Shirika la habari la serikali Mena, linasema kuwa maafisa wa usalama wameziba baadhi ya barabara huku magari ya kijeshi yakisemekana kuziba sehemu za kuingilia medani ya Rabaa al-Adawiya na Tahrir.
No comments:
Post a Comment