by zittokabwe
|
Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu
muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya sheria ya
marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Mjadala na upitishaji wa sheria hii
uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu kwa vitendo vya kihuni kutokea Bungeni
ambavyo nisingependa kuvirejea kutokana na aibu kubwa ambayo Bunge liliingia.
Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya. Hii
imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili,
wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo. Masuala ya Tume
imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka
Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na
kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa na
kuzungumza. Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia
mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia
siasa. Katiba ni uhai wa Taifa.
Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo
lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi. Kuna kundi lingine ambalo lingependa
mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata
Katiba bora. Kuna kundi la Wabunge ambao kwa chinichini wanataka mchakato
uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge.
Naamini watu hawa wanaota ndoto za mchana kwani hakuna mahusiano yeyote kati ya
uchaguzi mkuu na kuandika katiba mpya. Kama Bunge hili la sasa na Serikali hii
itashindwa kukamilisha zoezi hili, Bunge linalokuja na Serikali itakayoingia
madarakani itaendelea nalo. Hivyo sio lazima kupata Katiba mpya kabla ya
uchaguzi mkuu wa 2015. CHADEMA imependekeza kuwepo na marekebisho ya mpito
kwenye Katiba ya sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea
binafsi na kadhalika. Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao
ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.
Changamoto kubwa sana ya siasa za Tanzania ni kelele. Wanasiasa
hatuzungumzi kwenye masuala yanayohusu uhai wa Taifa. Kila chama kinakuwa na
misimamo yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya
kuzungumza na kujadiliana kama Watanzania. Mwaka 2011 hali ilikuwa hivi hivi
mpaka kundi la Wazee viongozi wastaafu walipoingilia kati na kupelekea
wanasiasa kukaa na kuzungumza. Bahati mbaya sana viongozi wale ndio sasa
wamepewa usukani wa kuandika Katiba kwa kuwa kwenye Tume. Hawawezi tena kufanya
kazi ile ya kutafuta suluhu iliyopelekea Rais kuzungumza na viongozi wa vyama
vyote vya siasa ikulu jijini Dar es Salaam.
Vyama vya Upinzani nchini sasa vimeungana kupinga muswada wa
marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria
na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na Uratibu, viongozi
waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo. Badala
ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno ya kejeli na kadhalika.
Taifa halijengwi namna hii. Taifa linajengwa kwa mwafaka na Katiba ni moja ya
nyenzo wa Mwafaka wa Taifa. Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Katiba haiandikwi
barabarani bali huandikwa mezani kwa watu kukaa na kukubaliana masuala ya Taifa
dhidi ya maslahi ya kivyama ya wanasiasa.
Hakuna kilichoharibika. Bado tunayo nafasi kama Taifa kukaa na
kukubaliana. Kwa hali ya sasa nafasi hii ipo mikononi mwa Mkuu wa Nchi, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha
umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba ya nchi yetu. Hata
hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa wanasiasa wa pande zote
kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama kutoridhia sheria hiyo. Si sawa kisiasa
kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti
wa chama chenye wabunge wengi bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati
huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani
Rais wake kuridhia sheria hiyo kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi na pia
kinatafsirika kama kumshurutisha (blackmail) Rais wake.
Kutosaini muswada huu kunaweza kuleta mgongano kati ya Wabunge
wa CCM na Rais. Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama chake kwamba
umoja wa kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya chama chao. Pia
kikatiba Rais anasaini miswada kuwa sheria akiwa Mkuu wa Nchi na sio Mkuu wa
Serikali ya Jamhuri. Akiwa Mkuu wa Nchi maslahi mapana ni kuweka mwafaka wa
pamoja miongoni mwa wananchi. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutumia mamlaka yake
kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni ili uweze
kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge. Ibara ya 97 ya
Katiba ya sasa imeweka masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais
ataurudisha muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji
wake utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote. Hii itakuwa hatua muhimu sana
katika historia ya demokrasia yetu. Rais afuate ushauri huu kwani una manufaa
makubwa.
Hata hivyo, ni lazima
pawepo na mazungumzo miongoni mwa wanasiasa na makundi ya kijamii kuhusu
Katiba. Katiba nzuri itapatikana pale tu ambapo mazingira ya kisiasa
yanaonyesha nia njema kwa pande zote kisiasa. Kukwepa kuangaliana machoni na
kuzungumza tofauti zetu za kimitazamo ni hatari zaidi. Juzi ngumi zimerushwa
Bungeni. Kesho zitakua mitaani na vijijini kwetu. Tunataka kujenga Taifa la
namna hiyo?
No comments:
Post a Comment