by zittokabwe
|
Zitto Kabwe, Mb
Kwa mshtuko na masikitiko makubwa kuanzia jana jioni tumepokea
taarifa za kufungiwa kwa magazeti mawili ya kila siku hapa nchini ya Mwananchi
na Mtanzania. Serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia sheria ya kidikteta ya
magazeti ya mwaka 1976 ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali iliiorodhesha kama
sheria kandamizi. Sababu zilizotolewa kuhalalisha uamuzi huu ni sababu zisizo
na maana na ambazo Serikali ingeweza kufungua mashtaka ya kawaida kabisa
mahakamani kushtaki magazeti hayo iwapo haikupendezwa na habari walizochapisha.
Moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi ni
kuchapisha taarifa kuhusu mishahara ya Serikali. Serikali inasema habari hii ni
siri. Serikali hii hii ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali kwa
uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack Obama wa
Marekani inalifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara ya watumishi wa
Serikali. Mishahara kuanzia mshahara wa Rais mpaka wa mtendaji wa Kijiji
haipaswi kuwa jambo la siri. Kuonyesha kuwa jambo hili linapaswa kuwa wazi
mkutano ujao wa Bunge tutatafuta kila namna kutaja mshahara wa Rais, Makamu wa
Rais, Waziri Mkuu na baadhi ya Watendaji wa Mashirika makubwa ya Umma kama njia
ya kuwaunga mkono gazeti la Mwananchi kwa habari yao hiyo. Mapato ya Mbunge yanajulikana
sasa kuwa ni shilingi milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya kuongeza posho za vikao
za shilingi laki 200,000 kwa siku na posho ya kujikimu ya shilingi 130,000 kwa
siku. Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao.
Tutaanza na mshahara wa Rais!
Gazeti la Mtanzania limefungiwa pamoja na mambo mengine kwa
kuandika 'mapinduzi ni lazima'. Inashangaza Serikali ya Chama cha Mapinduzi
inaogopa neno mapinduzi. Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde, aliyekuwa mbunge
wa Jimbo la Tandahimba alipata kusema bungeni kuwa 'lazima nchi ipinduliwe'. Ni
matumizi ya lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa analalamikia maendeleo duni ya
mikoa ya kusini na kutaka Kaskazini iwe Kusini na Kusini iwe Kaskazini.
Serikali inafungia gazeti kwa sababu ya kuandika Mapinduzi ni lazima ilhali
kila siku Zanzibar wanasema Mapinduzi daima!
Gazeti la Mtanzania linahaririwa na Absalom Kibanda, mwandishi
wa habari ambaye bado anaponya majeraha ya mwili na kisaikolojia ya kuteswa na
watu ambao mpaka leo hawajakamatwa. Badala ya Serikali kuwakamata watesaji wa
Kibanda, inamnyima kazi Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa kukaa miezi mitatu
bila kazi. Pia wanatutesa Watanzania kwa njaa ya kupata habari ambayo ni haki
ya msingi ya kikatiba. Hii ndio zawadi Serikali inampa Kibanda baada ya
kung'olewa kucha, kunyofolewa jicho, kukatwa vidole na kuteswa kwa namna
isiyoelezeka.
Matukio ya hivi karibuni na namna Serikali inavyoyachukulia
yanaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete kazidiwa nguvu na kundi la wahafidhina
ndani ya chama na Serikali yake. Rais ambaye alianza kwa kuhubiri uvumilivu wa
hali ya juu na hata yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu huu wengine wanauona
kama udhaifu lakini ameamua kujenga Taifa la kuvumiliana. Rais alipata
kulalamika hadharani kwamba kuna wenzake wanataka aongeze ukali. Ni dhahiri
kundi hili la wahafidhina sasa ndio linalomwongoza Rais Jakaya Kikwete. Kitu
kimoja tu Rais azingatie, kundi hili linaongozwa na maslahi binafsi ya kubakia
kwenye utawala wakati yeye anapaswa kuacha 'legacy'. Rais Kikwete asipokuwa
makini atakuwa Rais karatasi (lame duck) tu tunapoelekea mwisho wa utawala
wake. Maamuzi ya hovyo na ya kidikteta ya kufungia magazeti yanamchora vibaya
mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa. Wahafidhina kuwa nguvu zaidi ya
kiutawala ni makosa ambayo watanzania hawapaswi kuyakubali kamwe.
Wananchi sasa
waifanye Serikali kujutia uamuzi wake wa kufungia magazeti. Nimeamua mimi
binafsi kama mbunge kesho Jumatatu tarehe 30 Septemba, 2013 kupeleka taarifa
rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka muswada Bungeni wa kuifuta kabisa Sheria
kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976. Sasa tupambane na kundi dogo la
wahafidhina ndani ya Serikali na CCM wasiopenda mabadiliko na iwe fundisho kwa
wahafidhina wengine wowote waliopo ndani ya Serikali au nje ya Serikali kwamba
Uhuru wa habari sio jambo la kuchezea kama golori.
No comments:
Post a Comment