Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa siyo kazi ya Serikali kuviokoa vyama vya ushirika kutoka kwenye
madeni kwa sababu shughuli za ushirika ni za sekta binafsi na mali ya wanachama wenyewe.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni
jambo la kusikitisha kuwa makosa ya ushirika na wezi wa baadhi ya viongozi wa
vyama vya ushirika hatimaye yanabebeshwa vyama vya siasa.
Kama namna ya kuwasaidia wananchi,
Rais Kikwete amewataka viongozi mbali mbali wa mikoa kuwasaidia wananchi ili
kupata viongozi waadilifu na waaminifu na wala siyo wezi kama
ilivyo sasa kwa vyama vingi vya ushirika.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku
wa kuamkia leo, Jumamosi, Septemba 7, 2013, wakati alipopokea Ripoti ya
Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanza kwenye siku ya
kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Rais Kikwete aliwaambia viongozi
hao wa Mkoa wa Mwanza: “Tumewahi huko nyuma kulipa madeni yote ya vyama vya
ushirika. Nia ilikuwa kuvisaidia vyama hivyo na wanachama wake kujipanga upya
na kupata uhalali wa kuweza kukopa fedha za kjuendesha shughuli zao. Lakini
sasa, vyama hivyo, vimerudi kule kule kwenye madeni.”
Alitoa mfano wa Chama cha Ushirika
cha Mkoa wa Pwani kama moja ya vyama vya
ushirika ambavyo madeni yake yalilipwa na Serikali lakini sasa kina deni kubwa
zaidi kuliko hata lile lililolipwa na Serikali.
“Wale watu wa Pwani walikwenda
kukopa na benki moja ikakubali kuwapa fedha. Wameshindwa kulipa na ule ushirika
nadhani utakufa. Njia bora kwa vyama vya namna hiyo ni kuviachia vife tu kwa
sababu havina faida yoyote kwa mkulima.”
Aliongeza: “Vyama vya ushirika siyo
mali
ya Serikali. Ni mali
ya wanaushirika na hivyo ushirika ni sekta binafsi. Lakini hakuna shaka kuwa
baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanatesa wananchi. Wanakopa fedha
kwenye mabenki lakini wanashindwa kuzirudisha fedha hizo na hilo linapotokea Serikali inalaumiwa kwa hali
hiyo.”
Rais alikuwa anatoa maelekezo yake
baada ya kuambiwa kuwa Chama cha Ushirika cha Nyanza cha Mkoa wa Mwanza kilikuwa
kinakamilisha mpango wa kukopa kiasi cha sh bilioni saba kutoka Benki ya
Raslimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kununulia pamba.
Lakini aliwaambia viongozi hao:
“Uamuzi wa kukopa ama kutokukopa ni wa kwenu. Nyanza ni mali yenu, wezi
waliopata kukibebesha madeni chama hicho mliwachagua nyie wenyewe. Fedha ni
zenu lakini hatimaye athari za makosa yenu yanaiathiri Serikali na hata vyama
vya siasa.”
“Kuna wakati viongozi wa Chama cha
Nyanza walipata kuuza godown ya thamani y ash milioni 600 kwa sh milioni 50 tu.
Hawa ni wezi wa mchana wanaoiba kweupe. Wanaiba lakini wanataka Serikali
iwasaidie. Kwa nini? Nadhani kazi yetu kama
viongozi ni kuwasaidia wananchi kupata viongozi adilifu na aminifu siyo wezi,”
alisema Mheshimiwa Rais Kikwete na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba hata sisi
viongozi tunakataa kuwashughulikia wezi kwa sababu hawa ni watu maarufu na
wakati mwingine baadhi ya viongozi wanakula nao na jambo hilo
limekuwa tatizo kubwa sana.
Tunavifikisha vyama vya ushirika mahali ambako sina uhakika kama bado ni mali ya
wakulima. Wakulima wanakutana na ushirika wakati wa kuchagua viongozi tu na
baada ya hapo wakulima hawaonekani tena.”
No comments:
Post a Comment