Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kazi kuu na
kipimo halisi cha kiongozi bora na hodari ni jinsi kiongozi anavyohangaikia
maendeleo ya wananchi, ubunifu wake wa kuwaongezea wananchi mapato na kujali kumaliza
kero zao.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa kazi ya madiwani nchini haiwezi kuwa ni kupokea posho za vikao ama
kupima na kujigawia viwanja bali iwe ni kupambana na umasikini wa wananchi
ambayo ndiyo kazi waliyoomba wakati wanatafuta kura za kuwa madiwani.
Vile vile, Rais
amewataka madiwani wote nchini kutumia haraka na ipasavyo fedha zinazotolewa
kwa ajili ya ujenzi wa barabara ndani ya halmashauri zao na siyo kuziweka hadi
mwisho wa mwaka wa fedha na kulazimika kuzirudisha kwenye Mfuko wa Barabara.
Rais Kikwete
ameyasema hayo leo, Ijumaa, Septemba 6, 2013, wakati alipopokea Taarifa ya
Maendeleo ya Wilaya ya Misungwi wakati alipoanza ziara ya siku tano katika Mkoa
wa Mwanza kukagua na kufungua shughuli na miradi ya maendeleo.
Akiuliza
maswali na kutoa maelekezo wakati Ripoti hiyo inawakilishwa na Mkuu wa Wilaya
ya Misungwi, Bibi Mariam Lugaija kwenye Shule ya Sekondari ya Misungwi, Rais
Kikwete amewaambia viongozi wa Wilaya hiyo na wa Mkoa wa Mwanza:
“Kazi muhimu na
uhodari wa kiongozi unathibitishwa na jinsi kiongozi huyo anavyopambana
kupunguza umasikini wa wananchi na anavyobuni mbinu za kuongeza mapato ya wale
anaowaongoza.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Kila kiongozi lazima awe na uchungu wa maendeleo na tamaa ya kuleta
mabadiliko kwa wananchi wao. Kazi ya kiongozi ni kuhangaika na maendeleo ya
wananchi.”
Akionyeshwa
kutoridhishwa na kiwango cha uongozi cha baadhi ya madiwani mkoani humo, Rais
Kikwete amewaambia viongozi hao: “Kazi ya madiwani haiwezi kuwa kupima na
kugawa viwanja. Mliomba kazi ya udiwani ili kuwatumia wananchi na kuwaletea
maendeleo. Nyie madiwani hamuwezi kuendelea kuwasibiri TASAF kuwaletea wananchi
wenu maendeleo. Hii ni kazi yenu.”
Ameongeza kuelekeza
Rais Kikwete: “Kazi yenu haiwezi kuwa ni kusubiri posho ya vikao na kupokea mishahara
bure. Lazima muwe na tamaa ya maendeleo ya wananchi wenu.”
Aidha, aliwakumbusha
kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa
barabara kwenye halmashauri hizo, lakini madiwani wanashindwa ama kuchelewa
kuzitumia fedha hizo kujenga barabara hadi mwaka wa fedha unamalizika.
“Hili nalo
halikubaliki. Kwa sababu Serikali inawapa fedha nyingi, lakini nyie hamzitumii
kwa wakati na fedha hizo zinarudishwa kwenye Mfuko wa Barabara.”
No comments:
Post a Comment