Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , amezindua mtambo wa kufua umeme kiasi cha megawati 60 katika eneo la
Nyakato mjini Mwanza, umeme ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza shida
ya umeme katika Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Aidha, Rais Kikwete
ameiangiza Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
kuanza mara moja maandalizi ya kupeleka umeme kwenye machimbo ya madini ya
nikeli yaliyoko Kabanga, Ngara, Mkoa wa Kagera.
Vile vile, Rais
Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaharakisha mipango ya kujenga reli hadi
kwenye eneo hilo kama maandalizi ya kuanza kuchimbwa kwa madini hayo ambayo ni
mazito na kuyasafirisha kwa barabara kwenda bandarini Dar Es Salaam kutaharibu
kwa haraka barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa nchini.
Akizungumza kabla ya
kuzindua mtambo huo, Rais Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini
kuharakisha mipango ya kuunganisha eneo la Kabanga, Ngara, Mkoani Kagera kwenye
Gridi ya Taifa ili uzalishaji wa madini ya nikeli usije kukwamishwa na ukosefu
wa umeme. Amesema kuwa mgodi huo utahitaji umeme mwingi kiasi cha megawati 40.
Rais amesema kuwa
Serikali yake itahakikisha inafikisha reli kwenye eneo la Kabanga mapema ili
kuhakikisha kuwa nikeli inayozalishwa inasafirishwa kwa reli badala ya
barabara. Amesema kuwa madini hayo ni mazito mno na kuyasafirishwa kwa barabara
kutaharibu kabisa na katika muda mfupi barabara ambazo zinajengwa nchini kwa
gharama kubwa.
Mtambo wa Umeme wa
Nyakato wenye uwezo wa kuzalisha megawati 60 ulianza kujengwa mwaka jana, 2012,
baada ya Serikali ya Tanzania kutiliana mkataba wa ujenzi na Kampuni ya Semco
and Rolls Royce ya Norway mwaka 2011 wakati maandalizi ya ujenzi huo
yalipoanza.
Gharama za ujenzi wa
mtambo huo ambazo ni sh bilioni 130 (Euro milioni 48.7 na dola za Marekani
15.9) zimelipwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na
wananchi kwenye sherehe ya uzinduzi huo, Rais Kikwete amesema kuwa umeme siyo
anasa bali ni moja ya vigezo vya msingi na muhimu kabisa vya maendeleo.
“Vipo vigezo vingi
vya maendeleo ya nchi na binadamu, lakini moja ya vigezo hiyo ni umeme. Na
ukiangalia matumizi ya umeme kwa kila nchi yanaonyesha kiwango cha maendeleo
cha nchi hiyo. Katika Marekani, kwa mfano, kila mwananchi anatumia kiasi cha
kilowati 12,000 kwa wastani. Sisi katika Tanzania ni kilowati 89 tu na wastani
wa Bara la Afrika ni kilowati 150,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nc hi yetu ya
Tanzania ina umeme kiasi cha megwati 1,450 tu wakati katika Afrika Kusini ni
megawati 45,000 na unaweza kuona tofauti ya maendeleo. Hivyo, ni muhimu sana
kwetu kuongeza kiwango cha kuzalisha umeme katika nchi yetu.”
Katika siku ya tatu
ya ziara yake kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza, Rais Kiwete
pia amefungua Kituo cha Polisi cha Nyakato ambacho kimegharimu sh milioni 450,
Serikali ikiwa imechangia kiasi cha asilimia 20 cha gharama hizo.
Kituo hicho cha
kisasa kilianza kujengwa mwaka 2003 lakini ujenzi wake ukawa unakwamakwama
kutokana na ukosefu wa bajeti hadi uongozi wa polisi wa Mkoa wa Mwanza
ulipoamua kukijenga kituo hicho kwa njia
ya kuishirikisha jamii na ikaundwa Kamati ya Ujenzi chini ya uenyekiti wa Bwana
Alfred Wambiura.
Akizungumza kwenye
sherehe ya ufunguzi wa kituo hicho, Rais Kikwete ameahidi kuwa atajenga nyuma
moja kwa ajili ya mkazi ya polisi. Kituo hicho kina jumla ya askari polisi 65.
No comments:
Post a Comment