Friday, March 01, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA


MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MACHI HADI MEI 2013
Taarifa hii inatoa tathmini ya msimu wa mvua za Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2012,
mvua zinazoendelea katika maeneo ya kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini magharibi
na mikoa ya kusini pamoja na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua za Masika katika
kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei (MAM) 2013.
A. UTANGULIZI
Tathmini ya mvua za Vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2012 inaonyesha
kuwa maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani isipokuwa baadhi ya maeneo ya Dar es
Salaam, Tanga kisiwa cha Unguja ambayo yalipata mvua za chini ya wastani. Hata hivyo,
mtawanyiko wa mvua hizo haukuwa mzuri na uliambatana na matukio ya hali mbaya ya hewa
kama vile, upepo mkali na mvua kubwa ambayo yalisababisha maafa yaliyopelekea vifo,
uharibifu wa mali na miundombinu katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei, 2013 unaonyesha maeneo mengi yanayopata
misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu Kaskazini
Mashariki na Pwani ya Kaskazini) yanatarajiwa kupata mvua za wastani. Mvua zinazoendelea
kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (magharibi, nyanda
za juu kusini magharibi na kusini) zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani katika maeneo mengi
isipokuwa katika maeneo ya mikoa ya Njombe, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa
mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani.
Viashiria vikuu vilivyopo na vinavyotarajiwa kusababisha mvua hizi ni kuwepo kwa joto la juu
ya wastani katika maeneo ya mashariki mwa baharí ya Atlantiki (Pwani ya Angola), joto la
wastani katika eneo la magharibi mwa bahari ya Hindi, upepo wenye unyevunyevu hafifu kutoka
misitu ya Congo kuvuma kuelekea nchini na kuwepo kwa upepo hafifu wa mashariki kutoka
bahari ya Hindi.
B: TATHMINI YA MVUA ZA VULI OKTOBA HADI DISEMBA, 2012
Mvua katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2012, zilikuwa za wastani katika
2
maeneo mengi ya nchi isipokuwa baadhi ya maeneo machache yalipata mvua za juu ya wastani.
Aidha, maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam,Tanga na kisiwa cha Unguja yalipata mvua za chini
ya wastani. Kwa ujumla mtawanyiko wa mvua za msimu wa Vuli haukuwa wa kuridhisha na
uliambatana na matukio ya hali mbaya ya hewa yaliyosababisha vifo, uharibifu wa mali na
miundombinu katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, Mbeya,
Tabora, Kagera na Mwanza. Mvua zinazoendelea katika maeneo yanayopata mvua mara moja
kwa mwaka hususan maeneo ya kati ya nchi ni za wastani hadi juu ya wastani. Vifuatavyo ni
viwango vya mvua pamoja na wastani wa muda mrefu katika baadhi ya vituo hivyo:
Maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka:
Pwani ya Kaskazini: Matangatuani mm 623.6 (130.3%), Pemba mm 259.8 (94.3%), Amani
mm 415.7 (80.3%), JNIA mm 191.1 (61.1%) Zanzibar mm 422.9 (66.4%) na Morogoro mm
152.5 (77.6%).
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: Moshi mm 155.4 (111.6%), Arusha mm 377.7 (174.8%),
Lyamungo mm 200.9 (94.1%), Same mm 208.1 (125.8%) na KIA mm 158.9 (145.4%).
Kanda ya Ziwa Viktoria: Mwanza mm 605.9 (158.8%), Bukoba mm 492.5 (88.8%), Musoma
mm 226.7 (93.1%) na Shinyanga mm 264.5 (90.4%).
Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Magharibi: Tabora mm 265.2 (77.5%), Kibondo mm 320.3 (80.2%), Tumbi mm 246.9 (73.3%)
na Kigoma mm 376.9 (66.3%).
Kanda ya Kati: Dodoma mm146.7 (96.8%), Hombolo mm 92.6 (55.3%) na Singida mm 228.9
(108.1%)
Nyanda za Juu Kusini Magharibi: Iringa mm 211.8 (144.1%), Mbeya mm 193.7 (74.3%),
Tukuyu mm 437.2 (121.0%), Sumbawanga mm 324.3 (108.1%), Mahenge mm 239.1 (44.6%) na
Igeri mm 198.5 (60.3%).
Maeneo ya Kusini: Mtwara mm 59.7 (25.1%), Naliendele mm 52.5 (19.4%) Kilwa mm 259.9
(109.2%) na Songea mm 247.8 (103.6).
Angalizo: Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa
kama chini ya wastani, wakati viwango vya kati ya asilimia 75 hadi 125 hutafsiriwa kama
mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.
C: MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mwelekeo huu umezingatia hali ya mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa na athari
zake kwa msimu ujao wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2013 hapa nchini.
Uchambuzi wa hali ya joto la bahari unaonyesha kuwa kuna joto la juu ya wastani katika maeneo
ya magharibi mwa bahari ya Hindi (pwani ya Afrika mashariki) ambalo linatarajiwa kuendelea
kuwepo mpaka mwezi Machi, 2013 na kuwa hafifu kwa miezi ya Aprili na Mei, 2013. Joto hili
la bahari lililopo na linalotarajiwa kuwepo, linategemewa kusababisha ongezeko la mvua katika
maeneo ya mashariki mwa nchi hususan kwa mwezi Machi, 2013. Aidha, kuwepo kwa joto la
3
wastani kwa miezi ya Aprili na Mei, 2013 likiambatana na upepo hafifu kutoka bahari ya Hindi
kuelekea katika ukanda wa mashariki mwa nchi, hali ambayo inatarajiwa kupunguza kuwepo
kwa unyevunyevu wa kutosha kutoka bahari ya Hindi.
Joto la juu ya wastani mashariki mwa bahari ya Atlantiki (pwani ya Angola), linatarajiwa
kuendelea kuwepo katika msimu wote na upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo,
hivyo kusababisha upungufu wa mvua hususan katika maeneo ya magharibi mwa nchi. Aidha,
hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la Pwani ya Somalia linatarajiwa kudhoofisha ukanda
wa Mvua (ITCZ) katika maeneo ya nchi yetu, hivyo kupelekea kuwepo kwa upungufu wa mvua
katika msimu wa masika hususan katika miezi ya Aprili na Mei, 2013.
D: MWELEKEO WA MVUA: MACHI HADI MEI (MAM), 2013
(i) Mvua za Masika
Maeneo ya kaskazini mwa nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua
zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2013. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa kama
ifuatavyo:
Kanda ya Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera,Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi katika mikoa ya Kagera na Geita na
kusambaa katika maeneo mengine ya mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu wiki ya
pili ya mwezi Machi. Maeneo ya mikoa ya Kagera na Mara yanatarajiwa kupata mvua za
wastani, isipokuwa mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita na Simiyu ambayo inatarajiwa kupata
mvua za chini ya wastani.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Maeneo ya
kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi na zinatarajiwa kuwa za wastani
kwa maeneo ya ukanda wa pwani na chini ya wastani katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa
Morogoro na kusini mwa mkoa wa Pwani.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za
wastani.
(ii) Mvua za Msimu
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi):
Mvua zinazoendelea katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani na zitaisha wiki
ya nne ya mwezi Aprili, 2013.
Kanda ya Kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani.
Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2013.
Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi):
Mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani katika maeneo mengi.
Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2013.
4
Maeneo ya kusini (mkoa wa Ruvuma):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani na zitaisha mwishoni
mwa wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2013.
Nyanda za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, na maeneo ya kusini
mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani, isipokuwa maeneo ya
mkoa wa Iringa na kusini mwa mkoa wa Mbeya ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za chini ya
wastani. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2013.
Angalizo: Vipindi vifupi vya mvua kubwa ni matukio ya kawaida hata katika maeneo
yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya
hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo
wa mvua nchini. Pamoja na kutoa tahadhari, mrejeo utaendelea kutolewa kila inapobidi.
5
Kielelezo: Matarajio na mwelekeo wa mvua za Machi hadi Mei 2013
Rangi katika ramani inaonyesha matarajio ya mvua kuwa katika madaraja matatu:juu ya Wastani, Wastani
na chini ya Wastani. Namba ya juu inaonyesha uwezakano wa mvua kuwa juu ya Wastani, ya kati
inaonyesha mvua kuwa za Wastani na ya chini inaonyesha uwezekano wa mvua kuwa za chini ya wastani.
Mfano: rangi ya kijani katika maeneo ya Ruvuma,Tanga na Arusha inaonyesha uwezekano wa kupata mvua
juu ya wastani ni asilimia 20, Wastani ni asilimia 45 na chini ya Wastani ni asilimia 35.
E: ATHARI NA USHAURI
Kilimo na Usalama wa Chakula
Maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,
nyanda za juu kaskazini mashariki, kanda ya Ziwa Victoria, nyanda za juu kusini magharibi, na
maeneo ya kusini mwa nchi yanatarajiwa kuwa na unyevunyevu wa kutosha wa udongo.
Maeneo mengine ya nchi yaliyosalia yanatarajiwa kuwa na upungufu wa unyevunyevu wa
6
udongo katika miezi ya Aprili na Mei. Katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani, na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), nyanda za juu kaskazini
mashariki (mikoa ya Manyara, Arusha, na Kilimanjaro), ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya
Mara na Kagera), wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za kilimo cha
masika. Hata hivyo, wakulima katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita na Simiyu pamoja na
maeneo ya Morogoro kaskazini wanashauriwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na
kukomaa mapema.
Maeneo ya magharibi (mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, na Katavi), maeneo ya kati (mikoa ya
Dodoma na Singida), na pwani ya kusini (mikoa ya Lindi na Mtwara), wakulima wanashauriwa
kuendelea kutafuta na kufuata ushauri wa Maafisa Ugani katika maeneo yao utakaosaidia
kutumia kwa manufaa kipindi cha mvua kilichobaki. Maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi
(Mikoa ya Mbeya, Njombe na maeneo ya Iringa kusini), kanda ya kusini (mkoa wa Ruvuma)
pamoja na maeneo ya Morogoro kusini, wakulima wanashauriwa kuendelea na shughuli za
kawaida za kilimo wakati huu mazao yanapoelekea kukomaa.
Nishati na Maji
Vina vya maji katika maziwa, mabwawa na mito havitarajiwi kuongezeka kwa kiwango
kikubwa kutokana na mvua chache zinazotarajiwa katika kipindi cha msimu wa Machi hadi Mei.
Hivyo, inashauriwa maji yatumike kwa uangalifu na kuwepo mipango mbadala ya uzalishaji wa
nishati.
Malisho na Maji kwa ajili ya Mifugo na Wanyamapori
Hali ya malisho na maji inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili
ya mvua, isipokuwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua ambapo hakuna mabadiliko
makubwa yanayotarajiwa. Hata hivyo, wafugaji wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa
matumizi wakati wa kiangazi na kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa mifugo katika maeneo
yao. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani uoto pamoja na maua vinatarajiwa
kuimarika , hali hiyo itaimarisha bioanuai na uzalishaji mwingi wa asali na nta. Aidha, mvua
hizo zitasaidia kupunguza kuhama kwa wanyamapori na migogoro baina ya wanayamapori na
wananchi. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chini ya wastani maafisa wanyamapori na
misitu wanashauriwa kuchukua hatua stahiki.
Mamlaka za Miji
Pamoja na matarajio ya mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi,
uwezekano wa kutokea vipindi vya mvua kubwa hauwezi kuepukika. Hivyo, Mamlaka za miji
zinashauriwa kusafisha mifumo ya maji taka ili kuepusha maji kutuama na kupunguza madhara
yatokanayo na mafuriko.
Sekta ya Afya
Pamoja na matarajio ya mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi,
bado kuna uwezekano wa kutokea milipuko ya magonjwa kama vile malaria, magonjwa ya
macho, na kipindupindu. Hivyo, Mamlaka husika zinashauriwa kuchukua tahadhari na
maandalizi stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
7
Menejimenti za Maafa
Taasisi za maafa na wadau husika, wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya
kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kutokea.
Mamlaka inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,
wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata
na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
IMETOLEWA NA MAMLAKA YA HALI YA HEWA

No comments:

Post a Comment