Friday, March 01, 2013

Rais Barack Obama kualikwa Kenya

 
Rais Barack Obama
Rais wa Marekani Barack Obama, ni miongoni mwa viongozi wa dunia walioalikwa kwa sherehe za kumuapisha rais wa nne wa Kenya.
Mkuu wa utumishi wa umma, Francis Kimemia amesema kuwa serikali imewaalika Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na marais wa nchi za Muungano wa Ulaya.
Pamoja na walioalikwa , ni marais wa kanda ya Afrika Mashariki.Rais wa Uganda Yoweri Museveni,Jakaya Kikwete wa Tanzania , Paul Kagame wa Rwanda na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
"Mnaweza kuwa na uhakika kuwa tutamwalika rais wa Marekani, kushuhudia sherehe za kuapishwa kwa rais mpya,'' alisema Kimemia kwenye mkutano wa waandishi wa habari.
Bwana Kimemia aliwataka wakenya kupiga kura kwa amani wakati wa uchaguzi huo.
"tunawataka wakenya kuweka amani. Sisi tumefanya mikakati ya kuhakikisha kutakuwa na usalama wa kutosha na kuhakikisha kuwa tutafaulu,'' aliongeza Kimemia.
Rais mpya anatarajiwa kuapishwa tarehe 26, mwezi Machi, wiki tatu baada ya wakenya kumchagua.

No comments:

Post a Comment