Mzee Kitwana Suleiman Kondo, Mwenyekiti wa Taasisi
ya Maendeleo ya Waislamu (MDF);
Mheshimiwa Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Waislamu cha Morogoro;
Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;
Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na
Jumuiya mliohudhuria;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Niruhusuni
niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma,
kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa. Nakushukuru sana Mama Mwantumu Malale, Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro na viongozi wenzako kwa kunialika kuja
kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya ufunguzi wa jengo la Kitivo cha
Sayansi katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro. Mmenipa heshima kubwa ya
kuwa sehemu ya historia ya Chuo hiki. Kwa
kweli, nimefarijika sana kuona Chuo chetu kinazidi kupata mafanikio ya kutia
moyo hasa ukizingatia ukweli kwamba kina muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Natoa
pongezi nyingi kwako, Makamu Mkuu wa Chuo na wale wote walioshiriki kubuni wazo
la kuwa na jengo la Kitivo cha Sayansi na kufanikisha ujenzi wake. Juhudi zao na moyo wao wa kupenda maendeleo
ndio umetufanya sisi kujumuika hapa leo kushuhudia mafanikio haya. Hakika ni
jambo la kujivunia. Pia, nawapongeza sana Wajenzi na Mhandisi Mshauri kwa kazi
nzuri waliyofanya ya ujenzi wa jengo hili.
Sote tunaliona jengo lilivyojengwa vizuri na kwa namna yake
linapendezesha mandhari ya Chuo.
Kwa
namna ya pekee napenda kwa niaba yenu nitoe shukrani zangu za moyoni kwa taasisi
ya Al-Barakah kwa kufadhili ujenzi wa jengo hili. Asanteni sana kwa ukarimu wenu na upendo
mkubwa mliouonesha kwa nchi yetu na watu wake. Naomba taasisi nyingine na watu
binafsi waige mfano huu mzuri wa kusaidia miradi mbalimbali inayonufaisha jamii. Tukumbuke ule msemo wa wahenga kuwa “kutoa ni moyo, usambe si utajiri”.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Kwa
miaka mingi madhehebu ya dini na mashirika
ya dini yamekuwa washirika muhimu sana wa Serikali katika kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Yamekuwa
yanajihusisha na kutoa huduma kwa jamii kama vile afya, elimu na nyinginezo.
Kwa ajili hiyo watu wengi sana nchini wamenufaika na wanaendelea kunufaika na
huduma zinazotolewa na mashirika ya dini.
Kwa
miaka mingi mashirika na taasisi za madhehebu ya dini ya Kikristo
ndiyo yaliyokuwa yakionekana kutoa huduma hizo. Kwa upande wa Waislamu, ukiacha
Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, mchango umekuwa mdogo sana. Ni jambo la
faraja kubwa kuona Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF) ikionyesha njia. Kwa kumiliki na kuendesha Chuo Kikuu cha
Waislamu cha Morogoro kwa ufanisi, MDF inatoa mchango muhimu katika kuendeleza elimu
ya juu na maendeleo nchini. Idadi kubwa
ya wanafunzi waliofuzu masomo yao na waliopo katika Chuo hiki tangu kilipoanzishwa mwaka 2005 ni ushahidi tosha wa kazi nzuri inayofanywa
na MDF. Hongereni sana. Tunawaombea kwa Mola mpate mafanikio makubwa
zaidi miaka ya usoni kwa upande wa elimu na huduma nyingine muhimu.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Katika
kipindi cha miaka saba sasa, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika
upanuzi wa elimu tangu ya awali hadi
elimu ya juu. Tumeamua kufanya hivyo kwa
sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi,
sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawapati.
Tanzania ni kubwa kuliko Kenya na Uganda kwa eneo na idadi ya watu lakini ndiyo
tuliokuwa na idadi ndogo ya wanafunzi kwa ngazi zote hizo. Kwa mfano, mwaka 2005 idadi ya wanafunzi waliokuwa
Chuo Kikuu nchini Kenya ilikuwa 108,407,
Uganda 88,360 na kwa baadhi ya nchi
za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717,973. Wakati wenzetu wakiwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na
wanafunzi 40,719 tu katika vyuo
vikuu nchini. Hali ilikuwa hivyo pia kwa
elimu ya sekondari. Kenya ilikuwa na wanafunzi
925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini 4,186,882
wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi 524,325
tu waliokuwa katika shule za sekondari.
Tuliona
hali hii haikubaliki hivyo tukaamua hatuwezi kuiacha iendelee. Tukaamua kudhibiti. Tukachukua hatua tulizochukua
za kupanua elimu katika ngazi zote. Matokeo
ya uamuzi huo ni kwamba vijana wanaopata fursa ya kupata elimu katika ngazi
zote wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu,
tumewafikia na kuwapita majirani zetu. Kazi kubwa tunayoendelea nayo sasa ni
kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu waipatayo vijana wetu kwa kuongeza
walimu, vifaa vya kufundishia, vitabu na huduma nyinginezo. Inshallah hata kwa
dhamira yetu, hii njema Mola atatuwezesha. Mwanzo mgumu lakini hatma itakuwa
nzuri.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kufuatia
juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu nchini imeongezeka sana,
kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005
hadi wanafunzi 166,484 mwaka 2012. Kwa
upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa Kenya walikuwa na wanafunzi milioni 1.77. Haya ni mafanikio
makubwa.
Serikali
itaendelea kuwekeza kwenye upanuzi wa
fursa za elimu na ubora wake. Hata hivyo ushiriki wa wadau wengine kuunga mkono
juhudi za serikali ni jambo muhimu sana.
Tumeweka mazingira mazuri kwa
wadau hao kufanya hivyo na mafanikio yanaonekana wazi. Kama nilivyokwishasema
awali, mashirika ya dini yamekuwa wadau wa kutumainiwa na mchango wao uko wazi.
Unajieleza wenyewe. Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini, vinavyomilikiwa na umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 na sekta binafsi.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Serikali
inatambua na kuthamini mchango mkubwa na muhimu unaotolewa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa
na mashirika ya dini na sekta binafsi. Ninyi mmekuwa washirika wazuri na wa uhakika
katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu katika nchi yetu. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali
itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana na
Watanzania wengi zaidi waweze kupata elimu. Uamuzi wa kufanya utaratibu wa mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu uhusishe wanafunzi wa vyuo visivyokuwa vya umma ni
moja ya mambo mengi muhimu yanayofanywa na Serikali kuthibitisha usemi wangu
huo.
Tulipoingia
madarakani mwaka 2005 tulifanya mambo mawili muhimu kuhusu mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu. Kwanza uamuzi kwamba,
mikopo itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma na vile visivyokuwa vya
serikali. Kabla ya hapo ilihusu vyuo vya umma pekee. Pili kwamba, kila mwaka tuongeze
fedha zinazotengwa kwa ajili ya Mfuko
huo ili idadi ya wanafunzi wanaonufaika iongezeke. Tulikuta Mfuko ukiwa na shillingi billioni
56.1 unanufaisha wanafunzi 16,345 mwaka
2005. Tukaongeza kila mwaka na katika mwaka huu wa fedha (2012/13) tumetenga
shillingi bilioni 345 zinazowanufaisha
wanafunzi 98,772.
Tutaendelea
kuongeza fedha katika Mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na hata
ifikie siku moja tuweze kuwakopesha wote bila ya kujali sifa ya uwezo wa wazazi
au walezi kulipa ada. Kwa kasi
tuliyonayo na kwa jinsi tunavyozidi kufanikiwa katika kukusanya mapato ya serikali,
naamini miaka michache ijayo tunaweza kufikia lengo hilo. Nawasihi Bodi ya
Mikopo iwekeze katika kuimarisha uwezo
wa kuwafuatilia waliokopeshwa kulipa mikopo waliyopewa. Matamanio yangu ni kuwa
fedha zilizotolewa zizunguke ili tupunguze kiasi kinachotolewa na bajeti ya
serikali kila mwaka.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Niruhusuni
nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mkuu wa Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo, Wahadhiri
na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu hiki kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo ya
kuendeleza na kuboresha Chuo. Tumeshuhudia ujenzi wa jengo nililolifungua leo. Tumeona
mafanikio kwa upande wa ongezeko la idadi ya wanafunzi, walimu, wafanyakazi na
fani zinazofundishwa katika kipindi hiki kifupi cha uhai wa Chuo hiki.
Nimefurahishwa
na
kufarijika sana kusikia kuwa ubora wa
elimu inayotolewa hapa chuoni ni jambo linalopewa kipaumbele cha
kwanza. Jambo hili ni muhimu sana kulisisitiza kwani
tunataka wahitimu wa Chuo hiki wafanane na wahitimu wa Chuo chochote
kizuri
nchini na hata duniani. Ningependa kuona
wahitimu wa Chuo hiki wanagombewa katika soko la ajira. Hili ni jambo
linalowezekana. Kinachotakiwa
ni uamuzi wa Baraza na Seneti kuwa iwe hivyo na kuchukua hatua
zipasazo. Sina shaka kuwa mnaweza kufanya hivyo. Hakika mnaweza, na
sote kwa umoja wetu
tunaweza.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Nimefurahi
sana, pia, kusikia kuwa Chuo kinatoa mafunzo ya ualimu. Bila ya shaka mnaelewa
kwa nini nafurahi. Tuna uhaba mkubwa wa walimu nchini hivyo Chuo cho chote
kinachotoa mafunzo ya ualimu hunifurahisha.
Endeleeni kuimarisha mafunzo hayo ili Chuo chenu kitambulike na kukubalika
nchini kwa sifa ya kutoa walimu wazuri. Walimu wa kutoka Chuo hiki wawe wale wanaojua
vyema masomo wanayofundisha, mahiri kufundisha na waadilifu. Naomba pia mtoe kipaumbele cha juu kwa mafunzo
ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati. Mkifanya hivyo, mtakuwa mnatoa mchango mkubwa
katika jitihada za kupunguza uhaba wa walimu wa masomo hayo nchini. Naamini kitendo cha kuzindua Jengo la Kitivo
cha Sayansi, kilichofanyika muda mfupi uliopita kinatoa matumaini ya Chuo Kikuu
cha Waislamu cha Morogoro kuchangia katika jitihada za kupunguza pengo la
walimu wa sayansi nchini.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Nimewasikia
mkieleza kwa ufasaha changamoto kubwa na ndogo ambazo Chuo inakabiliana
nazo. Nawapongeza kwa dhati, wewe na
viongozi wenzako kwa ubunifu wenu na hatua mnazochukua kuzikabili changamoto hizo. Nawaahidi msaada na ushirikiano wangu na wa
serikali kwa yale yaliyoko kwenye uwezo wangu na wa serikali katika kutafuta
ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili.
Nawapongeza
kwa uamuzi wenu wa kutafuta vyuo vikuu rafiki vilivyoko katika nchi mbalimbali
duniani mnavyoweza kushirikiana navyo. Endeleeni
kufanya hivyo kwani vyuo vikuu vingi duniani hufanya hivyo. Hamtakuwa wa kwanza na wala hamtakuwa
mnafanya jambo la kustaajabisha. Mnaweza,
mkipenda, kuwaomba Mabalozi wetu
waliopo katika nchi mbalimbali duniani wawasaidie. Ni wajibu wao kufanya hivyo
kwani kusaidia kusukuma maendeleo ya hapa nchini kutoka huko waliko ndilo
jukumu lao la msingi. Vile vile, nimefurahishwa na mipango yenu ya baadaye ya
kuwa na matawi katika mikoa mbalimbali nchini.
Hongereni kwa uamuzi wenu wa busara. Lazima Chuo kitanuke kwa maana ya
kuwa kikubwa zaidi, makao makuu na kwa kuwa na vyuo vishiriki na shule au vitivo sehemu mbalimbali nchini.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kazi
iliyo mbele yenu ni kubwa, hivyo ni vyema kuweka mikakati mizuri na mipango
thabiti ya utekelezaji na ufuatiliaji wa dhamira yenu hiyo njema. Rai yangu kwenu ni kuwaomba muwe wabunifu zaidi
hasa katika kutafuta vyanzo vingine vya mapato vitakavyosaidia Chuo kujiendesha
bila kutegemea ada peke yake. Chuo
kiangalie uwezekano wa kufanya shughuli zitakazowaingizia mapato kama vile kufanya
shughuli za kutoa ushauri. Pia muangalie uwezekano wa kuwekeza wenyewe kwenye
miradi ya kiuchumi au kwa kushirikiana na wawekezaji katika baadhi ya maeneo.
Kuhusu
nafasi mbili za ufadhili nilizopewa na Chuo kikuu cha Tun Abdul Razak cha
Malaysia, nitafuatilia kujua kilichoendelea
na kinachoendelea. Je, nafasi hizo bado zipo?
Zikiwepo, nitawasiliana na wahusika waangalie uwezekano wa kuwapeni. Kama
zimeshagawiwa basi tusubiri safari ijayo. Kwa masuala ya ardhi na maombi mengine nimeyasikia,
yaleteni tuangalie namna ya kusaidiana.
Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo, na
Wafanyakazi wote wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;
Napenda
kuwakumbusha kuwa mnayo dhamana kubwa na wajibu mkubwa na wa kihistoria. Ule
ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Waislamu wazawa kuwa na Chuo
Kikuu inawapeni wajibu maalum wa kuhakikisha Chuo kinafanikiwa. Ni mtihani na
changamoto ya aina yake kuthibitisha kuwa Waislamu nao wanaweza kuwa na Chuo
kizuri na chenye kutoa elimu ya ubora wa hali ya juu. Kwa sababu hiyo hamna budi kuhakikisha kuwa mna
mipango mizuri ya kujenga Chuo cha hadhi na ubora wa hali ya juu. Ihakikishwe kuwa mipango hiyo inatekelezwa
kwa ukamilifu.
Aidha
jumuiya yote inao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, maarifa na weledi
ili dhima hiyo ya Chuo iweze kutimizwa kwa ukamilifu. Timizeni wajibu wenu
ipasavyo ili jina la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro likue haraka. Sifa
yake isambae na kuvuma kote nchini. Chuo kifanye vizuri ili wanafunzi waone
fahari kuwa wahitimu wa Chuo hiki. Chuo ambacho, wazazi wapende kuleta vijana
wao kuja kusoma hapa. Kwa jinsi Mkuu wa Chuo alivyoeleza, mimi nina imani
mnaweza, fanyeni kweli.
Ndugu Wanafunzi wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;
Naomba
wote
muone fahari ya kuwa wanafunzi katika Chuo cha kihistoria hapa
nchini. Nawasihi mjitume kwa kadri ya
uwezo na vipaji mlivyopewa na Mwenyezi Mungu mfanikishe kile
kilichowaleta. Jifunzeni kwa bidii mfaulu vizuri ili
mkihitimu muwe kielelezo kizuri cha mafanikio na ubora wa Chuo Kikuu
Cha Waislamu cha Morogoro. Muwe Mabalozi na kioo cha ufanisi wa Chuo
hiki.
Nawasihi mjiepushe na mambo yatakayowapunguzia muda au kuwaondoa katika
shughuli
ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza mpate digrii katika fani
mliyochagua
mwenyewe kuisomea. Vishawishi ni vingi
na wapo watu wengi wanaopanga kuwashawishi mtumie muda wenu adhimu
kufanya
wanayoyataka wao ambayo mkishiriki huwatoa kwenye malengo na kutekeleza
yao. Mambo
ya dunia ya nje ya Chuo ni mengi huna budi kutambua lipi ufanye na lipi
usifanye na kwa wakati gani!
Mwanafunzi
wa Chuo Kikuu ni mtu mzima, si mtoto. Lazima ujue kuwa unawajibika kwa kila
unaloamua na kutenda. Amua kuwajibika
vizuri. Fikiri kabla ya kutenda, changanua lipi ni lipi kabla ya kufanya uamuzi
wa kile unachotaka kufanya. Wakati wote
uongozwe na busara na hekima na siyo jazba na ushabiki wa matakwa ya
kundi. Kama ni jema fanya na kama si
jema usifanye. Kwanza tambua wewe ni
nani na uko hapa kwa ajili gani. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke
yako. Utafaulu au kufeli wewe. Utapata shahada wewe na si mtu mwingine. Hakuna ubia wa kufaulu au kufeli au kiwango
cha kufaulu. It will always remain
personal. Katika masomo unanufaika wewe. Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali maslahi
yako. Maslahi ya wengi yasiyojumuisha
yako, yahoji vizuri kabla ya kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama
umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo, sijui utakuwa shujaa wa
nani.
Mabibi na Mabwana;
Kabla
ya kumaliza napenda kutambua na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa
Benjamin Mkapa na viongozi wa MDF kwa juhudi zao za pamoja zilizowezesha Chuo
hiki kuwepo. Nitakuwa mchoyo wa fadhila
nisipowashukuru wananchi wanaokizunguka Chuo kwa ujirani mwema na wakazi wa
Morogoro kwa ujumla kwa kukipokea vizuri na kuishi na wanajumuiya wa Chuo hiki
kwa upendo mkubwa. Naomba muendelee na moyo na ushirikiano huo.
Baada
ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na
mafanikio tele.
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment