SERIKALI imeombwa kufanya utaratibu wa kuwalipa fidia baadhi
ya wananchi wa manispaa ya Bukoba iliyoko mkoani Kagera walioondolewa kwenye makazi yao ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege uliko mjini Bukoba.
Ombi hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali
mstaafu Fabian Massawe kwenye taarifa yake aliyoitoa kwa waziri wa uchukuzi Dr.Harrison
Mwakyembe aliyekuwa mjini Bukoba kukagua maendeleo ya shughuli za upanuzi wa
uwanja huo wa ndege.
Massawe amesema hadi sasa
ni wananchi 12 tu ambao wamelipwa fidia kwa ajili ya kupisha upanuzi wa uwanja kati ya 41 waliofanyiwa tathimini, amesema wananchi
hao mara kwa mara wamekuwa wakiandamana kudai haki yao kwenye ofisi yake.
Naye, mhandisi mshauri wa kampuni ya SSI inayosimamia ujenzi
wa uwanja huo, Patrick Kain amemweleza waziri Mwakyembe sababu zinazochangia kuchelewesha upanuzi wa uwanja
huo wa ndege, ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na mvua zinazonyesha mara kwa
mara katika mji huo na ndege zinazoruka
na kutua katika uwanja huo kutokuwa na ratiba maalumu.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya shughuli za upanuzi wa uwanja,
waziri wa uchukuzi Dr.Harrison Mwakyembe
amesema kuwa ameridhishwa na shughuli zinazofanywa za upanuzi wa uwanja huo ,
amesema serikali itaweka utaratibu wa kuondoa vikwazo anavyokutana navyo
mkandarasi vinavyopunguza kasi yake ya upanuzi wa uwanja huo ili uweze kumalizika
kwa wakati.
Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba unatarajia kugharimu
zaidi ya shilingi bilioni 21 na unatarajia kumalizika mwezi agosti, mwaka huu,
katika ziara hiyo Waziri Mwakyembe aliambata na naibu waziri wake Dr. Charles
Tizeba.
No comments:
Post a Comment