Thursday, March 05, 2015
WAZIRI MKUU AWAPA POLE WAFIWA, AWAFARIJI MAJERUHI KAHAMA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametembelea baadhi ya familia zilizopoteza
wapendwa wao pamoja na majeruhi waliolazwa kwenye hospitali ya wilaya
ya Kahama kutokana na maafa ya mvua ya mawe iliyonyesha usiku wa
kuamkia jana.
Akizungumza na wafiwa katika vijiji vya Mwakata na Magugung’hwa katika
kata ya Mwakata wilayani Kahama leo mchana (Alhamisi, Machi 5, 2015)
Waziri Mkuu alisema Serikali haitawaacha katika kipindi hiki kigumu
walichonacho.
Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuwafikishia wafiwa na waathirika
wa maaafa hayo salamu kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwaomba
wawe na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
Akiwa katika shule ya msingi Mwakata ambako watu 250 wanahifadhiwa
hapo kwa muda, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao pamoja na wananchi
waliofika kumsikiliza kwamba Serikali imepanga kuleta vyakula, mahema,
mablanketi na madawa ya hospitali ili kuwasaidia waathirika hao.
“Serikali haitaacha mtu afe kwa njaa,” alisema.
Pia aliagiza maghala ya NFRA yaliyoko Isaka yatumike kupokea misaada
ya chakula kwa sababu yako karibu sana kata ya Mwakata. “Ili uratibu
wa misaada uweze kufanyika hapa kijijini, ni vema maghala ya kuhifadhi
chakula cha msaada yakahamia hapa Isaka kwa sababu ni karibu sana na
hapa Mwakata,” alisema.
“Yakiwa hapa itasaidia usimamizi na uhakika wa huduma zinazotolewa kwa
waathirika. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya simamieni hilo kwa sababu
janga hili ni letu na linabebwa na Serikali,” aliongeza.
Alisema ameongea na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid
na kumwagiza atume watu wake wafanye tathmini ya hali ya afya kwani
katika hali ya majanaga kama haya, ni lazima kuna hatari ya kutokea
kwa magonjwa ya mlipuko.
Mapema, Mbunge wa Msalala, Bw. Ezekiel Maige aliiomba Serikali itume
misaada ya haraka ya vyakula na mahema kwa waathirika hao lakini pia
ipeleke kikosi cha wanajeshi ili wasaidie kujenga nyumba za watu
walioathirka kama ambavyo ilifanya kwa watu wa Kilosa mwaka 2009.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), Bibi Jenista Mhagama ambaye anasimamia idara ya
maafa ameuagiza uongozi wa wilaya ya Kahama kuhamishia timu ya
waratibu wake kwenye eneo la tukio badala ya kufanyia kazi kutoka
makao makuu ya wilaya ambako ni zaidi ya km. 30.
“Misaada iasche kuratibiwa wilayani bali ihamie hapa Mwakata, na hao
wanaotoa misaada waambiwe wailete hapa kwenye eneo la tukio … uratibu
ukifanyika kule hakuna atakayekuwa na picha halisi ya nini kinaendelea
kwenye kijiji hiki,” alisisitiza.
Mvua hiyo imesababisha vifo vya watu 42 na kujeruhi watu 98 huku mamia
watu wakiwa hawana mahali pa kuishi. Pia watu 52 kati ya 112 waliokuwa
wamelazwa hospitalini wameruhusiwa kurudi majumbani huku majeruhi 60
wakiendelea kupatiwa matibabu.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment