Ndugu
Wananchi;
Kama ilivyo ada tunamshukuru Mwenyezi
Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuzungumza kupitia utaratibu wetu huu mzuri
wa hotuba za kila mwisho wa mwezi. Kwa
mwisho wa mwezi wa Februari nina mambo matano ninayopenda kuyazungumzia.
Zoezi
la Uandikishaji Wapiga Kura
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la kwanza ni uandikishaji wa Wapiga Kura.
Tarehe 24 Februari, 2015 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter
Pinda alizindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya zoezi la
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini. Zoezi hili lilizinduliwa Makambako, Mkoani
Njombe na litaendelea nchini kote mpaka litakapokamilika kwa mujibu wa ratiba
itakayopangwa na Tume ya Uchaguzi.
Uandikishaji unatumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za
vidole (BVR) na macho ya mtu anayeandikishwa.
Teknolojia hii itatusaidia kuondoa kutoaminiana, manung’uniko na madai
kuhusu udanganyifu katika chaguzi zetu kwamba wamepiga kura wasiostahili. Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni
kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi yetu iwe na chaguzi zilizo huru,
wazi na haki.
Ndugu
Wananchi;
Mtakumbuka kuwa, kabla ya uzinduzi wa
zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya zoezi la majaribio ya
uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mashine za teknolojia hii mpya katika
kata 10 katika Halmashauri za
Kinondoni, Kilombero na Mlele kati ya tarehe 15 hadi 23 Desemba, 2014.
Habari njema ni kuwa, kwa kutumia
mashine za BVR, idadi ya waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa
kipindi kilichopangwa katika Kata hizo.
Katika Halmashauri ya Kilombero walioandikishwa walifikia asilimia 110.9 ya lengo, katika Halmashauri
ya Mlele uandikishaji ulifikia asilimia 101
ya lengo na katika Jimbo la Kawe, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni
walioandikishwa walikuwa asilimia 105.67
ya lengo. Mafanikio haya ni ya kutia moyo pamoja na changamoto
za kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo wenyewe kwa
watumiaji. Changamoto hizo zimefanyiwa
kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji
wa wapiga kura nchi nzima.
Ndugu
Wananchi;
Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la
uboreshaji wa Daftari na uandikishaji wa wapiga kura limeanza vizuri
Makambako. Wananchi wamejitokeza kwa
wingi kuliko ilivyotarajiwa. Kati ya tarehe
23 hadi 25 Februari, 2015 kwa mfano, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi
kuwa mkubwa wameweza kuandikisha wapiga kura 13,042. Kila kituo kilikuwa kinaandikisha
kati ya wapiga kura 80 na 150 kwa siku. Lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako
kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320. Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana
wameandikisha hadi wapiga kura 6,000
kwa siku. Kwa kasi hii na kama mambo
yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo hilo litafikiwa na hata kuvukwa.
Ndugu
Wananchi;
Hatuna budi kutoa pongeza kwa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kwa hatua hii ya kutia moyo tuliyofikia katika mchakato
huu. Inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni
mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa. Tunachokitaka kwa Tume ni kuona zoezi hili
linaendelea na kukamilika kama ilivyopangwa. Napenda kurudia ahadi
niliyokwishaitoa kwa Tume kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana
kuiwezesha kirasilimali ili iweze kutimiza jukumu lake hilo. Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa
zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa.
Hivyo basi, nimewataka wahakikishe kutoa kipaumbele cha kwanza katika
mgao wa fedha. Kama haifanyiki nawaomba
Tume waniambie mimi mwenyewe.
Wito wangu kwenu, wananchi wenzangu, ni
kujitokeza bila ya kukosa kwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya
uandikishaji katika maeneo yenu kama itakavyotolewa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi. Msifanye ajizi maana hakutakuwepo
na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya
fursa hii kupita.
Ndugu
Wananchi;
Kama ilivyoelezwa na Tume na mimi
kusisitiza mara kadhaa kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura
ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Vitambulisho
vya zamani vya mpiga kura havitatumika, hivyo watu wote ambao ni Watanzania na
wana umri wa miaka 18 au zaidi lazima wajitokeze kuandikishwa upya. Watu pekee
ambao hawatapaswa kujiandikisha tena ni wale tu walioandikishwa katika zoezi la
majaribio lililofanyika katika zile kata 10
za Halmashauri za Kinondoni, Ifakara na Mlele mwezi Desemba, 2014. Vitambulisho walivyopata ndivyo vyenyewe.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba
viongozi wa vyama vya siasa, Serikali, dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali
na Tume ya Uchaguzi katika kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi
wakajiandikishe. Naomba tusiwachanganye
wananchi kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha
kujiandikisha. Sisi katika Serikali tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha
kuwa kila atakayejitokeza kujiandikisha anaandikishwa. Aidha, tutahakikisha kuwa
kila panapojitokeza changamoto zinatafutiwa ufumbuzi kwa wakati mwafaka.
Tunatambua kuwa mfumo huu ni mpya
hivyo panaweza kujitokeza changamoto zinazosababishwa na upya wake. Nawaomba wahusika kuendelea kuwaelimisha
watendaji wanaohusika ili wapate uzoefu unaostahili. Aidha, nawasihi wananchi kuwa wavumilivu na
waelewa pale ambapo wakati mwingine watalazimika kukaa kwenye mistari kwa muda
mrefu kusubiri kujiandikisha, au wakalazimika kuja siku ya pili.
Ndugu
Wananchi;
Kupiga kura kuamua kuhusu Katiba
Inayopendekezwa au kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani ni haki na wajibu wa kila
raia. Lakini, kuipata haki hiyo na kuweza
kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na kitambulisho cha mpiga kura. Bila ya hivyo haiwezekani. Haya shime jitokezeni, mjiandikishe, ili
muweze kuitumia haki yenu na kutimiza wajibu wenu wa kuipigia kura Katiba
Inayopendekezwa na kuchagua viongozi mnaowaona wanafaa kuongoza nchi yetu,
jimbo lako na kata yako.
Kura
ya Maoni
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu Kura ya Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa. Kama mjuavyo,
baada ya Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa na Rais
kuchapisha Katiba hiyo katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga
kura ya maoni, kinachoendelea sasa ni matayarisho ya kufanyika kwa kura
hiyo. Yapo majukumu ya Serikali, yapo
majukumu ya Tume ya Uchaguzi, na yapo majukumu ya Serikali na Tume kwa
pamoja. Utekelezaji umeishaanza na
unaendelea. Miongoni mwa mambo
yanayotakiwa kufanyika ni uandikishaji wa wapiga kura ambao umekwishaanza na
unaendelea.
Ipo pia kazi ya kuchapisha na kusambaza Katiba
Inayopendekezwa ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa kabla ya kupiga kura ya
maoni. Tayari Katiba Inayopendekezwa imetangazwa
katika tovuti za Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Vijana na Michezo na katika tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia imechapichwa magazetini.
Hadi tarehe 27 Februari, 2015 vitabu 1,558,805 vilikuwa vimechapishwa na nakala
1,341,300 kusambazwa. Nakala 1,141,300
zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya
Tanzania Bara na nakala 200,000
zimegawiwa kwa Zanzibar. Kwa upande wa
Tanzania Bara kila Kata imepewa vitabu
300. Kwa vile Kata zina wastani wa
vijiji vitano (5) hii ina maana
kwamba kila kijiji kimepata vitabu 60
kwa kila kijiji ambayo si haba.
Ndugu
Wananchi;
Tume ya Uchaguzi itatoa maelekezo
kuhusu utaratibu wa kutoa elimu kwa umma.
Nimeambiwa tayari asasi za kiraia 420
kwa upande wa Bara na 75 kwa
upande wa Zanzibar zimejiandikisha kwa ajili ya zoezi hilo. Halikadhalika, Tume
itatoa maelekezo husika kuhusu kampeni ya Kura ya Maoni wakati ukiwadia. Naomba watu wawe na subira na kuzingatia
masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake. Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la
kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu. Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa,
amani na usalama.
Hali
ya Usalama Nchini
Ndugu
wananchi;
Jambo
la tatu ninalotaka kulizungumzia ni hali ya usalama nchini. Kwa jumla hali ya usalama ni nzuri, hata
hivyo kuna matukio ya kiusalama ambayo ningependa kuyazungumzia. La
kwanza ni mashambulizi yenye sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi. Na, la pili
ni la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Katika kipindi cha miezi 12 hivi kumekuwa
na matukio ya watu kuvamia vituo vya Polisi, wengine wanachoma moto au wengine
wanapora silaha. Pia kumekuwepo na matukio
ya kuwashambulia Polisi walioko kwenye doria na wengine kuporwa silaha. Vituo vya Polisi vilivyovamiwa na silaha
kuporwa ni vya Newala Mkoani Mtwara silaha tatu
ziliporwa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji silaha saba, Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga silaha tano, mbili za polisi na
tatu za raia waliokwenda kuzihifadhi pale, na Ushirombo Wilaya ya Bukombe silaha
18.
Pugu Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na
doria walishambuliwa na kuporwa silaha tatu. Kule Songea kulikuwepo na matukio mawili ya
Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.
Bahati mbaya, vijana wetu saba wa Jeshi la Polisi walipoteza
maisha katika matukio hayo. Newala alikufa
Polisi mmoja, Kimanzichana mmoja, Ikwiriri wawili, na Ushirombo watatu.
Wapo Polisi kadhaa waliopata majeraha ya namna mbalimbali katika mashambulizi
haya.
Ndugu
Wananchi;
Silaha zote 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa. Katika tukio la Tanga silaha moja kati ya mbili zilizoporwa imepatikana.
Watuhumiwa saba wametiwa
mbaroni, wanne kati yao ni wale waliokuwa wamejifisha katika
mapango ya Kiomoni katika Kitongoji cha Karasha-mikocheni, kilichoko kijiji cha
Mzizima wilayani Tanga. Tayari watu wanne
wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri wamekamatwa. Polisi wanaendelea na upelelezi kuwapata watu
wengine na kuzipata silaha saba
zilizoporwa kituoni hapo. Kwa tukio la
Newala silaha zote tatu zimepatikana
pamoja na bastola moja ya mtuhumiwa aliyehusikaa na watu wawili
wametiwa nguvuni. Hali kadhalika,
upelelezi unaendelea wa kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka
sasa: yaani Kimanzichana moja, Pugu
Machinjioni moja na Tanga iliyosalia
moja.
Ndugu
Wananchi;
Matukio haya yana sura mbili. Yana sura ya ujambazi, lakini pia baadhi yake
yana dalili za ugaidi. Vyombo vyetu vya
usalama vinaendelea kufanya kazi yake ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa
nafasi yake stahiki. Napenda kutumia nafasi
hii kutoa pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi wakishirikiana na Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya usalama kwa kazi kubwa na
nzuri waifanyayo kupambana na uhalifu nchini.
Mafanikio tunayaona, kama nilivyoeleza na kama tulivyosikia kule Tanga
hivi karibuni ni matunda ya ushirikiano huo.
Hata hivyo, nimewataka waendelee kuwasaka watu hawa waovu po pote walipo
ili wafikishwe mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi silaha zote
zilizoporwa.
Nawaomba wananchi wenzangu wote kushirikiana
kwa karibu na vyombo vya usalama hususan Jeshi la Polisi ili tuweze kupata mafanikio
zaidi dhidi ya uhalifu huu na uhalifu mwingineo. Nawaomba mfanye mambo
mawili: Kwanza, toeni taarifa Polisi mnapozipata habari za vitendo viovu au
nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu au taarifa za wale
waliokwishafanya uhalifu.
Pili,
naomba watu waache kuwashabikia watu hawa waovu wala kueneza taarifa zao potofu
kwenye mitandao ya kijamii. Badala yake
tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na vitendo
vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya wayafanyo. Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza
wananchi wote walioweza kutoa taarifa zilizowezesha kuzuia uhalifu usifanyike au
zilizowezesha kutiwa mbaroni kwa wahutumiwa wa vitendo vya ujambazi na
ugaidi. Hatuwezi kushinda uhalifu bila ushirikiano baina
ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.
Mauaji
ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
Ndugu
wananchi;
Nimesikitishwa sana na taarifa kuwa
mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yameibuka upya baada ya hali
kuwa tulivu mwaka 2011. Mwaka jana (2014)
yalitokea matukio matatu katika
mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio moja mkoani Geita.
Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu
zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo
havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote ya watu waliostaarabika, ya
watu wanaomuabudu Mungu. Watu wenye
ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata
hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine. Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa. Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao,
mtaa wao au katika nchi yao. Jamii nzima
na sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha
usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo
kwa watu wengine wote.
Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo
linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa letu. Ni vitendo visivyovumilika. Hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha
kuwa tunapambana nao kisawasawa na kuwashinda.
Tusikubali kamwe wakaturudisha kule kubaya tulikokuwa zamani. Naungana
na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote
wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe Mahakamani na
kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa wakati
wote Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa
hai. Tumefanya hivyo bila ya kuchoka tangu
tukio la kwanza baada ya mimi kuingia madarakani Aprili 17, 2006 na miezi
mitatu tu kule Nyahunge, Geita alipouawa
Alfa Amon ambapo watuhumiwa wawili waliuawa na raia. Mwaka 2007 kulikuwa na matukio saba.
Mwaka 2008 ndio ulikuwa mwaka mbaya sana walipouawa watu 18.
Kutokana na jitihada kubwa
zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi mauaji yalipungua na kuwa
tisa mwaka 2009. Mwaka 2010 kukawa na tukio moja na mwaka 2011 hapakuwepo na tukio
lolote. Mwaka 2012 kukawa na tukio moja, mwaka 2013 aliuawa mtu mmoja na wawili kujeruhiwa. Mwaka
2014 waliuawa watu watatu na wawili kujeruhiwa, na Januari, 2015
kumetokea tukio moja kule Geita.
Ndugu
Wananchi;
Tangu mwaka 2006 mpaka 2015,
watuhumiwa 139 wametiwa nguvuni,
miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa
matukio ya Desemba na Januari mwaka huu. Mashauri 35 yamefunguliwa mahakamani na kati ya hayo 10 bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 73 wameachiliwa na 15
wamepatikana na hatia. Kati ya hao waliopatikana
na hatia 13 wamehukumiwa kifo na
wawili wamepata kifungo cha miezi 6.
Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa.
Matukio ya mauaji ya watu wenye
ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa kumi
kati ya mikoa 30 hapa nchini. Mikoa hiyo ni hii ifuatayo: Mwanza matukio 13, Kagera sita, Tabora matano, Geita manne, Mara manne,
Kigoma manne, Simiyu matatu, Shinyanga mawili, Arusha moja na
Mbeya moja. Utaona matukio 41 kati ya 43 yametokea katika
ukanda wa ziwa ambapo pia wanaongoza kwa mauaji ya vikongwe na wanawake kwa
sababu za ushirikina.
Ndugu
Wananchi;
Inawezekana kuwa matukio ya hivi
karibuni yanaashiria kuwa uhalifu huu unataka kuibuka upya. Napenda
kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na Watanzania kwa jumla, kuwa
hatutaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Tutatumia mbinu na maarifa tuliyoyatumia
kukabili wimbi kubwa la mauaji lililokuwepo mwaka 2007 na 2008 na kwa sababu
hiyo tukaweza kupunguza hadi kufikia kutokuwa na tukio lolote la mauaji mwaka
2011.
Tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni
ushirikiano na msaada wa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na
kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Pia wasaidie kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga
wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino.
Ushirikiano wa wananchi wa wakati ule uliwezesha kupatikana kwa mafanikio
niliyaeleza. Naamini safari hii
tukifanya hivyo tutafanikiwa pia.
Ndugu
Wananchi;
Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na
ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana. Hata hivyo, litategemea watu kuacha imani za
ushirikina. Imani potofu, ati kuwa mtu
akiwa na kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi atafanikiwa katika shughuli
zake za biashara, uvuvi na uchimbaji wa madini ndicho kichocheo cha uovu wote
huu unaoendelea. Ni ujinga ulioje kwa
mtu kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake bali
kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa ngozi.
Nilisema katika hotuba yangu ya mwisho
wa mwezi Machi, 2008 kwamba, kama kuwa na kiungo cha albino ndiko kutakakomfanya
mtu kufanikiwa katika shughuli zake za kibiashara na kiuchumi basi ndugu zetu
wenye ulemavu wa ngozi wangekuwa ndiyo matajiri wakubwa nchini na duniani. Maana wao sio tu wana viungo bali wana mwili
mzima. Kwa sababu ya kuwepo imani hizi za hovyo, juhudi
za kuelimisha jamii kuachana na imani hizi potofu ziongezwe. Naomba hili ndilo liwe jambo la msingi katika
mapambano haya. Tukifanikiwa katika hili,
matatizo yote haya yatakoma. Serikali na
jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya ambayo siyo tu ni fedheha hata
kumsimulia mtu bali yanatisha na kusikitisha.
Ndugu
Wananchi;
Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya
viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi. Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili
niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya
kumaliza tatizo hili. Mimi naamini kuwa ushirikiano
wa karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu
zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii.
Ziara
ya Zambia
Ndugu
Wananchi;
Tarehe 25 na 26 Februari, 2015 nilifanya
ziara ya siku mbili ya kiserikali nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais mpya wa nchi
hiyo, Mheshimiwa Edgar Lungu. Ziara
ilikuwa na mafanikio makubwa. Mimi na
ujumbe wangu tulifarijika sana kuona kuwa mawazo ya nchi zetu mbili
yanashabihiana sana kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha uhusiano wetu na ushirikiano
na uhusiano wa nchi zetu mbili. Kimsingi
tumekubaliana katika masuala yote muhimu tuliyoyazungumza.
Kuhusu TAZARA tumekubaliana kuchukua
hatua thabiti kutatua matatizo ya kiungozi, kifedha na kiufundi yanayolikabili
shirika letu hilo hivi sasa. Tumeelewana
kuwa hatuna budi kufanya marekebisho ya kimfumo na kiutendaji ili kutatua
matatizo ya kimuundo na kimenejimenti yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa Shirika. Tumekubaliana pia kuwa, Serikali zetu mbili
zitekeleze ipasavyo wajibu wake kwa TAZARA ikiwa ni pamoja na kutoa mchango
wake wa fedha kwa ajili ya kulifufua Shirika hili muhimu kwa uchumi wa nchi
zetu mbili.
Ndugu
Wananchi;
Tumekubaliana pia, kwamba, tuangalie
uwezekano wa kuruhusu makampuni au mashirika mengine ya reli kutumia reli ya
TAZARA kusafirishia mizigo yao kwa kulipa ushuru kwa TAZARA kwa huduma
hiyo. Tumeagiza Baraza la Mawaziri
kulifanyia kazi wazo hili jema ili litekelezwe mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wa sekta ya nishati,
tumekubaliana kuwa, nchi zetu mbili
ziendelee kushirikiana kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA. Ndugu zetu wa
Zambia walitueleza dhamira yao ya kutaka kujenga bomba la kusafirisha gesi
kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.
Wameomba tukubali kuwauzia gesi asilia.
Niliwaeleza ni jambo linaowezekana, tumekubaliana nchi zetu zilifanyie
kazi ombi hilo.
Serikali ya Zambia, imeahidi
kuimarisha njia ya umeme kutoka Kasama hadi Mbala Zambia inakoanzia njia
inayoleta umeme Sumbawanga. Kufanya
hivyo kutaondoa matatizo ya sasa ambapo umeme unaofika Sumbawanga kutoka Mbala huwa
mdogo kiasi kwamba hauna nguvu ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, maofisini
na viwandani. Kwa sababu hiyo, hata
mpango wa kuupeleka umeme huo Namanyere, Nkasi na Mpanda haukuweza kutekelezwa
kama ilivyokuwa imekusudiwa awali.
Ndugu
Wananchi;
Kuhusu kuboresha huduma kwa abiria na
mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia pale Tunduma, tumekubaliana kuwa, Serikali
ya Tanzania ikamilishe ujenzi wa jengo litakalowezesha
huduma zote muhimu za mpakani kutolewa katika jengo hilo (One Stop Border Post). Wakati tunasubiri kukamilisha ujenzi huo,
tumekubaliana tuwe na jengo la muda la kurahisisha taratibu za usafiri wa
abiria na usafirishaji wa mizigo katika mpaka wetu na Zambia.
Vilevile, tulizungumzia njia za kuimarisha
na kuboresha taratibu za forodha kwa mizigo itokayo bandari ya Dar es Salaam
kwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Zambia. Tumekubaliana kuwa, Mamlaka ya Kodi ya Mapato
ya Zambia iangalie uwezekano wa kuwaweka maafisa
wake katika Bandari ya Dar es Salaam kama inavyofanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Hii itarahisisha
taratibu za forodha kwa bidhaa za Zambia katika bandari yetu. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshaanza
mchakato wa kupata fursa hiyo. Kwa jumla,
ziara ilikuwa ni yenye mafanikio makubwa.
Rambirambi
Ndugu
Wananchi;
Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi
hotuba hii tukapata habari ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa
Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Capt. John Damian Komba. Kifo chake kimeliondolea taifa letu mmoja wa viongozi
wake wazuri, msanii mahiri, raia mwema na mzalendo wa kweli. Marehemu alitumia muda mwingi wa maisha yake
kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo akiwa mwalimu na baadaye
Kiongozi wa Kikundi cha Sanaa cha JWTZ na hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha
Tanzania One Theatre cha Chama Cha Mapinduzi.
Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake ametoa mchango mkubwa kwa
maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa Chama Tawala. Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema
aliyoifanyia jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.
Ndugu
Wananchi;
Katika salamu zangu za rambirambi kwa
Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa CCM niliwaomba kupitia kwao salamu ziwafikie
Wabunge wote na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Hali kadhalika, niliomba kupitia kwao salamu
ziwafikie familia ya marehemu Capt. John Komba.
Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda kuwahakikishia kuwa tuko pamoja nao katika
kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.
Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na uvumilivu. Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole
nyingi kwa msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata. Nawaomba watambue kuwa namna bora zaidi ya
kumlilia Mbunge wao aliyewapenda ni kudumisha mema yote aliyofanya na
kukamilisha zile kazi ambazo alikusudia kuzifanya lakini hakuweza kufanya hivyo
kwa sababu ya kukutwa na umauti.
Mwisho nawaomba, Watanzania wote
tuungane na familia yake kumwombea marehemu Capt. John Damian Komba mapumziko
mema. Amin.
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu
Ibari ki Tanzania!
Asanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment