Rais wa Jamhuri ya
Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame amesema kuwa hatua ya Mwenyekiti wa Nchi
Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Rais Jakaya Mrisho Kikwete
kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Nchi Zilizoungana Kutekeleza Miradi ya
Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects ni hatua
muhimu katika kufungua utekelezaji wa miradi ya miundomninu katika kanda
nyingine za EAC.
Aidha, Rais Kagame
amemshukuru Rais Kikwete kwa uamuzi wake kuhudhuria Mkutano huo uliofanyika
leo, Jumamosi, Machi 7, 2015, katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Serena
mjini Kigali, Rwanda. Rais Kikwete amefanya ziara hiyo ya siku moja kuhudhuria
Mkutano huo kwa mwaliko wa Rais Kagame.
Naye Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete
ameweza kuhudhuria Mkutano wa leo, kwa sababu sasa njia imefunguka kuanza kazi
ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central Corridor unaokatisha
katikati ya Tanzania.
Marais Kagame na
Kenyatta walikuwa wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi za Mkutano huo
uliofanyika kwa kiasi cha saa mbili unusu mara baada ya Rais Kikwete kuwasili
Kigali akitokea Dar es Salaam kiasi cha saa sita mchana.
Akifungua Mkutano
huo, Rais Kagame alisema: “Nawashukuru waheshimiwa marais wote kwa kuja. Lakini
hasa hasa, namshukuru sana mwenyekiti wetu wa EAC Rais Kikwete kwa kupata muda
wa kuja kujiunga nasi katika mkutano huu.”
Aliongeza Rais Kagame
huku makofi yakiendelea kumkaribisha na kumshangilia Rais Kikwete: “Kuwepo
kwake hapa leo, kunaongeza matumaini kuwa miradi mbali mbali na mingi zaidi
katika kanda mbali mbali za nchi zetu wanachama wa EAC, sasa inaweza
kutekelezwa kwa haraka zaidi. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais.”
Mbali na Marais Kikwete,
Kagame na Kenyatta, Mkutano wa leo pia umehudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa
Uganda, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Makamu wa Rais wa Pili wa Burundi na
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia.
Nchi za Kenya,
Uganda,Rwanda na Sudan Kusini ndizo wanachama wa Northern Corridor na kwenye
mkutano wa leo, Burundi pia imetangaza kuwa imeamua kuwa mshiriki kamili wa
mikutano ya Ukanda huo badala ya kuwa msikilizaji kwa muda mrefu.
Akizungumza katika
Mkutano huo, Rais Kenyatta amesema: “Tunafurahi sana kwamba Mwenyekiti wetu wa
EAC yuko nasi leo kwa sababu uwepo wake utaongeza msukumo wa kutuwezesha kuanza
utekelezaji wa miradi mingine hasa katika Ukanda wa Kati. Tanzania ina mengi
kuchangia katika jambo hilo. Kwa mfano, umeme mwingi ambao utaanza kuzalishwa
na Tanzania mwaka huu, unahitajika kwa nchi zote za EAC na Northern Corridor.”
Rais Kikwete ambaye
alikuwa msikilizaji tu kwa sababu Tanzania inaendelea kuwa mwanachama wa EAC
bila kuwa mshirika wa Northern Corridor amezugumza kwa ufupi tu akisema kuwa kwa
sababu yeye ni mwalikwa na msikilizaji asingeweza kusema mengi.
Amewaambia viongozi
wenzake: “Nakushukuru Rais Kagame kwa kunialika. Kama unavyojua, mimi ni
msikilizaji tu na hivyo siwezi kusema sana. Lakini napenda kuwapongezeni nyote
kwa kazi mnayoifanya. Sote tunajua kuwa hakuna utengamano bila kuendeleza
miundombinu.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Kinachoendelea kule Northern Corridor kitasaidia sana katika mawazo
na utekelezaji wa kazi ambayo tunajiandaa kuianza kwenye Ukanda wa Kati.
Nawatakieni mafanikio zaidi na kasi ya Mwenyeji Mungu katika utekelezaji wa
miradi yenu.”
Chini ya Northern
Corridor nchi hizo zimebuni miradi 14, ambayo baadhi yao imeanza kutekelezwa
ikiwa ni pamoja na kuanzisha visa moja ya kusafiria ya watalii. Nchi hizo
ziliunda kundi hilo mwaka mmoja na miezi tisa iliyopita na wakuu wa nchi
wanachama hukutana kila baada ya miezi miwili kwa mashauriano na maamuzi.
Rais kikwete amerejea
nyumbani usiku wa leo baada ya kumalizika kwa Mkutano huo.
No comments:
Post a Comment