WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ameendelea kukemea tabia za utoro na mimba kwa wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari wilayani Chunya baada ya kupewa taarifa kwamba watoto
4,420 walitoroka shule na wengine 201 kupata mimba.
Februari
26, mwaka huu, Waziri Mkuu aliwaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwasaka na kuwakamata wale wote
waliohusika na utoro na ujauzito wanafunzi na kuwafikisha mahakamani mara moja
ili liwe fundisho kwa wengine baada ya kuelezwa kwamba wanafunzi 94 walipata
ujauzito na wengine 645 kuacha shule kwa sababu ya utoro.
Akizungumza
na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumamosi,
Februari 28, 2015) kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu
alisema haiwezekani kuiacha hali hiyo iendelee huku watoto wa wilaya hiyo
wakiharibiwa maisha kwa kukosa masomo.
“Utoro
kwenye shule za msingi, taarifa ya wilaya inaonyesha watoto 1,979 waliacha
shule kati ya mwaka 2010 na 2014 ambao ni wastani wa watoto 395 kila mwaka na
katika suala la mimba, taarifa hiyo inasema watoto 161 waliachishwa shule kwa
sababu ya ujauzito,” alisema.
“Haiwezekani
kabisa! Hivi akinababa kuamua kutembea na mtoto shule ya msingi ni lipi hasa
unalolitaka kwake… unamwachisha shule mtoto kwa lipi hasa, hapana. Nimeshatoa
agizo wahusika wakamatwe. Wa zamani tunaweza tusiwapate, lakini hawa wa mwaka
jana kwa shule za msingi wako 28, RC na watendaji wako fuatilieni na muwapeleke
kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
Akichanganua
takwimu za sekondari, Waziri Mkuu alisema kati ya mwaka 2010 na 2014 wanafunzi
2,251 waliacha shule kwa sababu ya utoro na wengine 40 waliachishwa kwa sababu
ya ujauzito.
“Ninawasishi
wazazi na uongozi wa wilaya na mkoa tufanye jitihada kuhakikisha jambo
hili linakomeshwa mara moja. Huwezi kununua madaftari an kumlipia ada tu halafu
usitake kuona mwanao anamaliza shule. Kila mzazi ana jukumu la kuhakikisha
mtoto wake anamaliza shule ili awe na maisha bora hapo baadaye,” alisema Waziri
Mkuu.
“Nirudie
kuwakumbusha wazazi kwamba mtoto wa mwenzio ni mtoto wako, huwezi kukubali
maisha yaharibike hivi hivi. Tuungane pamoja kuhakikisha tunashinda vita hii,”
alisisitiza.
Waziri
Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi
ambapo mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari,
atakagua ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji
wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba.
IMETOLEWA
NA
OFISI
YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI,
MACHI MOSI, 2015
No comments:
Post a Comment