WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewatembelea askari wa Jeshi la Polisi waliolazwa kwenye Hospitali
ya Mkoa wa Mbeya kutokana na ajali waliyoipata jana wakati msafara wake
ukielekea Kata ya Galula wilayani Chunya.
Waziri
Mkuu aliwatembelea majeruhi hao na kuwapa pole leo asubuhi (Jumapili, Machi
Mosi, 2015) kabla ya kuelekea wilayani Mbozi kuendelea na ziara yake ya Mkoa wa
Mbeya. Alifuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro
na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Seif Mhina.
Akizungumzia
hali ya majeruhi hao, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Ismail Macha alisema
jana walipokea majeruhi tisa lakini watatu walifanyiwa uchunguzi wa afya zao na
kuruhusiwa na wengine sita ilibidi wawalaze na kuwafanyia uchunguzi zaidi kutokana
na hali zao zilivyokuwa.
“Wengi
wao walipata zaidi mshtuko ndiyo maana tukaamua kuwalaza ili tuendelee kuwapa
uangalizi wa karibu… Mmoja tu ndiye amevunjika mkono wa kulia lakini wengine
walipata michubuko miguuni, mikononi na usoni,” alisema.
Aliwataja
waliolazwa kuwa ni Deogratius Nandi (31), Paulin Masolwa (27), Omary Hussein
(24), Hamisi Haji (29) ambao wote ni wanaume. Majeruhi wa kike ni Cecilia Mussa
Kabona (28) na Mwazanije Hassan (23) ambaye amevunjika mkono wa kulia.
Waliopata matibabu na kuruhusiwa ni Mashaka Shabani (42), Khalifa Rashid (26)
na Joel Cheja (21).
Dk.
Macha alisema wanatarajia kuwaruhusu leo mchana ama kesho asubuhi kwani hali zao
zinaendelea vizuri.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni vumbi na
kokoto barabarani ambazo zilifanya gari hilo la FFU lisesereke na kupinduka.
Hata hivyo, alisema mwendo mdogo wa gari hilo ulisaidia kuokoa maisha ya askari
hao.
“Ajali
ilitokea saa 5:30 asubuhi eneo la Chang’ombe ya Mjele. Eneo lile lina kokoto
kubwa kubwa ambazo zilisababisha gari lao kuserereka na kupinduka… gari
halikuwa kwenye mwendo mkali ndiyo maana askari hao wamepata majeraha madogo
madogo,” alisema.
Waziri
Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo
mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua
ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa miche
ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, MACHI MOSI,
2015
No comments:
Post a Comment