SERIKALI
imesema itajitahidi kuhakikisha inalipa deni lote la mahindi yaliyonunuliwa
kutoka kwa wakulima na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ifikapo
Machi 30, mwaka huu.
Akizungumza
na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumapili, Machi
2, 2015) kwenye uwanja wa CCM wa Vwawa wilayani Mbozi, Waziri Mkuu Mizengo
Pinda alisema Serikali imedhamiria kufuta deni lote.
“Hapa
Mbozi tulikuwa tunadaiwa sh. bilioni 21 lakini tumetoa sh. bilioni 4.5 kwa hiyo
tutabakia na deni la kama sh. bilioni 16 ambalo tunajitahidi liwe limeisha
ifikapo mwishoni mwa mwezi huu,” alisema.
“Tunachoweza
kuahidi kama Serikali ni kwamba, msimu huu hatutarudia kosa la mwaka jana
ingawa mtihani mkubwa tulionao ni wa kushughulika na hifadhi ya chakula kwa
kujenga vihenge (SILOS) ili hata kama kuna ziada n tusipate taabu ya
kuhifadhi,” aliongeza.
Alisema
alishakwenda Poland kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete na wao wameshakuja
kuona hali halisi ilivyo. “Tumependekeza vihenge vijengwe kwenye kanda za
Mbeya, Rukwa, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha au Kilimanjaro na Shinyanga ili
iweze kuhudumia kanda ya Ziwa,” alisema.
Wakati huo huo, Mbunge wa Mbozi ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi amesema Serikali
imekwishalipa zaidi ya sh. bilioni 81 na kwamba deni lililosalia linafikia sh.
bilioni 59.
“Hadi
mwishoni mwa mwaka jana, tulikuwa tumeshalipa sh. bilioni 51.5/- na mwaka huu
tumepata sh. bilioni 15 kutoka CRDB na hivi majuzi kuna bilioni nyingine 15
zimetoka Hazina… Agizo la Serikali ni kwamba mahindi yote yawe yamelipwa
ifikapo Machi 30, naamini tutakamilisha,” alifafanua.
Alielezea
pia tatizo la maji linaloukabili mji wa Mbozi na vitongoji vyake na kueleza
kwamba Serikali inashughulikia tatizo hilo katika programu mbalimbali.
Mapema, akiwa katika ghala la nafaka la
NFRA katika makao makuu ya wilaya ya Mbozi, Vwawa, Waziri Mkuu alielezwa kwamba
kanda ya Makambako ambayo inajumuisha vituo vya Makambako na Vwawa imezidiwa
uwezo na sasa wanalazimika kuhifadhi magunia ya mahindi nje kwa vile maghala
yamejaa.
Meneja
wa Kanda hiyo wa NFRA, Bw. Abdillah Nyangasa alisema kanda hiyo ina uwezo wa
kuhifadhi tani za nafaka 34,000 ambapo kati ya hizo, tani 22,000 ni maghala ya
Makambako na tani 12,000 ni maghala ya Vwawa, Mbozi.
Hata
hivyo, Bw. Nyangasa alisema kanda hiyo kwa sasa kina tani za mahindi 79,496.8
zikijumuisha tani 15,738.9 za msimu uliopita licha ya tani 63,757.8 ambazo
zimenunuliwa katika msimu huu.
“Ili
kukabiliana na uhaba wa maghala, kanda yetu hulazimika kufanya hifadhi ya nje
(outside storage) kwa kutumia maturubai (tarpaulins) ili mahindi yasiharibiwe
na hali ya hewa kama mvua au jua kali,” alisema Bw. Nyangasa.
Waziri
Mkuu anamaliza ziara yake ya siku saba mkoani Mbeya leo kwa kufanya majumuisho
na kisha kurejea jijini Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment