Mkoa wa Kagera umenufaika na shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge Tanzania MKURABITA
kwa kupima mashamba ya wakulima na wafanyabiashara na kutoa hati za
kimila 1,0024 katika Halmashauri za Wilaya nne mkoani Kagera .
Katika sherehe za uzinduzi wa
ugawaji wa Hati za Kimila zilizofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi
Machi 10, 2015 jumla ya Hati za Kimila
565 ziligawiwa kwa wananchi ambao ni wakulima wa miwa pamoja na kilimo cha
mazao mbalimbali katika mashamba ya
wakulima.
Mratibu wa MKURABITA Bi Seraphia
Mgembe alisema kuwa mpango wa MKURABITA ulianzishwa Septemba 2003, utekelezaji
wake ulianza Oktoba 2004 lengo likiwa ni kurasimisha ardhi ya wanyonge ili
kukuza uchumi, kupunguza migogoro ya ardhi, na kuleta maendeleo kwa wananchi
kupitia ardhi yao.
Bi Mgembe alisema kuwa baada ya
kutumia mbinu za kitaalamu katika kurasimisha ardhi ya wananchi kukwama,
MKURABITA waliamua kuzitumia Halmashauri za Wilaya ili kuwafikia wananchi kwa
urahisi zaidi jambo ambalo linaonyesha matumaini kwa kuwa wananchi wana
mwitikio mkubwa sana hasa mkoa wa Kagera.
Aidha MKURABITA kupitia mpango
huo wa urasimishaji wa raslimali za wanyonge hasa ardhi hutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Idara ya Ardhi katika
Halamashauri na kuwawezesha vifaa vya kisasa vya kupimia ardhi ili zoezi la
upimaji na utoaji wa hati za kimila liwe
endelevu katika Halmashauri husika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe.
John Mongella aliyekabidhi hati hizo kwa wananchi 565 wa Wilaya ya Missenyi aliwashukuru MKURABITA kutoa hati hizo
kwa wananchi wa mkoa wa Kagera a
pia alisema kuwa wananchi watazitumia
hati hizo kujikomboa kiuchumi kwa kuapata mikopo toka katika taasisi za Kifedha.
Mhe.John Mangella aliwaasa wananchi waliopata
hati hizo kuzitumia kuinua uchumi wao kwa kunzia mwananchi mmoja mmoja, kaya ,
kitongoji hadi ngazi ya kijiji. Aidha aliwakumbusha kuwa maendeleo ili yawepo
kunahitajika ardhi, watu, uongozi bora na siasa safi Kama Mwlimu Nyerere alivyowahi kunena.
Aidha, aliwaagiza
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za
Wilaya katika mkoa wa Kagera kuendeleza
zoezi la kupima mashamba ya wananchi na kila baada ya miezi mitatu watoe hati
za kimila angalau 200. Vilevile waliaswa kuvitunza vifaa vya upimaji
wanavyowezeshwa na MKURABITA mara baada ya kuwajengea uwezo.
Mkuu wa Mkoa Mhe. John Mongella
aliziomba taasisi za Kifedha hasa benki ya Wakulima mkoani Kagera kuzitambua
hati za kimila na kuwakopesha wananchi wenye hati hizo bila mizengwe kwani hati
hizo zinatambuliwa na serikali kuwa ni hati halali zenye dhamana kwa mashamba
ya wananchi.
Akimalizia Mkuu wa Mkoa Mhe. John
Mongella alimwomba mratibu wa MKURABITA kuufanya mkoa wa Kagera kuwa ni mkoa wa
mfano katika kupima mashamba ya wananchi na kutoa hati za kimila kutokana na
wananchi kuonyesha mwamko mkubwa wa kupimiwa mashamba yao ili wapate hati hizo.
Naye John Rugeiyamu Mwenyekiti wa
Kijiji cha Mabuye Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kwa niaba ya wananchi waliopata hati za kimila alisema hati
zimekuja kwa wakati muafaka kwani watazitumia kupata mikopo ya kuinua uchumi wa
maisha yao na zitapunugza sana migogoro ya ardhi katika vijiji.
Meneja Msaidizi Benki ya Wakulima
Bw. Nthony Nzigula alisema wananchi waliopata hati za kimila wanaruhusiwa
kukopa katika benki yao ambayo kwa sasa ina mpango wa kufungua matawi yake
kupitia SACCOS ambazo tayari wamezibainisha kila Wilaya ili kusogeza huduma zao
karibu na wananchi.
Halmashauri za Wilaya
zilizonufaika na Urasimishaji wa Raslimali za Biashara za Wanyonge Tanzania ni
Muleba hati 3271, Ngara hati 2962,
Karagwe hati 3238, na Missenyi hati 565 jumla wakulima waliopata hati za kimila
katika mkoa wa Kagera 10,024. Aidha mwaka wa fedha 2015/16 zoezi hilo
litafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.
No comments:
Post a Comment