1) Mheshimiwa
Spika, ninakushukuru sana kwa fursa uliyonipa kutoa maelezo yangu
binafsi katika Bunge lako Tukufu leo. Ninatoa maelezo haya kwa mujibu wa
Kifungu cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013
kinachosema kwamba,
“Mbunge
yeyote anaweza, kwa idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi Bungeni
yanayolenga kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia
jamii”
2) Mheshimiwa
Spika, Nilijiunga na Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Mwaka 2015
nikiwa na lengo kuu la kupaza sauti ya vijana kwenye masuala yanayohusu
nchi yetu na kutetea maslahi ya Watanzania hususani Wananchi wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma, na Watanzania kwa ujumla.
Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Wananchi wa Kigoma Kaskazini
walinichagua tena Mwaka 2010 kupitia tiketi ya CHADEMA.
3) Mheshimiwa
Spika, kupitia fursa ya ubunge niliyopewa na wananchi wa Kigoma
Kaskazini kwa udhamini wa CHADEMA, nimejifunza mengi hapa Bungeni na nje
ya Bunge hili. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na nimejulikana ndani
na nje ya Tanzania. Muhimu zaidi ni kwamba nimepata fursa adhimu ya
kutoa mchango wangu katika kutunga sheria na sera mbalimbali kwa ajili
ya maendeleo ya nchi yetu. Aidha, nilipata fursa ya kipekee kama Mbunge
na Mwenyekiti wa Kamati zako mbili ya kuisimamia, kuishauri na
kuiajibisha serikali.
4) Mheshimiwa
Spika, Ninawashukuru sana wanachama wa CHADEMA kwa dhamana mbalimbali
walizonipa ndani ya CHADEMA. Ninawashukuru viongozi wangu na hasa
Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kunilea na kuniamini
kufanya naye kazi kwa kipindi chote tangu nilipokuwa mwanafunzi Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, katika chama na hapa Bungeni. Kama ambavyo
nimesema mara nyingi, CHADEMA imenilea na kunikuza tangu nikiwa na umri
wa miaka 16 na tangu kipindi hicho nimejifunza mengi.
5) Mheshimiwa
Spika, Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Kigoma
Kaskazini kwa mapenzi yao na imani waliyonipa na kuniwezesha kukalia
KITI hiki ninachokalia ndani ya Bunge lako Tukufu. Nashukuru kwamba juzi
nilipata fursa ya kipekee ya kuwashukuru kwa imani waliyonipa
kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Mola atawalipa wananchi wa
Kigoma Kaskazini kwa imani kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha
kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.
6) Mheshimiwa
Spika, kwa muda mrefu sasa pamekuwa na msuguano wa kiuongozi kati yangu
na viongozi wangu ndani ya CHADEMA uliosababishwa na tofauti za
kimtazamo juu ya tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama chetu.
Hatimaye tofauti hizi zilipelekea mwezi Novemba 2013 Kamati Kuu ya
CHADEMA kunivua nafasi zangu zote za uongozi nilizokuwa nazo.
Sikuridhika na maamuzi hayo na hivyo nikaonyesha kusudio la kukata rufaa
katika Baraza Kuu la chama chetu kama taratibu za kikatiba za chama
chetu zinavyotaka. Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa
hiyo, na huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka
pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya uanachama wangu
hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika
vikao vya chama. Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye
Mahakama Kuu imetoa hukumu yake tarehe 10 Machi 2015. Katika hukumu hii,
nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi letu
liliwasilishwa kimakosa.
Pamoja
na kwamba hatukuridhika na mwenendo wa jinsi kesi hii ilivyoamuliwa
pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe, ninaheshimu maamuzi ya mahakama na
sina mpango wa kukata rufaa.
7) Mheshimiwa
Spika, katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa katiba ya chama chetu,
ilitarajiwa kwamba baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu ingekaa
na kunipa rasmi mashtaka yangu yanayohusu uanachama wangu, mimi kuitwa
kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi wake. Hata hivyo, mara
baada ya hukumu ya Mahakama Kuu dunia nzima ilitangaziwa na Mwanasheria
wetu Mkuu, kwa niaba ya chama, kwamba mimi nimeshafukuzwa na sio
mwanachama tena wa CHADEMA. Baada ya hapo viongozi wangu wametoa matamko
mbalimbali yote yakionyesha kwamba sitakiwi tena katika chama hiki,
pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo sijawahi kukabidhiwa barua
yeyote inayonitaarifu kufukuzwa kwangu katika chama.
8) Mheshimiwa
Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ni wazi kwamba uanachama wangu
wa kisiasa ndani ya CHADEMA umeshaondolewa. Ninaweza kuendelea kupigania
uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na misingi yote
kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini mimi ni mwanasiasa. Sikuja
hapa bungeni kwa sababu ya kushinda kesi mahakamani. Nilichaguliwa na
wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba huwezi kuwa mbunge
bila udhamini wa chama cha siasa. Huu ndio utaratibu wa kisheria
tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi wangu katika chama ni kwamba
udhamini wa chama changu umekwishaondolewa.
9) Mheshimiwa
Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ninaomba kukutaarifu wewe na
Bunge lako tukufu kwamba sina mpango wa kuendelea kupigania uanachama
wangu wa CHADEMA katika viunga vya mahakama. Kwa hiyo ninatangaza rasmi
leo kwamba taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu nitaachia uanachama
wa CHADEMA, chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa
tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na viongozi
katika chama changu. Nimeona kuwa kuendelea kupigania uanachama
kisheria ni kutatiza na kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini
katika wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo wa vyama vingi vya
siasa. Kwa kuwa taratibu hizo sijui zitakamilika lini, natumia fursa
hii kuwaaga wabunge wenzangu.
10) Mheshimiwa
Spika, vyama vya siasa ni jukwaa muhimu katika ujenzi wa demokrasia
lakini havipaswi kamwe kuwa juu ya wananchi. Kwa hiyo ni maoni yangu
kwamba wakati sasa umefika wa kukomesha udola na ufalme wa vyama vya
siasa hapa nchini. Mfumo wa siasa ambao unavipa vyama vya siasa mamlaka
ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya wananchi haupaswi kuendelea katika
Karne ya 21 na katika nchi ambayo inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia
ya kuheshimu wananchi. Mimi ninaondoka bungeni sio kwa sababu wananchi
wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka niondoke. Siondoki kwa
sababu nimeshindwa kufanya kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki
kwa sababu wanachama wenzangu katika CHADEMA wametaka niondoke.
Ninaondoka kwa sababu mfumo wetu wa kisheria unavipa vyama vya siasa
mamlaka juu ya wananchi na wapiga kura. Ni matumaini yangu kwamba Bunge
lako tukufu halitaruhusu mfumo huu unaoruhusu vyama vya siasa kupora
mamlaka ya wananchi uendelee. Ni Bunge lako pekee lenye uwezo wa
kukomesha mfumo ambao unatukuza Parties’ Power, badala ya People’s
Power.
11) Mheshimiwa
Spika, kama nilivyosema awali kwamba vyama vya siasa ni jukwaa. Bahati
nzuri nchi yetu inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na sasa tuna
vyama 22. Kwa hivyo, wananchi wanaoniunga mkono wasisikitike kwa maamuzi
yangu ya leo. Bado ninayo fursa ya kuwatumikia kupitia jukwaa lingine
ambalo nitaamua katika siku chache zijazo, na inshala Mungu akitujalia
nitarudi tena hapa Bungeni katika Bunge la 11 kwa nguvu za wananchi.
12) Mheshimiwa
Spika, kwa miaka kumi niliyotumikia hapa Bungeni, si yote niliyoyafanya
yalikuwa sahihi, yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya
kazi zangu, kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa yote
ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu,
sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika.
13) Mheshimiwa
Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya kisiasa bila ya kulishukuru
Bunge lako Tukufu. Kwanza, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta,
mzee wa kasi na viwango! Bado ninakumbuka vizuri jinsi hoja ya Buzwagi
ilivyotikisa Bunge lake na hatimaye kupelekea nchi yetu kufanya
mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera
mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo kukuza mapato ya
sekta ya madini kutoka Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450
bilioni kwa mwaka.
14) Mheshimiwa
Spika, ninajivunia kuwa sehemu ya Bunge la Kumi chini yako, Mama
shupavu Anna Semamba Makinda. Katika Bunge hili nimekuzwa, nimejifunza,
nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja
tumepigania maslahi ya wananchi wetu kwa juhudi na maarifa na hivyo
kuleta mabadiliko kadhaa. Ni katika kipindi hiki ambapo wabunge tumekuwa
na sauti. Bunge la Tisa lilijijenga likawa ‘Bunge lenye Meno’ katika
kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye Nguvu’ katika
mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya
kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu. Na katika siku
za hivi karibuni Bunge la Kumi litakumbukwa kwa Hoja Maalumu ya Tegeta
Escrow iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia Baraza la
Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa
katika miaka iliyopita.
15) Mheshimiwa
Spika, wajumbe wa PAC ( ambao nimeishi nao kama familia ) tumekuwa
nguzo kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi.
Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa kunipa
ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa kwa
miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye nia ya dhati ya
kuitumikia nchi yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile
bila woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu
na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi. Pamoja na kwamba
ninaondoka Bungeni leo, ninaahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa
Kigoma Kaskazini na Taifa langu katika kusimamia ukweli, kutetea
demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa
kawaida bila ubaguzi wowote.
16) Mheshimiwa
Spika, Kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA, najivunia kwa fursa
mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia
kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Inawezekana tusiweze
kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini
ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika dhamira kubwa ya
kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote
ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira na
kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, yaani Taifa la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika
harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na
unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu
binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.
17) Mheshimiwa
Spika, Ninawashukuru tena na tena wana Kigoma na wananchi wote wa
Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka
takribani kumi. Ninawahakikishia kuwa changamoto nilizokumbana nazo na
ambazo zimenilazimisha leo niondoke bungeni zimechochea zaidi dhamira,
nia na sababu yangu ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi kuliko wakati
mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya.
Mheshimiwa Spika,
Asanteni sana na Kwa herini!
No comments:
Post a Comment