Thursday, March 19, 2015

SERIKALI YASAMBAZA NAKALA MILIONI 1.3 ZA KATIBA PENDEKEZWA *Nakala zaidi ya 650,000 kusambazwa kwenye taasisi







WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema hadi kufikia Februari 26, mwaka huu,
Serikali imekwishasambaza jumla ya nakala 1,341,300 za Katiba
Inayopendekezwa Kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni jijini Dar
es Salaam, jana jioni (Jumatano, Machi 11, 2015) Waziri Mkuu alisema
Zanzibar imepatiwa nakala 200,000 na kuongeza kuwa nia ya Serikali ya
kuchapisha nakala milioni mbili iko palepale.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alibainisha kwamba nakala 658,700 zilizobakia
zitagawanywa Kwenye wizara zote za Tanzania Bara na Zanzibar,
Mahakama, Bunge, Baraza la Wawakilishi, taasisi za Serikali, Tume
zote, taasisi za dini, asasi za kiraia, vyombo vya sheria, vyuo vya
elimu ya juu, vyama vya siasa na na taasisi zinazojitegemea ili
kuongeza wigo wa usambazaji kwa wananchi wengi zaidi.

“Lazima nikiri kwamba kuzisambaza na kuzifikisha kwa walengwa ni jambo
moja na kuhakikisha kwamba zinasomwa ni jambo jingine. Wito wangu kwa
Watanzania wote ni kuhakikisha wanasoma na kuielewa Katiba
Inayopendekezwa ili wanapokuja kupiga kura waelewe ni nini wanafanya,”
alisema.

“Niwasihi sana Watanzania wenzangu, wasikubali kurubuniwa juu ya
kilichoandikwa Kwenye Katiba Inayopendekezwa, na tena mtu asikubali
kuombwa kuomba auze nakala yake. Tusikubali watu warubiniwe kirahisi.
Kila mmoja ahakikishe anaisoma na kuielewa, na wenye mitandao na blogs
watumie fursa hii kuusambazia umma nakala za Katiba hii ili watu wengi
zaidi waweze kuisoma,” alifafanua.



IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM



No comments:

Post a Comment