TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewataka Watanzania washirikiane
na wazazi na walimu kuhakikisha watoto wa kike wanasoma kwa bidii na kutimiza
ndoto zao za ukubwani.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 20, 2013)
wakati akizindua Mradi wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi
Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara. Mradi huo
unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo,
umelenga kuwafikia wasichana 10,513 katika wilaya mbili za mkoa wa Mtwara,
yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Kabla ya kuzindua mradi huo, Mama Pinda aliwaita
wasichana watatu na kupanda nao jukwaani na kuwahoji mmoja baada ya mwingine
kwamba wangependa kufanya nini wakiwa wakubwa.
Mwanafunzi wa kwanza, Rahma Jamaldini (14) anayesoma
darasa la saba katika shule ya msingi Chikongola alijibu kwamba yeye angependa
kuwa rubani na akaambiwa na Mama Pinda ajitahidi katika masomo ya sayansi na
hisabati ili asome hadi Chuo Kikuu kuweza kutimiza ndoto yake hiyo.
Wa pili alikuwa ni Eliza Paulo (8) mwanafunzi wa darasa
la pili katika shule ya msingi Chikongola aliyesema angependa kuwa mama. Aliwavunja
mbavu watu waliohudhuria uzinduzi huo alipoulizwa tena ni kitu gani angependa
kufanya mbali ya kuwa mama kwa kujibu kwamba angependa kupika. Alipoulizwa mara
ya tatu kitu kingine ambacho angependa kufanya, akajibu kuosha vyombo. Mama Pinda
allimhimiza asome kwa bidii ili awe mama mzuri.
Wa tatu alikuwa ni Bora Hamisi (8) ambaye pia ni mlemavu
wa ngozi. Bora anasoma darasa la pili katika shule ya msingi Msufini mjini
Mtwara. Yeye alisema angependa fundi wa kushona nguo. Naye aliambiwa asome kwa
bidii hasa somo la stadi za kazi.
Mama Pinda alisema amewaita watoto hao ili wawe mfano wa
kudhihirisha ndoto na matamanio ambayo watoto wa kike wanayo na kwamba wasiposaidiwa
kwa kuwekewa mazingira mazuri yatakayowafanya wahitimu masomo yao, kamwe
hawataweza kutimiza ndoto zao.
“Watawezaje kutimiza ndoto zao kama hawahudhurii masomo kama
wanafunzi wengine? Wanapaswa wasome vizuri, waende sekondari na hata vyuo vya
elimu ya juu. Tuweke miundombinu itakayowasaidia kuhudhuria masomo bila kukosa,”
alisema.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa TMARC, Bi. Diana Kisaka alisema
mradi huo umelenga kuinua uelewa wa wasichana kuhusu miili yao na mabadiliko
yanayotokea katika kipindi cha balehe; kuwapa ufahamu kuhusu makundi mbalimbali
miongoni mwa jamii iliyowazunguka na kuwapa upeo wao kuhusu umuhimu wa
kuzingatia malengo yao katika maisha.
Naye Mkuu
wa Vodacom Foundation, Bw. Yesaya Mwakifulefule alisema Vodacom Foundation imechangia
sh. milioni 160 kwenye Mradi wa Hakuna Wasichoweza kwani inatambua umuhimu wa
elimu na suala zima la kuendeleza wasichana kielimu.
“Vodacom Foundation inashugulika na masuala ya elimu kwa
kuchangia madawati na teknolojia ya habari na mawasiliano katika shule
mbalimbali hapa nchini. Hapa Mtwara tumetoa kompyuta 20 kwenye shule ya sekondari
ya wasichana ya Mtwara ambazo zimeunganishwa na intaneti ya Vodacom,” alisema.
Naye
mwakilishi kutoka Shirika la Misaada la Maendeleo la Marekani (USAID), Bi. Ludovicka Tarimo, alisema taasisi yake imechangia Dola za Marekani 196,650
kwenye mradi huo ambao wanaamini kupitia
utekelezaji wake, utawasaidia mamilioni ya watoto wa kike hapa nchini kupata
mafunzo ya kujitambua na hatimaye kufanikiwa kielimu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMANNE, AGOSTI
20, 2013.
--
Irene K. Bwire
No comments:
Post a Comment