HATI ZA KUMILIKI ARDHI ZITOLEWE UPYA, ZA DIJITALI
NA ZIHUSISHWE NA NAMBA YA MLIPA KODI (TIN)
Kamati ya Hesabu za
Serikali imekutana na Wizara ya Ardhi kwa madhumuni ya kupitia Hesabu za Wizara
kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2012. Changamoto za Wizara ni nyingi sana na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amehoji mambo mengi sana
na mengi ni wizi, upotevu wa mapato ya Serikali na malalamiko ya wananchi
kuhusu ardhi. CAG alitoa hoja za ukaguzi maeneo ya mapato kutokusanywa,
kulimbikizwa na hata kukusanywa bila kuyawasilisha Wizarani.
Katika Mwaka wa Fedha
2011/12 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni tisini na tisa
(99 bilioni) lakini ilikusanya shilingi bilioni ishirini tu (20 bilioni) sawa
na asilimia 21 ya makadirio.
CAG pia alihoji
masuala ya viwanja vilivyopimwa, kugawiwa watu lakini watu hawakupewa hati
ambapo zaidi ya viwanja 7, 342 vilikutwa ni viwanja vyenye shaka. Pia viwanja
160 jijini Dar es Salaam vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 555.8 milioni viligundulika
ni viwanja ambavyo walijigawiwa maafisa wa Ardhi maana haoakuwa na ushahidi
wowote wa mauzo ya viwanja hivyo. Hoja nyingine ni pamoja na ukiukaji wa sheria
kwa kujengwa kwenye fukwe nk.
Katika Ripoti ya
Hesabu za Serikali Kuu 2011/12 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
alipendekeza kuanzishwa kwa haraka mfumo fungamanifu wa Taarifa za Ardhi,
kutunza kumbukumbu kielektroniki na kuunganisha kuanzisha utaratibu wa kwamba
wakati wa kusajili hati ya ardhi anayesajili kuwa na namba ya utambulisho wa
mlipa kodi (TIN).
Baada ya mjadala wa
kina na kushauriana na wakaguzi na wataalamu Kamati ya Hesabu za Serikali
iliona kuwa kuna haja kubwa sana ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo
mzima wa kutoa hati za kumiliki Ardhi. Hivyo Uamuzi mkubwa tuliochukua ni kuagiza kuwa hati zote za kumiliki ardhi
zitolewe upya, ziwe za dijitali na hati ziendane na namba ya Mlipa kodi
(TIN).
Kamati imeagiza
kuwa Wizara kutoa majibu ya utekelezaji
wa agizo hilo ifikapo Mwezi Januari mwaka 2014. Tunaamini kuwa iwapo hati
zote za ardhi zitakuwa za dijitali, tutaondoa kabisa tatizo la hati mbili
kwenye kiwanja au shamba moja, itakuwa ni rahisi kwa usimamizi wa ardhi na
itaondoa mgogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Pia tunadhani pia itakuwa rahisi
kujua nani anamiliki ardhi kiasi gani, wapi nk.
Tunaamini kuwa mfumo
wa dijitali katika hati za ardhi utaongeza usalama zaidi kwa wamiliki wadogo wa
ardhi na kuondokana kabisa au kwa kiasi kikubwa na hati za bandia ambazo
zinaumiza zaidi wananchi masikini wanaotapeliwa kila wakati. Ardhi yenye hati
za kidijitali na zinazotunzwa kielektroniki zitakuwa na thamani zaidi na
zitawezesha mahitaji zaidi ya hati hizo kwa shughuli mbalimbali za wananchi.
Mapato yatokanayo na
umiliki yatakusanywa kirahisi sana na kwa kuwa kila hati itakuwa na namba ya
utambulisho wa mlipa kodi (TIN) itakuwa
ni njia rahisi ya kuzuia ukwepaji kodi ya ardhi. Kwa kuwa kamati imeagiza
kuanza kutumika kwa risiti za elektroniki kwa malipo ya serikali, tutaweza
kupandisha mapato ya Serikali na hasa kwenye halmashauri za wilaya na kuepukana
na kodi sumbufu kwa wananchi.
Changamoto kubwa ni
kama matajiri wenye ardhi kubwa watakubali mageuzi haya kwani hawapendi
ijulikane kiwango cha ardhi wanachomiliki na pia itazuia ukwepaji kodi na
kupunguza rushwa kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi.
Mfumo huu hata hivyo
uwezeshe watu kuweza kutafuta kwenye mtandao hati, iwe rahisi kutafanya
utafutaji. Pia mfumo huu unaweza kusaidia sana suala la fidia kwa wananchi
wanaohamishwa kupisha uwekezaji mkubwa kama kwenye sekta za madini na gesi
asilia. Kwa mfano mwekezaji atapaswa kuhakikisha hati za kijiditali
zinapatikana kwa wananchi wanaohamishwa kupisha mradi baada ya maridhiano ya
wananchi hao kuhusu kupisha mradi na mahala watakapohamia.
Kuna haja pia hata
hati za madini (mining rights) na leseni mbalimbali ziwe za dijitali na
kuhusishwa na TIN. Huko ndipo tunapaswa kuelekea.
Zitto Kabwe
MwenyeKiti PAC
No comments:
Post a Comment