Wednesday, August 14, 2013

Rais Robert Mugabe arushia MDC vijembe



Mugabe angali kutawazwa kama mshindi wa uchaguzi mkuu kutokana na kesi ya MDC mahakamani
Rais aliyechaguliwa tena kutawala kwa muhula mwingine nchini Zimbabwe Robert Mugabe, amewaambia wapinzani wake kwenye uchaguzi uliokamilika hivi karubini kuwa ikiwa hawajapendezwa na matokeo ya uchaguzi basi 'wajinyonge'.
Mugabe aliongeza kuwa hawezi kurudi kwenye serikali ya muungano iliyoafikiwa kutokana na vurugu zilizofuata uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.
Mugabe aliyatoa matamshi yake makali kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya mashuja waliopigania uhuru wa Zimbabwe.
Morgan Tsvangirai, anayeongoza chama cha upinzani MDC, alisusia sherehe hizo ambapo Mugabe alitoa hotuba yake ya kwanza tangu kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 31 mwezi Julai.
MDC kimewasilisha malalamiko yake mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu hali ambayo imesababisha kucheleweshwa kuapishwa kwa Mugabe. Alishinda uchaguzi huo kwa asilimia sitini ya kuza zote. Hata hivyo majaji wengi wanasemekana kumuunga mkono Mugabe kwa hivyo huenda kesi ya MDC ikatupiliwa mbali.
Chama cha Mugabe Zanu-PF kilishinda wingi wa viti vya bunge kikipata zaidi ya thuluthi mbili ikiwa ni viti 160 ya viti kati ya 210 vya bunge zima.
Sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa Zimbabwe, ni sherehe za kujivunia kwa wazimbabwe wakati ambapo nchi hiyo ilijipatia uhuru wake miaka ya sabini.
Hii leo Mugabe ameitoa hotuba yake ya kwanza katika eneo la kumbukumbu la vita hivyo na ambako baadhi ya wapigania uhuru wamezikwa.
Hotuba za Mugabe zinasifika zaidi kwa siasa zake kali za kizalendo, na ambazo zaidi hulenga mkoloni wake wa zamani Uingereza na pia anatarajiwa kujipiga kifua kufuatia ushindi wake mkubwa katika uchaguzi mkuu uliopita mwezi jana.
Chama cha MDC kinasusia sherehe hizo katika kile kinachosema ilikuwa wizi mkubwa wa kura uliofanywa na chama cha Zanu-PF, kwa hivyo sherehe hii bila shaka itazongwa na siasa.
Mugabe bado hajaapishwa kwa muhula wake wa saba akitawala Zimbabwe, kwa sababu ya kesi ya MDC mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
MDC kilisema kina ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa wizi wa kura ulitokea na kwamba kulikuwa na visa vingine vilivyohujumu matokeo ya uchaguzi huo ikiwemo, rushwa , dhuluma na kuvurugwa kwa daftari la wapiga kura.

No comments:

Post a Comment