Kamati ya Kudumu ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano Tanzania ya Miundombinu
ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Peter Joseph Serukamba (Mbunge Kigoma
Mjini) ilifanya ziara ya kukagua miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege
mkoani Kagera jana Agosti 14, 2013.
Kamati hiyo mara baada ya
kuwasili mkoani Kagera na kupokelewa na
Mkuu wa Mkoa wa Kagera ofisini kwake majira ya saa 5:00 asubuhi ilianza ziara yake mkoani hapa kwa kutembelea
bandari za Bukoba na Kemondo kujionea miundombinu ya bandari hizo.
Katika bandari ya Bukoba baada ya
kutembelewa na kukaguliwa Kamati iliuagiza
uongozi wa bandari kufanya ukarabati wa haraka katika sehemu ya abiria
kwa kufumua paa ambao limezeeka na kullipandisha juu zaidi ili kuruhusu hewa
zaidi katika eneo hilo na kweka paa jipya lisilovuja.
Pia katika Bandari ya Kemondo
Mwenyekiti wa kamati Mhe. Serukamba baada ya kusomewa taarifa alimwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mara moja nyumba za
watumishi zilizoko katika eneo la bandari ya Kemondo zilizochukuliwa na Shirika la nyumba la Taifa zinarejeshwa
kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni bandari ya Kemondo.
Katika hatua nyingine wajumbe wa
Kamati walitembelea Wilayani Missenyi na kukagua eneo la Omukajunguti ambapo
serikali inatarajia kujenga uwanja wa kimataifa wa ndege. Katika eneo hilo
Kamati ilitoa maelekezo kwa taasisi inayohusika, Wizara na Halmashauri
kukamilisha maandalizi ya kiwanja hicho.
Kamati iliagiza Wizara ya
Uchukuzi kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TIAA) pamoja na
Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kukaa pamoja na kuweka mipaka halisi ya
kiwanja cha Omukajunguti pia kufanya tathimini na kuwalipa wananchi fidia zao ili
kupisha ujenzi wa uwanja huo.
Aidha katika Uwanja wa Ndege wa
Bukoba wajumbe wa Kamati waliridhika na maendeleo ya ujenzi na kumsisitiza
Mkandarasi kuhakikisha anamaliza kazi zake kwa muda aliopewa kufikia Februari
2014. Aidha Wizara kuhakikisha inawalipa fidia wananchi ambao bado hawajalipwa
fidia zao kiasi cha milioni 900 katika mwaka huu wa fedha 2013/2014.
Gari la Wabunge Lapata Ajali
Wakati msafara wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ukielekea Wilayani Missenyi kukagua sehemu
utakapojengwa uwanja wa Kimataifa wa
Ndege wa Omukajunguti, gari aina ya Costa lenye namba za usajili T 570 BYU
lilowabeba Waheshimiwa Wabunge 11 lilipata hitirafu na kutaka kuungua.
Ajali hiyo ilitokea eneo la
Mwanzo Mgumu kilometa moja kutoka mpakani mwa Wilaya ya Bukoba na Wilaya ya
Missenyi ambapo gari hilo aina ya costa lilianza kutoa moshi mwingi kwa upande
wa nyuma wakati likiwa kwenye mwendo mkali na kuleta hofu kubwa kwa abiria
walikuwemo ndani ya gari hilo.
Mara baada ya dereva wa costa kugundua
kuwa gari linataka kuungua alifanikiwa kulisimamisha gari hilo na kuwaambia
abiria wake kuwa gari linaungua na alitoka haraka ndani ya gari na kutimua mbio
na kuwaacha wabunge wakiangaika kutoka wakati gari likitoa moshi mwingi sana.
Kwa mujibu wa wabunge walikuwemo
kwenye gari hilo walisimulia kuwa baada ya kuambiwa kuwa gari linaungua kila
mmoja alifanya juhudi za kujiokoa yeye mwenyewe ambapo mmoja wao alipita dirishani
na wengine walifanikiwa kusukuma mlango na
ukafunguka na kutoka salama.
Kwa Bahati hakuna Mbunge
aliyeumia isipokuwa Mhe. Batenga aliumia
mkono kidogo baada ya kubanana sana mlangoni. Baada ya kila mmoja kutoka gari
hilo liliendelea kutoa moshi mzito sana lakini kwa halikushika moto na baadae lilizika na kuacha
kutoa moshi.
Wabunge waliokuwemo katika gari
hilo ni Rebbecca Mngondo (Arusha Viti Maalumu), Rita Kabati (Iringa Viti
Maalumu), Mariam Msabaha (Zanzibar Viti Maalumu), Mhe. Batenga (Kagera Viti
Maalumu), Mhe. Madabida (Dar es Salaam Viti Maalum), Clara Mwatuka (Mtwara Viti Maalumu).
Wengine ni Mzee Hussein
(Zanzibar), Mussa Haji Kombo (Pemba Zanzibar), Abdul Mteketa (Jimbo la
Kilombelo), Mutula Mutula (Jimbo la Tunduru Kusini). Aidha Mwenyekiti wa Kamati
Mhe. Peter Serukamba Hakuwemo katika gari hilo lilotaka kuungua.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2013
No comments:
Post a Comment