Tuesday, August 06, 2013

HALMASHAURI YA WILAYA YA KARAGWE YAVUNJWA KYERWA YAANZA RASMI


·   Uchaguzi wa Wenyeviti Wafanyika Kuwapata Wenyeviti Wapya
·   Mwenyekiti na Makamu Wake Wachukua Halmashauri Zote Mbili
Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa yaanza rasmi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na kuundwa Halmashauri mbili Karagwe na Kyerwa Julai 31, 2013.
Hatua hiyo ilitanguliwa na uzinduzi rasmi wa wilaya 19 mpya  nchini ikiwemo Kyerwa uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete  katika wilaya mpya ya Kyerwa wakati wa ziara yake ya kazi mkoani Kagera Julai 27, 2013.
Kabla ya kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mhe.  Massawe Aliwashukuru madiwani kwa kuendesha mchakato wa kuunda halmashauri mpya ya Kyerwa kwa amani na utulivu na kusikilizana  ikiwemo kugawana mali na rasilimali za Wilaya mama ya Karagwe bila malumbano.
Mhe. Massawe alisema kuundwa Halmashauri mpya ni lengo la serikali kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi ili kurahisha utoaji wa huduma hizo ambapo alisema mwaka 2005 Wilaya ya Karagwe ilikuwa na shule 194 lakini kufikia mwaka 2013 zimejengwa shule na kufika 205.
Vile vile mwaka 2005 maji yalikuwa yanapatikana Wilayani Karagwe kwa ujazo wa lita 125 lakini kufikia  mwaka 2013 zinapatikana lita za ujazo 254 na kuwahudumia wateja 445. Aidha, mwaka  2005 vilikuwepo Vyama vya Msingi 53 na SACCOS 14, kufikia mwaka 2013 Vyama vya Msingi 79 na SACCOS 79.
Mkuu wa Mkoa alisema hizo ni juhudi za serikali katika kuhakikisha huduma  kwa wananchi zinaboreshwa na ndiyo maana serikali iliridhia kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Kyerwa. Baada ya ufafanuzi huo Mkuu wa Mkoa alitamka rasmi kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Aidha, baada ya kuivunja Halmashauri ya Wilaya Karagwe alimkabidhi hati ya kuanzishwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. George Mkindo ambapo ilipelekea kufanyika uchaguzi wa wenyeviti wa Halmashauri zote mbili siku ya pili yake.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bw. Singsbert Kashuju alichaguliwa kuwa Mwenyekiti  mpya wa Halmashauri ya Wilaya Mpya ya  Kyerwa na aliyekuwa makamu wake Bw. Wales Mashanda alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Hoja za Ukaguzi Katika Halmashauri za Wilaya.
Katika hatua nyingine Mhe. Massawe alihudhuria vikao maalum katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kagera na kujadili taarifa za hoja za ukaguzi za Mkuaguzi na Mdhibiti Mkuu wa fedha ya serikali ili kuhakikisha hoja hizo zinafungwa na fedha ya serikali inatumika kama ilivyokusudiwa.
Katika majadiliano hayo kwenye vikao maalum Mhe. Massawe alisistiza Mabaraza hayo ya Madiwani kuzisimamia Halamashauri hasa watendaji kujibu hoja kwa wakati, Kupunguza utegemezi wa Serikali Kuu na kubuni vyanzo  vipya vya mapato katika Halmashauri zao.
Pia kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati, Madiwani kutohusika katika wizi wa fedha za Halmashauri za Wilaya na kutangaza maslahi binafsi pale wanapohusika katika kupata tenda za miradi ya Halmashauri zao.
Aidha Mhe. Massawe alitoa siku saba kwa kila Halmashauri ya Wilaya Mkurugenzi kuhakikisha watumishi wote waliochukua masurufu bila kurejesha warejeshe ndani ya siku saba baada ya vikao kwa kila halmashauri na  wasiporejesha wakatwe kwenye mishahara yao na apewe taarifa.
Ufuatao ni ukaguzi wa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2007/2008 mpaka 2011/2012 na Halmashauri za wilaya za Mkoa wa Kagera zilipata hati zifuatazo: Missenyi hati safi miaka 5, Biharamulo Hati safi miaka 5, Bukoba hati safi  4 na hati ya mashaka 1.
Bukoba Manispaa hati safi 4 na hati ya mashaka 1, Muleba hati safi 4 hati ya mashaka 1, Karagwe hati safi 3 hati za mashaka 2, Ngara hati safi 3 hati za mashaka 2. Mkuu wa mkoa kujadili hoza za ukaguzi  katika Halmashauri za Wilaya ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muunganoa wa Tanzania la April 29 2009.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2013




Wananchi na Madiwani Waliokuwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Wakishuhudia Kuvunjwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na Kuundwa Halmashauri mbili.
 Mhe. Massawe Akimkabidhi Rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Bw. George Mkindo Hati ya Kuanzishwa Rasmi Halmashauri Hiyo Wilayani Karagwe.

No comments:

Post a Comment