Jumanne
tarehe 20 Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari
zinazohusu matamshi ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika
kuhusu sakata ya mabilioni ya Uswisi. Waziri amesema kwamba Serikali ya
Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze
kusaidia uchunguzi. Habari kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo
iliandikwa na Gazeti la The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba
2012.
Nimeona
ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka
rekodi sawa juu ya Azimio la Bunge na kwamba Serikali inapaswa
kutekeleza Azimio na sio kutoa kauli tata za kukata tamaa.
Moja,
Suala hili japo sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala
la Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali wakati akichangia hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia
wakati akileta maombi yake ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na
Bunge. Kama sio sababu mpya ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni
wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio la
Bunge. Watanzania wasikubali propaganda hii ya Serikali. Bunge limeagiza
Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi
binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala
haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu kuficha nini? Kwa nini baada ya
wiki iliyopita Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara
jijini Dar es Salaam na namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje
(international transfers), leo Serikali inakuja na kauli za kukakata
tamaa? Kunani?
Pili,
Watanzania wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa
fedha hizi za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa
kodi kwenye nchi zao na kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku moja
haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama
hili. Ndio maana Azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi ambao
hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya Swiss. Nawakumbusha kwamba mwaka
1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph
Kabila kule Kongo - Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za
Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu! Waswiss walitaka Kabila
awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani
Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha. Zaire ilikadiriwa
kuwa na zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya
nje ya nchi hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo
kila nchi inapewa. Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao
walijibiwa hivi hivi. Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua
taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi.
Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila
Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau
historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe
Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa
kuimba. Sasa Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss
badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa
Bungeni. Naitaka Serikali ianze uchunguzi mara moja kama namna
ilivyoelekezwa na Bunge. Suala hili sio suala la kisiasa, sasa ni Azimio
la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala hili sio suala
la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni suala la Wananchi. Wananchi
hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya kutekeleza Azimio lao.
Kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya
Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa
fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliopelekea
Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya Tanzania. Hatutakaa
kimya mpaka tuone mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio
la Bunge itakuwa ni salamu tosha mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu
kwamba hawana pa kujificha na Tanzania sio Taifa la kuchezeachezea.
Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda atupishe
mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta. Watanzania sio mabwege tena,
Mwakyembe alipata kusema.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment