Halmashauri ya Wilaya ya Muleba
imepewa miezi mitatu kujisafisha yenyewe
na kuwachukulia hatua watendaji wote waliohusika na ufujaji wa fedha za serikali, kutozingatia
kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao
kwa wananchi wa Wilaya ya Muleba.
Muda wa miezi mitatu ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe.
Kanali Mstaafu Fabian I. Masswe alipokuwa mgeni rasmi katika kikao cha balaza
la Madiwani (Full Council) kilichofanyika siku ya Ijumaa tarehe 2/11/2012
wakati alipowasilisha ripoti maalum.
Mhe. Massawe alitoa muda huo
baada ya kuwasilisha ripoti ya ukaguzi maalumu mbele ya Madiwani uliofanyika
mwezi Agosti mpaka Septemba 2011 kwenye halmashauri hiyo ambapo ukaguzi huo
uliombwa na Madiwani wenyewe kuwa ufanyike baada ya kutordhika na mwenendo wa
Halmashauri yao.
Ripoti ya ukaguzi maalum
uliofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hazina
pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera ilibainisha kuwa vitabu 133 vya
kukusanyia ushuru havijulikani vilipo,
Halimashauri haijui vitabu hivyo viko wapi.
Pia ripoti hiyo ilibainisha kuwa
baadhi ya watendaji wa kata na vijiji kuwa na vitabu mara mbili ambavyo
wanavitumia kukusanyia ushuru wa halmashauri jambo ambalo linaikosesha
halmashauri hiyo kutopata mapato kutokana
na watendaji hao kutowasilisha kabisa au kuwasilisha mapato kidogo kwenye Halmashauri tofauti na
wanavyokusanya.
Vile vile ripoti maalum ya
ukaguzi ilibainisha sehemu kubwa ya malipo kufanyika bila kufuata utaratibu wa
kulipa fedha za serikali ambapo nyaraka za ulipaji hazikuonekana, pia mlipwaji
hajulikani ni nani na fedha zilizolipwa zililipwa bila kuidhishwa na serikali.
Aidha ripoti hiyo pia ilibaini
udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, usimamizi wa miradi ya
maendeleo, Halmashauri kufanya manunuzi makubwa kwa kutumia masurufu, Usimamizi
mbovu wa mali za Halmashauri na upotevu wa mali za Halmashauri katika ngazi za
vijiji.
Mkuu wa Mkoa aliiagiza Halmashauri
pamoja na Madiwani wake kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua za kinidhamu
ndani ya miezi mitatu na taarifa kuwasilishwa kwake.Baadhi ya Maafisa
wanaohusishwa na tuhuma hizo ni pamoja na Mhandisi wa ujenzi na Mratibu wa
TASAF.
Wilaya ya Muleba imekuwa katika
malumbano ya kisiasa ya muda mrefu jambo
ambalo linairudirudisha nyuma kimaendeleo huku miradi ya maendeleo ikishindwa
kuteketelezeka kwa wakati kutokana na malumbano hayo jambo alilokiri mbele ya kikao hicho mwenyekiti wa
Halmashauri Bw. George Katomelo wakati wa kufungua kikao hicho cha balaza la
Madiwani.
No comments:
Post a Comment