Baadhi ya wanafunzi wakiandamana.
Wanafunzi wa kidato cha sita na cha tano wakiwa nje ya jengo la manispaa ya Bukoba.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bi Ziporah Lion Pangani akiongea na wanafunzi shule ya sekondari ya Ihungo waliofanya maandamano.
Wanafunzi wakisikiliza kwa makini.
WANAFUNZI wa kidato cha tano na sita wa shule ya sekondari Ihungo ambayo
ni miongoni mwa shule kongwe hapa nchini iliyoko katika manispaa ya
Bukoba wameandamana hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bukoba
kupinga vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya walimu wao.
Wanafunzi hao waliandamana jana hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya
ya Bukoba Ziporah Pangani na kutoa malalamiko mbele yake kwa kile
walichodai kuwa wanafanyiwa hujuma na mwalimu anayewafundisha somo la
kemia waliyemtaja kwa jina la Philemon Tumwesige.
Kwa nyakati tofauti bila kutaja majina yao wakimlalamikia mwalimu
Tumwesige walisema kuwa amekuwa ha tabia ya kutoingia darasani
kuwafundisha somo hilo la kemia, walisema kuwa tangu mwaka huu wa sasa
wa masomo uanze ameingia darasani mara 13 wakati katika kipindi hicho
alitakiwa kuwa ameingia darasani mara 56.
Waliendelea kumlalamikia kwa kumueleza mkuu wa wilaya kuwa amekuwa
na tabia ya kuwachangisha fedha ili aweze kuwafundisha, walisema mwalimu
Tumwesige alikuwa akimtaka kila mwanafunzi amchangie shilingi 5,000 ili
aweze kuingia darasani.
Walisema idadi kubwa wanafunzi walimchangia kiasi hicho, walimweleza
mkuu huyo wa wilaya kuwa pamoja na kumchangia kiasi hicho cha fedha
amekuwa akigoma kuwafundisha na mara kwa mara alikuwa akisema kuwa
anafanya hivyo ili wanafunzi wa shule hiyo wasifaulu somo la kemia.
Wanafunzi hao walisema kinachodhihirisha mkakati wake wa kutaka
wanafunzi wasifaulu mtihani wao wa kemia ni matokea ya mtihani wa
majaribio wa somo la kemia uliofanywa na wanafunzi wa kidato cha sita
katika shule hiyo, walisema kati ya wanafunzi zaidi ya 400 wa kidato cha
sita waliofanya somo hilo la kemia waliofaulu ni 17 tu.
Walimuomba mkuu wa wilaya afanye utaratibu ili wapatiwe mwalimu
mwingine wa kemia, walisema kamwe mwalimu huyo awezi kuwapa elimu sahihi
kwa kuwa wameishavutana naye sana, walisema kila siku wamekuwa
wakimtolea taarifa kwa uongozi wa juu wa shule hiyo lakini hatua
zimekuwa hazichukuliwi dhidi yake.
Mkuu wa wilaya Bi. Pangani aliwaahidi kushughulikia suala hilo
haraka iwezekanavyo ili lipatiwe ufumbuzi, aliwaambia warudi shuleni
watulie ili ofisi ya elimu iweze kushughulikia suala hilo, "Nendeni
shuleni mtulie najua mnadai haki yetu na haki yenu itapatikana.
Alimaliza.
No comments:
Post a Comment