Michoro
ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila iliyo kijijini Kwembe katikati ya
Wilaya za Kisarawe Mkoa wa Pwani na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii ni
sehemu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
(MUHAS) inayojengwa kwenye eneo la ekari 3800
kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya
wapatao 15,000 kwa mwaka, na pia itakua sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi
yote makuu na ya kawaida nchini.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, ujenzi wa Hospitali hii, ambayo pesa ya ujenzi wake imeshapatikana, unatarajiwa kuanza
mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada
ya ujenzi kuanza. Kwa maneno mengine Kampasi ya Muhimbili ya Mloganzila
inategemewa kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka 2015.
Tayari
wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi ya
Mloganzila wameshaanza mafunzo ndani na nje ya nchi. Mara hospitali hiyo kubwa
na ya kisasa itakapokamilika itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa mia
sita (600).
Sambamba na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila
pia ujenzi wa Kampasi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeshaanza na kufikia hatua ya juu na ambapo pia hospitali
hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mfuko wa
Afya ya Jamii (National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel
Humba mchakato wa kufanikisha uanzishaji wa Chuo Hospitali hiyo
vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo Madaktari na watumishi wengine
wako nchini na nje ya nchi kwa ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.
Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya
kisasa vya tiba vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango
cha Kimataifa, ikiwa ni mikakati kabambe ya serikali ya awamu ya nne
katika kuhakikisha nchi ina wataalamu wengi na huduma za kisasa za afya ili
kuondokana na adha ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Kwa sasa MUHAS inachukua takriban wanafunzi
2442 wa udaktari na huduma za afya kwa mwaka. Hivyo ujio wa kampasi ya Afya
Mloganzila na Kampasi ya afya ya UDOM utaharakisha mpango wa serikali wa
kupunguza wastani wa wagonjwa kwa daktari mmoja kwa kiwango
kikubwa. Hivi sasa wastani ni daktari
mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
No comments:
Post a Comment