Wednesday, December 25, 2013

MKUU WA MKOA WA KAGERA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO NA KUHIMIZA UKAMILISHWAJI WA MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA SASA


Na Sylvester Raphael


Mkoa wa Kagera umeanza kutekeleza mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa ili kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka katika sekta za Kilimo, Maji, Elimu, Uchukuzi, Nishati na Madini, na Uwezeshaji wa wananchi kupitia mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe katika kuhakikisha mkoa wake unatekeleza mkakati huo wa Matokeo Makubwa Sasa amefanya ziara ya mkoa mzima ili kuhimiza, kukagua na kupokea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa.
Elimu, katika sekta ya elimu Mhe. Massawe alikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara za masomo ya sayansi  kila shule, aidha kupokea vyumba ambavyo tayari vimekamilika kwa kila wilaya  na kuhimiza  ujenzi wa nyumba za walimu na kukamilisha vyumba vya maabara.
Maji, katika mkakati wa Matokeo Makubwa sasa serikali imejipanga kuhakikisha inatekeleza miradi ya maji kwa vijiji kumi ambapo Mkuu wa Mkoa alikagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo ya maji kwa wananchi na kujionea miradi ambayo tayari imekamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
Kilimo, mkoa wa Kagera umejipanga kutokomeza ugonjwa wa mnyauko ambapo Mkuu wa Mkoa ametangaza operesheni tokomeza Mnyauko katika mkoa wa Kagera kuanzia Januari 2014 .Zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa mkoa wa Kagera wanategemea zao la ndizi kama zao kuu la chakula na biashara.
Nishati na Madini, serikali  kwasasa inatekeleza mkakati wa kupeleka umeme vijijini ili wananchi waishio vijijini waweze kupata umeme. Miradi mingi kwa hivi sasa inaendelea kutekelezwa ya kupeleka umeme vijijini.
Katika Wilaya ya Misenyi  mradi wa umeme unaotekelezwa hivi sasa ni wa kutoa umeme Bunazi Makao Makuu ya Wilaya kuelekea Mtukula mpakani mwa Tanzania na nchi ya Uganda ambapo vijiji vyote ambavyo vipo katika eneo hilo vitapatiwa umeme kufikia  Desemba 31, 2013.
Wahamiaji Haramu, Mkuu wa mkoa wa Kagera kupitia kaulimbiu ya “Hakuna wa Kubaki na Hakuna wa Kurudi” katika ziara yake ya mwisho wa mwaka 2013 amekuwa akiwahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kamati za ulinzi na usalama za Wilaya ili kuhakikisha wahamiaji haramu wote wanarudi kwao na hakuna kurudi.
Pia Mhe. Massawe katika ziara yake alifanya mikutano ya hadhara  na wananchi na kuwakumbusha kuendelea kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI ambao sasa unaonekana unaendelea kupanda tena katika mkoa wa Kagera kutoka asilimia 3.4 hadi 3.7 Pia Mkuu wa Mkoa aliwaeleza wananchi jinsi serikali inavyotekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa.

No comments:

Post a Comment