Monday, December 30, 2013

MATUKIO YA TAMASHA LA IMANI NA AMANI

Baadhi ya waandishi wa habari katika mkoa wa Kagera walioudhuria tamasha la Amani na Imani lililoandaliwa na kikundi cha wasanii cha Nazareth Singer of Faith organization, lilifanyika katika ukumbi wa klabu ya usiku ya Linas.
 Baadhi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini walioudhuria tamasha hilo.
 Baadhi ya viongozi wa serikali walioudhuria tamasha hilo toka kushoto ni meneja wa benki ya CRDB tawi la Bukoba, Karlo Sendwa, Januari Makamba naibu waziri mawasiliano, sayansi na teknologia, mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe na afisa tarafa ya Rwamishenye.

 W.asanii wa kikundi cha Kaswida toka Maruku walikuwa ni miongoni mwa vikundi vya nyimbo za dini vilivyoshirikia katika tamasha hilo.
 Kikundi cha Kaswida.

 Kundi la Nazareth Singers lililoandaa tamasha linaloongozwa na msanii maarufu John Mgango  likitumbuiza.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera, kanali mstaafu Fabian Massawe akonyesha umahili wake.

Msanii wa nyimbo za Injili, Christina Shusho.

Friday, December 27, 2013

MATUKIO YA UBATIZO WA REVELIAN NA PATRIC

 Ernestina Mwesiga, akiwa na wajukuu zake, kulia ni Ivan Kalumuna na Kushoto ni Irene Ayesiga.
 Watoto waliobatizwa aliyevaa t shirt nyekundu Revelian Edius na aliyevaa shati la mikono mifupi ni Muumuliza, kulia ni Margareth Abella.
 Wasimamizi wa ubatizo kushoto, na kulia ni Edwin Mwesiga, kaka yao wazazi wa waliobatizwa, ubatizo ulifanyika katika kanisa la kirutheri la Katare na hafla ya kuwapongeza vijana ilifanyika Rushasha.
 Baadhi ya walioudhuria hafla fupi.
 Wazazi wa watoto waliobatizwa, kutoka kulia ni Bw. Kato na anayefuata ni mke wake, kutoka kushoto ni mwenza wake Edius Njunwa wa pili toka kwake.


Thursday, December 26, 2013

WAZIRI MKUU PINDA AKIWA KATAVI

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda akisalimiana na watoto  baada ya ibada ya Krismasi iliyofanyika  kijijini kwa Waziri Mkuu, Kibaoni wilayani Mlele, Katavi Desemba 25,2013. (Pichana Ofisi ya Waziri  Mkuu)
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na wazee baada ya ibada ya  Krismasi iliyofanyika kijijini kwake, Kibaoni wilayani  Mlele, Katavi, Desemba 25, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri  Mkuu)

MAMBO YA SIKUKUU YA KRISMAS

 Watoto wa wakurugenzi wa mtandao huu wa kijamii, kutoka kushoto ni Ayesiga Rugalabamu na kulia ni Ivan Rugalabamu.
 Mambo ya ufukwe wa hoteli ya Spice iliyoko katika manispaa ya Bukoba.


 Mmoja wa wakurugenzi wa mtandao huu, Margreth Abella, akiwa na wadau.
Wadau wakuu wa mtandao huu.

Wednesday, December 25, 2013

MKUU WA MKOA WA KAGERA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO NA KUHIMIZA UKAMILISHWAJI WA MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA SASA


Na Sylvester Raphael


Mkoa wa Kagera umeanza kutekeleza mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa ili kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka katika sekta za Kilimo, Maji, Elimu, Uchukuzi, Nishati na Madini, na Uwezeshaji wa wananchi kupitia mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe katika kuhakikisha mkoa wake unatekeleza mkakati huo wa Matokeo Makubwa Sasa amefanya ziara ya mkoa mzima ili kuhimiza, kukagua na kupokea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa.
Elimu, katika sekta ya elimu Mhe. Massawe alikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara za masomo ya sayansi  kila shule, aidha kupokea vyumba ambavyo tayari vimekamilika kwa kila wilaya  na kuhimiza  ujenzi wa nyumba za walimu na kukamilisha vyumba vya maabara.
Maji, katika mkakati wa Matokeo Makubwa sasa serikali imejipanga kuhakikisha inatekeleza miradi ya maji kwa vijiji kumi ambapo Mkuu wa Mkoa alikagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo ya maji kwa wananchi na kujionea miradi ambayo tayari imekamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
Kilimo, mkoa wa Kagera umejipanga kutokomeza ugonjwa wa mnyauko ambapo Mkuu wa Mkoa ametangaza operesheni tokomeza Mnyauko katika mkoa wa Kagera kuanzia Januari 2014 .Zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa mkoa wa Kagera wanategemea zao la ndizi kama zao kuu la chakula na biashara.
Nishati na Madini, serikali  kwasasa inatekeleza mkakati wa kupeleka umeme vijijini ili wananchi waishio vijijini waweze kupata umeme. Miradi mingi kwa hivi sasa inaendelea kutekelezwa ya kupeleka umeme vijijini.
Katika Wilaya ya Misenyi  mradi wa umeme unaotekelezwa hivi sasa ni wa kutoa umeme Bunazi Makao Makuu ya Wilaya kuelekea Mtukula mpakani mwa Tanzania na nchi ya Uganda ambapo vijiji vyote ambavyo vipo katika eneo hilo vitapatiwa umeme kufikia  Desemba 31, 2013.
Wahamiaji Haramu, Mkuu wa mkoa wa Kagera kupitia kaulimbiu ya “Hakuna wa Kubaki na Hakuna wa Kurudi” katika ziara yake ya mwisho wa mwaka 2013 amekuwa akiwahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kamati za ulinzi na usalama za Wilaya ili kuhakikisha wahamiaji haramu wote wanarudi kwao na hakuna kurudi.
Pia Mhe. Massawe katika ziara yake alifanya mikutano ya hadhara  na wananchi na kuwakumbusha kuendelea kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI ambao sasa unaonekana unaendelea kupanda tena katika mkoa wa Kagera kutoka asilimia 3.4 hadi 3.7 Pia Mkuu wa Mkoa aliwaeleza wananchi jinsi serikali inavyotekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa.

WACHINA WAMTEMBELEA PINDA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  na balozi wa  China nchini, Dr, Lu  Youqing  (kulia) wakizunguma na Bibi  Estephanoia Chifunta wakati alipomtembelea nyumbani  kwake katika kijiji cha Kibaoni wilayani Mlele, Katavivi Deemba 23, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Sunday, December 22, 2013

KAPOTIVE STAR SINGER YAZINDUA ALBAMU YA ZAWADI YA KRISMAS

Baba askofu msaidizi wa jimbo la Bukoba Methodius Kilaini akimpokea mstahiki Meya wa manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa albamu ya zawadi ya kristimas  ya kundi la wasanii wa nyimbo za injili la Kapotive star Singer uliofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Linas.
Baadhi ya wageni meza kuu, toka kushoto Philbert Nyerere, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya uzinduzi wa albamu, Meya Anatory Amani, Askofu Methodius Kilaini na Padre Alcheleus.
Wasanii wa kikundi cha Kapotive star Singer.
Kulia ni mshereheshaji maarufu mkoani Kagera Bw. Lutakwa, anayefuata ni mratibu wa kundi hilo Bw. Kagya.
Katikati ni msanii maarufu Bw. John Mgango aliyetunga wimbo wa hamasa ya maendeleo ya mkoa wa Kagera.
Wasanii wa Kapotive stra singer wakizindua albamu yao ya zawadi ya kristimas.
Kushoto  ni msanii maarufu nchini ambaye ni mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili, Upendo Nkonyi, kulia ni mmoja wa wakurugenzi  wa mtandao huu, Margareth Abella Mwesiga.

Saturday, December 21, 2013

HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013


Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji. Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu. Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.
Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia. Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu maendeleo. Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga. Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.
Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na sio Kigoma tu. Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani. Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia yetu.
Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana. Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli. Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo. Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria. Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu! Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA. 
Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule. Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. Ninasukuwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu. Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni  2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania. Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).  Nimewatajia hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!
Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake zinakuwa huru.
Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo. Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.

Friday, December 20, 2013

MAMBO HAYO

 Ankal akimkabidhi zawadi ya Krismasi na kadi Kamanda wa FFU Ughaibuni The Ngoma Africa Band ya Ujeruman, Ras Ephraim Makunja, a.k.a Field Marshal wa jamii ya Annunaki walipokutana leo katikati ya jiji la Dar es salaam na kufanya mazungumzo ya faragha ya saa moja katika kiota cha Break Point cha mjini. Katika mazungumzo yao waliongelea mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuendeleza undugu uliopo baina ya Globu ya Jamii na FFU Ughaibuni, na kupanga tarehe ambazo The Ngoma Africa Band itakuwa huru kuja kufanya maonesho kadhaa nchini Tanzania.

UZINDUZI WA ALBAMU YA KAPOTIVE SINGER


KUNDI MAHIRI LA KAPOTIVE STAR SINGERS-BUKOBA, WANAKULETEA UZINDUZI WA ALBUM YAO NZURI SANA YA “ZAWADI YA KRISSMAS” SIKU YA JUMAPILI, TAR. 22/12/13, KATIKA UKUMBI WA LINAS CLUB, KUANZIA SAA 8 MCHANA HADI 1 JIONI.

UZINDUZI HUO UTAHUDHURIWA NA WAIMBAJI WA KIMATAIFA UPENDO NKONE TOKA DAR-ES-SALAAM. PAMOJA NA KWAYA ZA MT. JOHN BOSCO-VIJANA, KWAYA YA VIJANA –ELCT - KENGELE TATU, NA KWAYA YA SDA.

KIINGILIO KITAKUWA KAMA IFUATAVYO:

-        10,000 KWA MTU MMOJA
-        50,000 KWA WATU SITA (TICKET YA FAMILIA)
-        5,000 KWA WATOTO

KARIBU SANA TUWAUNGE MKONO WAIMBAJI WETU WA KAPOTIVE STAR SINGERS, KARIBU SANA TUONANE ANA KWA ANA NA DADA UPENDO NKONE. HII SI YA KUKOSA.


Thursday, December 19, 2013

PINDA BUNGENI

 Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda akizungumza na Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa TLP, Agustine Mrema, Bungeni mjini Dodoma, Desemba 19, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akijibu maswali Bungeni mjini Dodoma Desemba 19,2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

CHADEMA KWAENDELEA KUFUKUTA MOTO

habari za kazi na poleni na majukumu, ningependa kushirikiana nanyi nduku zangu kuufikisha ujumbe huu kwa Watanzania wenzangu ili wapate kujua kila kinachoendelea na si kupotoshwa na kukubali kutumika.
mimi ninaitwa Habibu Mchange, ni mfuatiliaji na mchambuzi wa maswala ya kisiasa, Nimewahi kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kupitia CHADEMA jimbo la kibaha mjini. Ni mwanachama mtiifu wa CHADEMA niliyetangazwa kuvuliwa uanachama wa BAVICHA. naomba kuwasilisha.



UNAFIKI WA MBOWE NA VIBARAKA WAKE KWA WATANZANIA.
 
Juzi niliandika kuhusu unafiki wa MBOWE kuwahadaa Watanzania ya kwamba yeye hanunuliki, nilitoa ushuhuda wa MBOWE kupokea million 100 kutoka kwa ROSTAM AZIZ aliyekuwa mwanamkakati muhimu wa ushindi wa Urais kwa mgombea wa CCM mwaka 2005 Mheshimiwa JAKAYA KIKWETE, ambapo pesa hizo zilipokelewa mwezi oktoba 2005 na kumfikia mbowe kupitia kwa mke wake ndugu LILIAN MTEI MBOWE, na kumfikia MBOWE ambaye kipindi hicho alikuwa anagombea URAIS kupitia CHADEMA,
 
 hapa mbowe sio tu kwamba alinunuliwa, alihongwa ama kutumiwa kuwadhoofisha wapinzani waliokuwa na nguvu kipindi hicho, bali pia alidhihirisha namna gani yeye ni mpinzani mtiifu kwa CCM (alikubali kutumika) na ni MNAFIKI ALIYETUKUKA.
 
Leo tarehe 18.12.2013, Magazeti kadhaa yameripoti juu ya muendelezo wa unafiki wa MBOWE na vibaraka wake.
 
Magazeti yameandika pamoja na mambo mengine, kwa ufupi kabisa hivi ifuatavyo.
 
·         Amemshinikiza mbunge wa viti maalum ndugu JOYCE MUKYA kukatisha ziara ya kikazi za kibunge  alipopangiwa na kumlazimisha wakakutane nyumbani kwake DUBAI, inawezekana ni kwenda kumlea motto wao FREELADY MBOWE, ama vinginevyo, lakini huu ni uthibitisho wa UNAFIKI wa MBOWE mbele ya WATANZANIA, kushiriki kutumia kodi za watanzania kwa matumizi binafsi tena ya KIMAPENZI na mwanamke aliyemteua kuwa mbunge bila ya kuwa na uwezo wa kukidhi vigezo vya uteuzi wa UBUNGE ndani ya chama. Kwa sasa JOYCE MUKYA ni mbunge, Hawara na mama wa motto mmoja aitwaye FREELADY MBOWE, Aliyejifungulia NEW YORK NCHINI MAREKANI kwa kutumia kodi za Watanzania.
 
·         MFUASI WAKE ASIYEJIELEWA – JOSHUA NASSARY, wiki chache zilizopita mbunge huyu wa UPEPO WA CHAMA alishiriki kumtuhumu ndugu Zitto Kabwe Kuwa anasafiri nchi nyingi ili apate posho za safari, afadhali aliyemtuhumu kuwa anasafiri, lakini yeye ameumbuliwa kuwa AMESHIRIKI KUCHUKUA pesa za UMMA WA WATANZANIA, kisha kutokwenda kushiriki ziara ya kimafunzo kwa maslahi ya nchi. Million 8 alizopewa nassary si pesa nyingi kusema anaweza kutia hasara sana, lakini ni pesa zinazoweka rehani ule upambanaji anaojitambulisha nao mbele ya jamii, ni pesa zinazoweka hatiani uwajibikaji anaojitamba nao, ni pesa zinazomdhihirisha kwamba yeye ni mwizi wa mali ya umma kama walivyo wezi wengine.
 
UNAFIKI WA AWALI WA MBOWE NA WAFUASI WAKE.
 
·         Walijitangaza hadharani kuwa Hawapokei na wanapinga posho, LAKINI MPAKA SASA WANARAMBA POSHO KAMA KAWAIDA, na pindi inapotokea imecheleweshwa kulipwa wanasimama kidete kuidai, mwanachadema pekee asiyepokea posho ni ZITTO KABWE.
 
·         MBOWE, kwa mbwe mbwe kubwa alilirudisha gari la kiongozi wa upinzani, kwa nderemo, vigeregere, matarumbeta waandishi wa habari na vifijo, kuwa kutumia gari la KUB ni kuwakosea Watanzania, kuwadharirisha na kuzitumia vibaya rasilimali za Taifa letu, hapa mbowe akajidai  ni mzalendo, tuliokuwa tunamfahamu tulicheka tukamuacha kama ataweza kuhimili alichokisema.
 
 
 
·         MBOWE, kwa aibu kubwa, akajirudishia gari la KIONGOZI WA UPINZANI, hapa akatafuna matapishi yake mwenyewe, ila safari hii alifanya kimya kimya.
   
·         Kwa masikitiko makubwa hivi sasa mbowe anashirikiana na watuhumiwa wengine wanaomiliki mali nyingi nje ya nchi ikiwemo uswiz na kwengineko.
 
·         Mbowe anamiliki NYUMBA TATU, Pesa na mali nyinginezo nje ya nchi, anamiliki NYUMBA – AFRIKA YA KUSINI , DUBAI NA MAREKANI. Ameshaitwa kuhojiwa namna alivyoweza kuzipata NYUMBA HIZO ama kama kuna biashara anafanya zaidi ya UMILIKI WA DANGURO LA BILLCANAS.
 
·         Mbowe anawatetea watoto wa kimasikini wa Kitanzania, ili hali watoto wake wote sio Watanzania kwa Kuzaliwa, Mpaka sasa anajitamba kwenye vikao vya chama kuwa motto wake mmoja amezaliwa NEW YORK (Huyu ni mmarekani wa kuzaliwa), Mtoto wake Mwingine amezaliwa LONDONI huyu ni Muingereza kwa kuzaliwa , na motto wake wa sasa hivi aliyemzaa na JOYCE MUKYA amezaliwa NEW YORK (Huyu naye pia ni mmarekani wa kuzaliwa). Uzalendo wa MBOWE uko wapi mpaka sasa?.
 
UNAFIKI ZAIDI
Naomba nishirikiane nanyi kujiuliza maswali machache, UKO WAPI UZALENDO WA MBOWE?,
Kuna Tofauti gani kati ya mali za Mbowe nje ya Nchi na Vijisenti vya Andrew Chenge?. Mbona hawa wote ni wamiliki wa mabilioni nje ya nchi?.
 
Uzalendo wa Mbowe unatokana na nini kwa Watanzania, kwanini Watanzania Tumpende Mbowe ambaye hatupendi?, hapendi shule zetu, Hapendi Hospitali zetu, hapendi ardhi yetu ndio maana anamiliki majumba nchi za nje.
 
Kwanini tusiamini mbowe anashiriki kutuchafua kama Taifa hasa vijana akijua kabisa watoto wake yeye sio Watanzania. Ina maana mbowe hapendi watoto zake waje kuwa viongozi wa Taifa hili kama ilivyo kwake?, kama la, kwanini amewanyang’anya haki ya wao kuwa watanzania wa kuzaliwa?.
 
Nimeamua kujitoa Muhanga kuwaelewesha masikini wenzangu, walalahoi wenzangu na wanyonge wenzangu, Mbowe sio mtetezi wetu, mbowe ni mfanyabiashara ambaye mtaji wake ni umasikini wetu, anatutumia sisi masikini na walalahoi kama mtaji wake wa kisiasa, anatutumia bila ya sisi kujijua, mbowe ni Tapeli wa kisiasa.
 
HISTORIA INAMPINGA
Mimi ni mkuumini wa Historia ya ukombozi, ninafahamu dunia nzima namna nchi zilizohitaji ukombozi namna zilivyopata ukombozi na namna ya viongozi wao waliowakomboa walivyojitokeza kwenye jamii.
 
Mbowe ndio mfanyabiashara pekee anayejiita mtetezi wa masikini duniani, tangu nimewahi kuifahamu historia ya ukombozi,
 
Hakujawahi kutokea Duniani labda ahera, Masikini wakatetewa na Tajiri, Haijawahi na Jaitawahi kutokea Mfanya biashara yoyote akapanga kupata hasarfa eti kwa maslahi ya Umma, wafanya biashara wote wanawaza faida, hata mbowe anawaza faida na sasa anatafuta faida kwa gharama yoyote.
 
Tunamsifia Mandela leo, Mandela hakuwa mfanyabiashara, Mandela hakuwa tajiri, Mandela alichangiwa na masikini wenzake kuikomboa Arika ya Kusini, Mandela hakuwahi Kuikopesha ANC pesa ili iwaondoe Makaburuu, Mandela alifanana na jamii aliyotaka kuikomboa na Mandela alifanikiwa kuikomboa.
 
Wote tunamsifia Nyerere Hapa Tanzania, Nyerere Hakuwa Mfanyabiashara, mwalimu Hakuwa Tajiri, mwalimu Hakuwahi kuikopesha TANU ili kumuondoa MKOLONI, nyerere alichangiwa na masikini wenzake, aliombewa na walalhoi wenzake na alilindwa na mafukara wenzake.
 
Mkifano ni mingi, hivyo hivyo kwa Samora Machel, Kwame Nkuruma, Milton Obote, Robert Mugabe, Kamuzu Banda, Dkt Martin Lutherking, Mahatma Gandh, Mao Zedong, AmilicaCabra na wengineo wote, KAMWE KUNGURU WASIOFANANA HAWAWEZI KURUKA PAMOJA.
Nitaendelea kuwafundisha mengi ninayoyajua kuhusu MBOWE NA CHADEMA kwa kadri itakavyowezekana.
 
Itoshe tu kusema kwa sasa kwamba Taifa letu kweli linahitaji mabadiliko makubwa ya kiutawala, linahitaji mabadiliko makubwa sana ya kisera kimfumo na kimuundo, na ni kweli kabisa CCM imeshindwa kuendana na Kasi hii ya uhitaji wa mabadiliko, lakini Bahati mbaya sana watu sahihi wa kufanya Mabadiliko bado hawaonekani, bado Hawapo, Bado wanafanyabiashara ya kisiasa.
 
TAHADHARI.
Nimekuwa nikipokea meseji za vitisho kupitia simu, email na facebook, kuwa nitauawa kama wangwe, ninasema hivi, nipo tayari kwa yote na mwenye uhakika wa kufanya hivyo asipate shida, anipigie simu kwa namba yangu 0762178678 NITAMGUATA ALIPO ATIMIZE LENGO LAKE.
Kwangu Daima NYEUPE NI NYEUPE na NJANO NI NJANO.
Mimi
Habibu Mchange
0762178678
mchangehabibu@yahoo.com