Na Zitto Kabwe
Wiki
ya Machi 18 - 22, 2014 ilianza kwa siku ya Jumanne Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba aliwaslisha rasmi Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge Maalumu la Katiba. Wiki
hiyo imeishia kwa siku ya Ijumaa Rais wa Jamhuri ya Muungano ndugu Jakaya
Mrisho Kikwete kutoa hotuba kwa Bunge Maalumu. Hotuba zote zimepokelewa kwa
hisia tofauti kulingana na msimamo wa kila mtu kuhusu hoja inayoonekana ni
kubwa
kuliko zote katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya - Muundo wa Muungano. Wale wanashabikia muundo wa Serikali Tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya Jaji Warioba. Wale wanaoshabikia muundo wa Serikali mbili walifurahishwa mno na hotuba ya Rais Kikwete. Sikufurahishwa na hotuba zote mbili.
kuliko zote katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya - Muundo wa Muungano. Wale wanashabikia muundo wa Serikali Tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya Jaji Warioba. Wale wanaoshabikia muundo wa Serikali mbili walifurahishwa mno na hotuba ya Rais Kikwete. Sikufurahishwa na hotuba zote mbili.
Nitaeleza.
Moja, hotuba
zote mbili zilichukua muda mrefu zaidi kuelezea sura moja tu ya Rasimu ya
Katiba nayo ni sura ya Sita inayohusu muundo wa Jamhuri ya Muungano kana kwamba
Katiba hii inahusu suala hilo tu. Ni dhahiri suala hili ni kubwa na muhimu
kwani linahusu uhai wa Dola yenyewe na siwezi kubeza. Hata hivyo masuala kama
Haki za Raia ni muhimu zaidi kwani hata uwe na muundo wa namna gani wa muungano
au hata muungano wenyewe kuvunjika, bila ya kuwa na haki za msingi za raia
kwenye katiba katiba hizo zitakataliwa tu na wananchi. Huu mtindo unaozuka wa
kudhani muundo wa muungano ndio mwarobaini wa matatizo ya ufisadi, matumizi
mabaya ya madaraka, ubadhirifu, umasikini, elimu ya hovyo, afya dhaifu,
utatufikisha pabaya na hata kurudi tena kuandika katiba kudai haki hizo. Jaji
Warioba na Rais Kikwete wameshindwa kuruka kiunzi cha kwamba Katiba ni zaidi ya
Muungano.
Pili, wote
wawili Rais Kikwete na Jaji Warioba wamejenga hoja zao kuhusu miundo ya
Muungano wanayopendekeza au kuunga mkono kutokana na misingi ama ya
'malalamiko' au 'hofu'. Jaji Warioba aliorodhesha malalamiko 11 ya upande wa
Zanzibar dhidi ya Muungano na malalamiko 10 ya upande wa bara. Kimsingi
malalamiko yote ya upande wa bara yanazaliwa na vitendo vya upande wa Zanzibar
isipokuwa lalamiko namba vii linalohusu kupotea kwa utambulisho wa Tanganyika
katika muundo wa Muungano.
Jaji
Warioba anajenga msingi wa pendekezo la Tume yake kutokana na kujibu malalamiko
au maarufu kero za Muungano na anasema
"....muundo wa Serikali mbili
hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali mbili waliotuchia waasisi
siyo uliopo sasa...... waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye Serikali
mbili, na siyo Nchi Mbili zenye Serikali Mbili".
Nukuu hii niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee wangu Warioba.
Rais
Kikwete alijenga msingi wa maoni yake kwenye hofu za kuwa na Serikali tatu.
Hofu hizo ni pamoja na gharama za kuendesha Muungano, kuzuka kwa hisia za
Utaifa wa Utanganyika na Uzanzibari, uwezekano wa Muungano kuvunjika kwa
kushindwa kuhudumia majeshi na hata Jeshi kuchukua Nchi ikipidi na kutupilia
mbali katiba na Serikali ya Muungano kutokuwa na Rasilimali zake. Rais alisema
'Serikali ya Muungano ni egemezi na tegemezi' nukuu ambayo niliipenda kuliko zote
katika Hotuba ya Mzee wangu Jakaya Kikwete.
Rais
Kikwete hakuniridhisha kabisa namna ya kumaliza kero za Muungano kwa muundo
uliopo sasa kwani muundo huo umeshindwa kuzimaliza kwa takribani miaka 50 tangu
Muungano uundwe. Haiwezekani muundo uliozalisha kero lukuki ndio utarajiwe
kuzimaliza kero hizo. Kwa vyovyote vile ni lazima kuwa na muundo mpya lakini
kiukweli ni lazima muundo huo mpya ujibu hofu alizoeleza ndugu Rais maana ni
hofu za kweli.
Jaji
Warioba hakuniridhisha na namna suala la Uraia litakavyotatuliwa kwani kutoa
jibu la kubakia na 'kukubali' Nchi mbili halafu uraia mmoja kunaleta mashaka
makubwa. Kama tunataka kuwa na Uraia mmoja ni lazima tuwe Nchi moja, hatuwezi
kuwa na Nchi mbili uraia mmoja.
Vilevile
vyanzo vya mapato ya Muungano ni vidogo mno kuendesha dola. Hivyo basi rasimu
iliyopo mbele ya Bunge Maalumu ina mapungufu makubwa japo imetoa mapendekezo
yatakayomaliza malalamiko ya Muungano.
Sasa
kazi ya Bunge ni moja tu nayo ni kuboresha rasimu iliyopo mbeleyake ili
kumaliza kero za muungano zilizopo na kujibu hoja za hofu za muundo mpya.
Hakuna sababu ya kubishana kwenye takwimu za Tume, tume imefanya wajibu wake na
sasa Bunge Maalumu nalo litimize wajibu wake.
Iwapo
kama kweli tunataka kusikia Watanzania wanataka nini kwenye muundo wa Muungano,
tusimamishe Bunge na twende tukawaulize kwa kura (referendum). Vingivenyo tuboreshe rasimu iliyopo na iliyotokana na
maoni ya wananchi wote kwa kujibu hizo hofu muhimu alizoainisha ndugu Rais na
hayo malalamiko muhimu yaliyoainishwa na Tume. Sio kazi ya Bunge Maalumu
kutafuta ubora wa hotuba zilizotolewa mbele yetu bali kuona mazuri ndani ya
hotuba hizo yasaidie kazi yetu Tuzingatie kuwa tusijenge Nchi kwa kujibu
malalamiko na hofu tu maana hofu na malalamiko hayaishi katika dunia
inayobadilika kwa kasi sana.
Tuamue
tunataka kuwa Jamhuri ya Muungano ya namna gani. Nini sababu ya Jamhuri yetu na
aina gani ya Tanzania tunataka kujenga. Tuanze kwa kutafsiri sababu ya Tanzania
kuwepo na Tanzania gani tunataka kujenga kisha tutunge Katiba itakayowezesha
kutufikisha huko tutakapo kufika.
No comments:
Post a Comment