JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MACHI HADI MEI 2014
Taarifa hii inatoa tathmini ya msimu wa mvua za Vuli
kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2013, mvua zinazoendelea katika maeneo ya
kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na mikoa ya kusini
pamoja na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua za Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei (MAM) 2014.
A. MUHTASARI
Tathmini ya mvua za Vuli katika kipindi cha miezi ya
Oktoba hadi Disemba, 2013 inaonesha
kuwa maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani isipokuwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani
na kanda ya kati ambayo yalipata mvua za chini ya wastani. Kwa ujumla,
mtawanyiko wa mvua hizo haukuwa mzuri hasa kwa maeneo yanayopata misimu miwili
ya mvua. Katika kipindi cha miezi ya Januari hadi Februari, 2014 matukio ya
hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa
na upepo mkali yalijitokeza kama ilivyotarajiwa. Matukio hayo
yalisababisha uharibifu wa mali,
miundombinu pamoja na vifo. Mtawanyiko wa mvua katika maeneo yanayopata msimu
mmoja wa mvua kwa ujumla ulikuwa wa kuridhisha. Aidha, kwa maeneo yanayopata misimu
miwili ya mvua, kulikuwa na vipindi vya mvua za nje ya msimu zilizosababisha
madhara mbalimbali.
Mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei, 2014
unaonyesha kwamba maeneo mengi
yanayopata misimu miwili ya mvua kwa
mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya
Kaskazini) yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Maeneo ya
ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es salaam pamoja na
visiwa vya Unguja na Pemba) yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani. Mvua
zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka
(magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na kusini) zinatarajiwa kuwa za
wastani hadi juu ya wastani.
Viashiria
vikuu vinavyotarajiwa kusababisha
mvua za Masika, 2014 (Machi hadi Mei) ni kuwepo kwa joto la chini ya wastani
katika eneo la mashariki mwa Bahari ya
Atlantiki (Pwani ya Angola) ambalo linatarajiwa kuwepo kwa kipindi chote cha
msimu, joto la wastani hadi juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa
Bahari ya Hindi na kuwepo kwa upepo
wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea nchini hususan katika
kipindi cha miezi ya Aprili na Mei, 2014. Aidha, hali ya joto katika eneo la
ncha ya kusini mwa Bara la Afrika inatarajiwa kudhoofisha mfumo wa mgandamizo
mkubwa wa hewa kusini mwa bara la Afrika hivyo kusababisha upungufu wa mvua za
msimu wa masika katika maeneo
ya ukanda wa Pwani.
B:
TATHMINI YA MVUA ZA VULI OKTOBA HADI DISEMBA, 2013
Mvua za vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba
hadi Disemba 2013, zilikuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo,
baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo ya kati mwa nchi yalipata mvua za
chini ya wastani. Kwa ujumla mtawanyiko wa mvua za msimu wa Vuli haukuwa wa kuridhisha hususan kwa maeneo
mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (Tanga, Arusha na Kilimanjaro). Mvua
zinazoendelea katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua zimekuwa ni za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo yaliyo
mengi. Aidha, maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Pwani, Dar es Salaam pamoja na kaskazini mwa mkoa
wa Morogoro) yamepata mvua kubwa nje ya msimu kwa kipindi cha miezi ya Januari
na Februari 2014. Mvua hizi za nje ya msimu zilizoambatana na matukio ya upepo mkali na mawimbi makubwa
baharini, zilisababisha madhara kama vile vifo, uharibifu wa miundombinu na mali kwa
baadhi ya maeneo. Maeneo yaliyoathirika na mvua hizo ni pamoja maeneo ya wilaya
za Same, Mwanga na Hai katika mkoa wa Kilimanjaro, pia katika baadhi ya maeneo
ya mkoa wa Morogoro ambako mafuriko yalisababisha vifo na uharibifu wa
miundombinu ya barabara na Reli. Vifuatavyo ni viwango vya mvua ilivyonyesha
pamoja na ulinganifu wake kwa wastani wa muda mrefu katika asilimia kwa baadhi
ya vituo nchini:
Maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka:
Pwani
ya Kaskazini: Matangatuani 390.1 mm (81%), Pemba 159.4 mm (57.9%),
Amani 573.9 mm (110.9%), JNIA 184.6 mm (59.0%),
Zanzibar 338.9 mm (53.2%) na Morogoro 151.3mm (77.0%) za mvua.
Nyanda
za Juu Kaskazini Mashariki: Moshi 124.6 mm (89.4%), Arusha 222.8 mm (103.1%),
Lyamungo 195.9 mm (91.8%), Same 130.0 mm (78.6%) and KIA 129.3 mm (118.3%) za
mvua.
Kanda
ya Ziwa Viktoria: Mwanza 365.4 mm (95.8%), Bukoba 501.5 mm (90.4%), Musoma
154.4 mm (63.4%) and Shinyanga 274.7 mm (93.9%) za mvua.
Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Magharibi: Tabora 394.3 mm
(115.2%), Kibondo 369.4 mm (92.5%), Tumbi 361.8 mm (107.5%) and Kigoma 440.3 mm
(113.7%) za mvua.
Kanda
ya Kati: Dodoma 88.5 mm (58.4%), Hombolo 68.2 mm (40.7%) and Singida 135.3 mm
(63.9%) za mvua.
Nyanda
za Juu Kusini Magharibi: Iringa 77.9 mm (53.0%), Mbeya 228.2 mm (87.5%), Tukuyu
386.7 mm (87.1%), Sumbawanga 273.0 mm (91.0%), Mahenge 536.3 mm (109.1%) and Igeri 345.4 mm (104.9%) za mvua.
Maeneo
ya Kusini: Mtwara 149.8 mm (62.9%), Naliendele 117.8 mm (43.6%) Kilwa 58.6 mm (24.6%) and Songea 298.2 mm
(124.7%) za mvua.
Angalizo: Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya
wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani; asilimia 75 hadi
125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125
hutafsiriwa kama juu ya wastani.
C: MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mwelekeo huu umezingatia hali ya mifumo ya hali ya hewa
iliyopo, inayotarajiwa na athari zake kwa msimu ujao wa mvua za Masika
(Machi hadi Mei, 2014).
Uchambuzi wa hali ya joto la bahari unaonesha ongezeko la
joto katika maeneo ya kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi ambalo linatarajiwa
kuendelea kuongezeka kwa kipindi chote cha msimu. Wakati huo huo, joto la wastani linatarajiwa
katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi na Pasifiki wakati wa msimu. Kwa
upande mwingine, joto la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo kwa
kipindi chote cha msimu katika maeneo ya mashariki mwa Bahari ya Atlantiki.
Hali ya joto la bahari lililopo na linalotarajiwa kuwepo, linategemewa
kusababisha ongezeko la upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo
kuvuma kuelekea katika maeneo ya magharibi na kati ya nchi hususani katika
miezi ya Aprili hadi Mei, 2014.
Joto la juu ya wastani iliyopo katika maeneo ya ncha ya
kusini mwa bara la Afrika inatarajiwa kuendelea kuwepo katika kipindi cha Machi
hadi Mei, 2014, hali hii inatarajiwa kusababisha mifumo ya migandamizo mikubwa
ya hewa iliopo katika maeneo hayo kuwa hafifu. Hali hii inatarajiwa kudhoofisha
ukanda wa mvua (ITCZ) katika maeneo ya Pwani ya nchi yetu, hivyo kupelekea
kuwepo kwa upungufu wa mvua katika msimu wa masika. Hata hivyo, kuelekea
mwishoni mwa msimu, upepo unaovuma kutoka mashariki unatarajiwa kuimarika na
hivyo kuwa na uwezekano wa kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika
maeneo ya Pwani.
D:
MWELEKEO WA MVUA: MACHI HADI MEI (MAM), 2014
(i)
Mvua za Masika
Maeneo ya kaskazini mwa nchi
yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya
kwanza ya mwezi Machi, 2014. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
Kanda
ya Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera,Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya
kwanza ya mwezi Machi katika mikoa ya Kagera na Geita na kusambaa katika maeneo mengine ya mikoa ya
Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu wiki ya pili ya mwezi Machi. Maeneo haya
yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, isipokuwa maeneo ya mashariki mwa
mkoa wa Mara ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani.
Ukanda
wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro pamoja na
Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na
ya tatu ya mwezi Machi, 2014 na zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi
wastani isipokuwa maeneo yaliyopo magharibi mwa mkoa wa Morogoro ambayo
yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda
za juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili hadi
ya tatu ya mwezi Machi, 2014. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu
ya wastani katika maeneo mengi isipokuwa kwa baadhi ya maeneo yaliyoko
mashariki mwa mkoa wa Kilimanjaro ambapo mvua za chini ya wastani zinatarajiwa.
(ii)
Mvua za Msimu
Kanda
ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi):
Mvua zinazoendelea katika maeneo hayo
zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla, hata hivyo mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika
maeneo ya kaskazini mashariki mwa mkoa wa Tabora. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha
wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2014.
Kanda
ya Kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinazoendelea kunyesha katika
maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani. Msimu wa mvua
unatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2014.
Ukanda
wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi):
Mvua zinazoendelea kunyesha
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya kaskazini
mashariki mwa mkoa wa Lindi ambapo mvua za chini ya wastani zinatarajiwa. Msimu
wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2014.
Maeneo
ya kusini (mkoa wa Ruvuma):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na
zinatarajiwa kuwa za wastani na zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa wiki ya pili
ya mwezi Aprili, 2014.
Nyanda
za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Katavi):
Mvua zinazoendelea kunyesha
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya mkoa wa
Njombe ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani. Mvua hizo zinatarajiwa
kuisha katika wiki ya kwanza ya mwezi
Mei, 2014.
Angalizo: Vipindi vifupi vya mvua
kubwa ni matukio ya kawaida hata katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu
wa mvua. Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa
mifumo ya hali ya hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa
taarifa kuhusiana na mwelekeo wa mvua nchini pamoja na kutoa tahadhari kila
inapobidi.
Kielelezo: Matarajio na mwelekeo wa mvua za Machi hadi Mei 2014
Rangi
katika ramani inaonesha matarajio ya mvua kuwa katika madaraja matatu:juu ya
Wastani, Wastani na chini ya Wastani. Namba ya juu inaonesha uwezakano wa mvua
kuwa juu ya Wastani, ya kati inaonyesha mvua kuwa za Wastani na ya chini
inaonyesha uwezekano wa mvua kuwa za
chini ya wastani. Mfano: rangi ya kijani iliyokolea katika maeneo ya Ziwa
Victoria na maeneo kusini magharibi ni asilimia 40 juu ya wastani, Wastani ni
asilimia 35 na chini ya Wastani ni
asilimia 25.
E: ATHARI NA USHAURI
Kilimo
na Usalama wa Chakula
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa
na unyevunyevu wa kutosha wa udongo isipokuwa maeneo ya ukanda wa pwani na
baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na visiwa vya
Unguja na Pemba ambayo yanatarajiwa kuwa na upungufu. Katika maeneo ya Ukanda wa
Ziwa Victoria (mikoa ya Mara, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Geita na Simiyu pamoja
na maeneo ya Morogoro), wakulima
wanashauriwa kuendelea na taratibu za kwaida za shughuli za kilimo. Hata hivyo,
mvua za juu ya wastani zinaweza kusababisha unyevunyevu wa kupitiliza unaoweza
kuathiri mazao, hivyo wakulima wanashauriwa kufuata ushauri wa wataalam wa
kilimo.
Katika maeneo ya pwani ya kaskazini
(mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba),
Wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.
Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua
kwa mwaka (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Dodoma, Iringa, Lindi,
Mtwara pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa Morogoro), hali ya unyevunyevu wa
udongo inatarajiwa kuwa ya kutosheleza,
hivyo wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za kilimo. Hata
hivyo, mvua za juu ya wastani katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya (Singida, Mbeya,
Njombe na maeneo ya Ruvuma) zinaweza kusababisha unyevunyevu wa kupitiliza
unaoweza kuathiri mazao na shughuli za uvunaji.
Nishati
na Maji
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata
mvua za juu ya wastani, vina vya maji katika maziwa, mabwawa na mito vinatarajiwa
kuongezeka katika kipindi cha msimu wa Machi hadi Mei. Aidha miundombinu ya
kuhifadhi maji iboreshwe kwa wakati ili kusaidia uvunaji wa maji katika kipindi
cha mvua hizi. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani,
mbinu za kuvuna na kuhifadhi maji zizingatiwe.
Malisho na Maji kwa ajili ya Mifugo na Wanyamapori
Hali ya malisho na maji inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi ya
nchi isipokuwa maeneo machache ya ukanda wa pwani ambayo yanatarajiwa kuwa na
mvua za chini ya wastani. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chini ya wastani wafugaji
wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi wakati wa kiangazi
na kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa
mifugo katika maeneo yao. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na juu
ya wastani uoto, bioanuai, maua na upatikanaji wa asali na nta vinatarajiwa
kuimarika. Aidha, mvua hizo zitasaidia kupunguza kuhama kwa wanyamapori na migogoro baina ya wanayamapori na wananchi.
Mamlaka
za Miji
Katika kipindi cha msimu wa Machi hadi
Mei, vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini, hivyo mamlaka
za miji zinashauriwa kuchukua tahadhari stahiki ikiwa ni pamoja na kusafisha miundo
mbinu ya maji taka na mitaro ili kupunguza athari za maji kutuama na mafuriko. Pamoja
na matarajio ya mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya ukanda
wa pwani na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, kuna uwekano
wa kutokea vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo hayo. Hivho tahadhari
stahiki zichukuliwe.
Sekta
ya Afya
Kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu na chini ya wastani
kuna uwezekano wa milipuko ya magonjwa kama vile malaria, kipindupindu, kuhara
damu na homa za matumbo. Hivyo, jamii na mamlaka husika zinashauriwa
kuchukua tahadhari na maandalizi stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza
kujitokeza.
Mipango
Sekta mbalimbali za uchumi na
kijamii zinashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa mvua za msimu wa masika,
2014 katika mipango inayoandaliwa ya utekelezaji na ufanikishaji wa shughuli za
taasisi sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Menejimenti
za Maafa
Taasisi za maafa na wadau wa sekta husika,
wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya kukabiliana na majanga ya
hali ya hewa yanayoweza kuathiri jamii na shughuli za kiuchumi.
Mamlaka inawashauri watumiaji
wa taarifa za hali ya hewa waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI
MKUU
No comments:
Post a Comment