Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Massawe akiwasha moja ya zana za kilimo zilizotolewa na mradi wa DASIP.
Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha kilimo kwa
wananchi wa mkoa wa Kagera kwa kutoa vifaa vya kisasa vya kilimo kupitia mradi
wa uwekezaji katika sekta ya kilimo Wilayani (District Agricultural Sector
Investment Project – DASIP)
Serikali kupitia Mradi wa DASIP
imetoa zana za kisasa za kilimo na vifaa
mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha kisasa na chenye tija katika
Halmashauri saba za Wilaya za Mkoa wa Kagera ili ziweze kuinua uchumi wa
wananchi wake kupitia kilimo cha kisasa.
Zana na vifaa vilivyotolewa na
serikali kupitia mradi wa DASIP mkoani Kagera
ni matrekta madogo (Powertllers)manne,
Mashine za kupandia mpunga (Transplanters) 4, Kasiki (Cash boxes) 18 za
kutunzia fedha kwenye SACCOS vijijini, na Kompyuta 6 kwaajili yakutunzia
kumbukumbu za kilimo za wakulima.
Gharama ya zana na vifaa hivyo vya
kilimo kwa jumla ni shilingi milioni 174,000,000/= vikiwa na mchangunuo
ufuatao, trekta ndogo 4 za kilimo kila moja sh 5,000,000/=, Mashine za kupandia
mpunga 4 kila moja sh 13,000,000/=,
Kompyuta 6 kila moja sh 2,000,000/= na kasiki 18 kila moja sh 500,000/=.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe
Massawe akikabidhi zana na vifaa vya kilimo kwa Wakurugenzi watendaji wa
halmashauri aliishukuru serikali kutoa
zana hizo za kisasa ambazo zitawafanya wakulima wa mkoa waKagera kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na
biashara kwa wakati muafaka.
Aidha kutokana na mradi wa DASIP
kuonyesha mafanikio makubwa mkoani Kagera Mhe. Massawe aliiomba serikali kuongeza
muda wa mradi huo ambao ulianza mwaka 2006 na kumaliza muda wake mwezi desemba
2013.
“Kama ilivyo miradi mingine mfano
TASAF naiomba serikali kuongeza muda wa mradi huu wa DASIP au serikali ifikirie
kuanza DASIP II ili kunufaisha wananchi walio wengi mkoani kwetu Kagera kwani
mradi huu umekuwa wa tija kwa wakulima wetu,” Alitoa wito Mhe Massawe.
Katika hatua nyingine Mhe.
Massawe aliwaasa Wakurugenzi kuhakikisha zana hizo zinakwenda kwa wakulima walengwa
ili wazitumie na kuzifanya halmashauri za wilaya kujiongezea mapato ya ndani
kupitia kilimo.
Lengo la mradi wa DASIPlilikuwa
ni kuchangia katika kupunguza umasikini vijijini kwa kuongeza uzalishaji na
tija katika kilimo hatimae kuongeza patola mkulima na uhakika wa chakula katika
kaya, aidha, DASIP ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza sekta na
mipango ya kilimo.
Mradi wa DASIP ulikuwa unafanya
kazi katika sehemu kuu nne ambazo ni Uimarishaji wa uwezo wa wakulima, Uandaaji wa mipango ya maendeleo ya kilimo na
uwekezaji katika kilimo, Uimarishaji wa vyama vya kuweka na kukopa pamoja na
masoko na mwisho ni Uratibu wa mradi wenyewe.
Halmashauri za Wialaya za mkoa wa
Kagera zilizonufaika na vifaa vya kilimo kutoka katika mradi wa DASIP ni Bukoba, Biharamulo, Chato (Mkoa mpya
wa Geita), Karagwe, Missenyi, Muleba na Ngara. Aidha, halmashauri hizo zimeingiza miradi ya
DASIP katika bajeti za kila mwaka ili kuhakikisha shughuli zote zilizokuwa
zikifanywa na DASIP zinaendelea na kwa ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment