Monday, March 24, 2014

Shuguli ya kuitafuta MH370 yasitishwa


Jamaa za abiria wa ndege hiyo wamekumbwa na majonzi makubwa.
Mamlaka ya usalama wa safari za baharini nchini Australia imesema kuwa operesheni ya kuitafuta ndege ya shirika la Malaysia iliyotoweka imesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa na mawimbi makali baharini.
Taarifa zinasema kuwa upepo mkali pamoja na mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo ina maana kuwa ndege hazitoweza kupaa kwa usalama. Mawimbi makali yameilazimisha meli ya jeshi la wanamaji wa Australia kuondoka katika eneo ambalo mabaki yanayodhaniwa kuwa ya ndege hiyo yalionekana hapo jana Jumatatu.
Dr Erik van Sebille, ambaye ni mtaalam wa maswala ya Baharini katika chuo kikuu cha New South Wales mjini Sydney, amefanya utafiti katika eneo hilo la kusini mwa Bahari Hindi kutambua ni wapi na vipi vifusi vinasafirishwa na mawimbi ya bahari. Anasema itakuwa vigumu sana kupata mabaki ya ndege hiyo.
Shughuli ya kuitafuta MH370 imesitishwa
" Ni eneo lisiloweza kukalika duniani, acha niseme. Upepo unaovuma ni mkali sana, mawimbi ni makubwa, ni mojawepo wa mawimbi makubwa zaidi baharini. Unapofika katika eneo hili la kusini, unaanza kuhisi athari za eneo la Antactica kwenye bahari. Hapa tunazungumzia dhoruba kali kali sana hususan wakati huu tunapoingia majira ya kupukutika," anasema Dr. Erik van Sebille.
Kadhalika amesema kuwa vifusi vilivyoenekana hapo jana tayari vimekwishaondolewa katika eneo hilo na mawimbi makali.
"Haitakuwa rahisi kabisa kupata kijisanduku cha kunasa habari. Mawimbi ya eneo hili ni makali na kwa hiyo vifusi ambavyo wametambua kwa sasa huenda vimehamishwa katika kipindi cha majuma mawili au matatu tangu ndege hiyo ianguka-na huenda vimesafiri kilomita alfu moja tayari. Na hii inaifanya vigumu kurejelea utafutaji kwa sababu bahari inabadilika sana hapa-ina vurugu ukipenda."
Hapo awali naibu waziri wa mashauri ya nchi za Kigeni wa China Xie Hangsheng, aliitaka serikali ya Malaysia kutoka ushahidi unaoelezea kuwa ndege hiyo ilianguka katika eneo la Kusini mwa bahari Hindi. Ndege hiyo ilitoweka kwenye mtambo wa Radar zaidi ya majuma mawili yaliyopita.

No comments:

Post a Comment