Awabeza
wanaoupinga. Asema ni mawakala wa ukoloni na wapinga mapinduzi.
Naibu Kaibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi upande wa Zanzibar, ndugu Vuai
Ally Vuai ameeleza kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kudumisha muungano ulioasisiwa
na muasisi wa Serikali ya mapinduzi na Chama cha ASP Marehemu Abeid Amani
Karume.
Mheshimiwa Vuai ameyaeleza hayo katika
Kongamano la kumuenzi muasisi wa Mapinduzi-marehemu Mzee Abeid Amani karume
lililoandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
chini ya mwenyekiti wake Ndugu Sadifah Juma, lililofanyika katika Ukumbi wa
chuo cha Ufundi Karume, Mbweni Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi
wa Umoja huo akiwemo Katibu Mkuu wa UVCCM, ndugu Martine Shigela, Makatibu wa
Idara za UVCCM na maafisa wengine wa Makao Makuu Bara na Zanzibar, na wajumbe
wengine 600 kutoka katika Mikoa mbalimbali ya Zanzibar, pamoja na wawakilishi
kutoka vyuo vikuu.
Katika Nasaha zake na salamu za ufunguzi wa
Kongamano hilo, Mheshimiwa Vuai alifafanua umuhimu wa kuwaenzi waasisi wa
muungano na kusema kuwa vijana wana wajibu wa kutafakari na kujifunza kutokana
na viongozi wao waliopita, wajifunze ujasiri, uzalendo na kusimamia misingi ya
umoja na utaifa. Alisema kuwa Mapinduzi
yalikuwa ni halali kwa kuwa Serikali iliyopinduliwa ilikuwa ni Serikali chini
ya Sultan ikinufaisha wachache, hivyo Mapinduzi yalilenga kuleta utawala ulio
huru wa watu wa Zanzibar, yalilenga kutetea Uafrika yakiongozwa na mioyo ya
kizalendo na nia ya kuijenga Zanzibar na kunufaisha wengi katika wazanzibar
wenyewe.
Alisisitiza kuwa muungano una manufaa
makubwa kwa wanzanzibar akitolea mifano ya manufaa yanayopatikana katika sekta
mbalimbali za kimaendeleo na kijamii ambapo alianza kwa kutaja manufaa
yanayopatikana katika sekta ya Elimu ambapo alitaja kuwa kupitia muungano ,
wanafunzi takribani 1251 waliweza kupatiwa mikopo ya elimu ya juu chini ya bodi
ya mikopo ya wanafunzi (HESLB) ikiwa ni wanafunzi si zaidi ya mia nane na
sitini (860) ndio ambao waliweza kupatiwa mikopo na Serikali ya Mapinduzi hii
ni kulingana na bajeti na uwezo wa Serikali ya mapinduzi.
Lakini pia, Mheshimiwa Vuai alitaja fursa
katika sekta ya afya, ambapo akasema kuwa wagonjwa mbalimbali ambao wamekuwa na
matatizo makubwa na yanayohitajia utaalamu zaidi wamekuwa wakipelekwa katika Hospitali Kuu ya rufaa ya Muhimbili
kama walivyo watanzania wengine kwa gharama ya chini sawa na watanzania
wengine, na akasisitiza haya yanapatikana chini ya kivuli cha muungano. Akaeleza
pamoja na fursa hii kuwepo kwa fursa nyingine za makazi, biashara n.k.
Pamoja na kufafanua juu ya faida na manufaa
hayo Mheshimiwa vuai alisema kuwa ni kweli kuwa zipo kero mbalimbali katika
muungano, ambapo akasisitiza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha
Mapinduzi (NEC) imejadili na kutoa fursa kwa kero hizo kujadiliwa na kutafutiwa
ufumbuzi. Mheshimiwa Vuai alisema kama tatizo ni kujiunga na OIC, NEC ya CCM
imetoa fursa ya kulijadli hilo na kuruhusiwa ikionekana inafaa, ama ikiwa kero
ni mapato ya Bandari, ama mafuta ama takwimu basi NEC imetoa fursa ya
kuyajadili haya na ikionekana inafaa yatolewe katika muungano, na pia kulibainisha
suala la mahusiano ya kimataifa na suala la Zanzibar kujiunga na Umoja wa
Visiwa Duniani.
Akasisitiza kuwa vijana wasiwe tayari
kufuata mawazo ya wapinga mapinduzi na wapinga muungano kwani hao ni watu
wanaotaka kurudisha ukoloni kwa mlango wa nyuma, kwa kuwa wanapinga muungano
bila ya kuwa na sababu za msingi wala hoja.
“..wakiulizwa kwanini hamtaki muungano hali ya
kuwa imetolewa nafasi ya kujadili kero na kasoro zilizopo katika muungano ili
uwe bora zaidi na wenye manufaa zaidi, wapinga muungano husema tu kuwa hatutaki
muungano, lakini sisi wanaotuita wahafidhina tunajua kuwa wao ni mawakala wa
ukoloni na wapinga mapinduzi..” alisema Mheshimiwa Vuai.
Pamoja na kuelezea kwa kina suala la
muungano, Mheshimiwa Vuai aliwakumbusha Vijana juu wajibu na jukumu lao la
kushiriki katika uchaguzi wa wajumbe wa mabazara ya katiba na kutumia haki yao
hiyo ya kidemokrasia.
Kongamano hilo la siku moja lilimalizika
saa 12: 15 jioni, ambapo mada mbalimbali kama Mchango wa Marehemu Karume katika
Ukombozi wa Zanzibar iliyofikishwa na Ndugu Haji Machano Haji pamoja na mada ya
Fursa za Kielimu, Kiuchumi na Kijamii, zilizopatikana baada ya Mapinduzi
Matukufu ya January 12, 1964 iliyowasilishwa na Haroun Suleiman (MNEC) na Mada
ya Mwisho kuwasilishwa ikiwa ni DHANA YA MAPINDUZI YA JANUARY 12, 1964 na
kwanini yalifanyika ikiwasilishwa na Ramadhan A. Ramadhani (MNEC).
Wajumbe wa Kongamano hilo wanategemea
kuhudhuria shughuli ya Kumbukumbu ya Marehemu Mzee Karume zitakazofanyika kesho
Jumapili tarehe 07 April 2013, katika Afisi kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
iliyopo kisiwandui Zanzibar.
No comments:
Post a Comment