Saturday, April 06, 2013

MWENYEKITI WA UVCCM TAIFA ATOA MSAADA KWA WAJASILIAMALI


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na mbunge wa jimbo la Donge Mheshimiwa Sadifah Juma, amefanya mkutano wa hadhara jimboni humo ambapo amechangia takribani shilingi milioni 4, ikiwemo pesa taslimu shilingi milioni tatu na laki mbili (3,200,000) pamoja na vifaa vya ushoni vyenye thamani ya shilingi milioni 1 kwa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali vya jimboni Donge.

Sadifah amechangia kiasi hicho kwa vikundi 12 vya ujasiriamali ambapo vikundi 4 vya ufugaji wa kuku wa kisasa vilipatiwa kiasi cha shilingi laki 300,000 kila kimoja,vikundi hivyo ni Inshaallah Hatuchoki, Letu moja , Sisi kwa sisi na kikundi cha Mkorofi si mwenzetu. Mbali na vikundi hivyo pia vikundi vya utengenezaji matofali, vikundi vya ushonaji na vikundi vya kukopeshana vilinufaika na michango ya Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Sadifah.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kutoka Makao Makuu ya Jumuiya hiyo wa afisi kuu ya Zanzibar na Dar es salaam wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja huo Ndugu Shigela Martine, Makatibu wa Idara za Jumuiya hiyo na maafisa wa Makao Makuu, Mheshimiwa Sadifah ameichangia timu ya mpira wa miguu ya Kata ya Vijibweni-mahonda vifaa vya michezo.

Mbali na michango hiyo ya fedha taslimu na nyenzo za kimaendeleo, Mhe. Sadifah amesisitiza vijana wa jimbo hilo kujituma kwa hali na mali katika kujiletea maendeleo binafsi na pia kushiriki katika shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo, akasisitiza kuthamini na kuvitunza vifaa vlivyotolewa katika vikundi hivyo na kuvitumia ipasavyo ili viweze kuwa msaada endelevu kwa vikundi hivyo.

Nae, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndugu Martine Shigela aliwasisitiza Vijana kuwa msitari wa mbele katika kushiriki shughuli mbalimbali za mendeleo na kuwa mfano bora wa kufanikisha na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini pia akawaahidi Vijana wa jimbo hilo kuwa Jumuiya ya Vijana itawasaidia katika kuwapa mafunzo ya ujasiriamali ambayo Jumuiya hiyo inayatoa kwa vijana mbalimbali hapa nchini ili kuwawezesha kushiriki shughuli za kimaendeleo na ujasiriamali kwa uhakika na ufanisi zaidi. 

Mheshimiwa Sadifah yupo jimboni humo katika ziara mbalimbali za kumuenzi muasisi wa Mapinduzi-Marehemu Abeid Aman Karume, aliyefariki tarehe 06th April 1972, ambapo kilele cha maazimisho ya kumbukumbu hizo yatafanyika katika afisi kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyopo kisiwandui mjini unguja kesho Jumapili tarehe 07th April 2013.

No comments:

Post a Comment