Naibu
Katibu Mkuu CHADEMA, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa
Fedha na Uchumi ndugu Zitto Kabwe ameanza ziara ya mikoa ya kanda ya Magharibi
ya Katavi, Tabora na Kigoma.
Lengo la ziara ni kukagua uhai wa CHADEMA,
kuhamasisha ujenzi wa chama vijijini na kueneza sera za CHADEMA katika
kumkomboa Mtanzania.
Naibu
Katibu Mkuu atafafanua juhudi za CHADEMA katika kuleta mabadiliko nchini na
hasa mabadiliko ya sheria mama ya nchi KATIBA ikiwemo na hoja mbalimbali ambazo
CHADEMA inataka ziwemo kwenye Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwemo Haki ya wananchi kuwa na sauti katika umiliki wa rasilimali, haki ya
elimu bora na bure, afya bora na haki ya hifadhi ya jamii.
Naibu
Kiongozi wa Upinzani ataelezea juhudi ambazo CHADEMA imefanya Bungeni katika
kuisimamia Serikali kupitia hoja mbalimbali za wabunge. Hii ni pamoja na
kupambana na ufisadi kwa mfano utoroshaji wa fedha nje na kupambana dhidi ya
uporaji wa Ardhi ya wananchi.
Waziri
Kivuli wa Fedha atafafanua namna sera mbovu za CCM zinavyoendeleza umasikini wa
wananchi wa vijijini na kueleza namna gani sera za CHADEMA zinazolenga kukuza
uchumi wa vijijini zitakavyowezesha kutokomeza umasikini kwa kuwekeza vya
kutosha katika miundombinu na huduma za kijamii za vijijini.
Mara
baada ya kumaliza ziara ya Kanda ya Magharibi na kukamilisha baadhi ya Majukumu
ya kibunge na kimataifa katika kupambana na utoroshaji wa Fedha kutoka Afrika,
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni ataendelea na ziara katika mikoa mingine na
hasa kanda za Ziwa na Kusini.
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini
Jumamosi, 5 Oktoba 2013, Dar-es-Salaam
No comments:
Post a Comment